Friday, January 04, 2008

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikagua shamba lake la mananasi yaliyopandwa kwa ustadi mkubwa na kwa kuzingatia vipimo vya kitaalam hyuko Kiwangwa Bagamoyo jana.
Picha na Freddy Maro toka: jakayakikwete.com

JK ateta na Kibaki

na Waandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete ameanzisha mazungumzo ya moja kwa moja na Rais Mwai Kibaki wa Kenya, katika jitihada za kumaliza vurugu zilizoibuka nchini humo, kutokana na mabishano ya matokeo ya uchaguzi mkuu.

Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana, ilisema kuwa Kikwete pia amekuwa na mazungumzo na Raila Odinga, mgombea wa Chama cha ODM na Kalonzo Musyoka, mgombea wa Chama cha ODM-Kenya, na wanasiasa wengine mashuhuri wa nchi hiyo.

“Vile vile amekuwa na mashauriano na viongozi wengine wa Afrika na dunia akiwemo Rais wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Thabo Mbeki na Dk. Asha-Rose Migiro, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa juhudi zinazofanywa na Rais Kikwete na viongozi wenzake ni kutaka kuona kuwa matatizo yanayoikabili Kenya hivi sasa yanatatuliwa kwa njia ya mazungumzo.

Wakati huo huo, baadhi ya wazazi wenye watoto wanaosoma nchini Kenya wameeleza kuwa wanahangaika kuwapata watoto hao ambao wamekwama nchini humo kutokana na vurugu zinazoendelea.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba hivi sasa hakuna usafiri wa kuweza kuwarejesha watoto hao, kwani Jeshi la Polisi mkoani Arusha limezuia kwa muda safari za mabasi kati ya Tanzania na Kenya.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa wazazi hao, baadhi ya matajiri na raia wa nchi hiyo wamekimbilia na kuingia nchini kwa kasi.

Vyanzo vya habari mbalimbali vililieleza gazeti hili juzi na jana kwamba baadhi ya matajiri hao wameanza kuingia nchini Jumapili na kwa sasa wanaishi kwenye hoteli kadhaa jijini Dar es Salaam.

Chanzo kimoja ambacho kinafanya kazi kwenye hoteli moja iliyopo eneo la Kigamboni, kililiambia gazeti hili kwamba matajiri wengi hivi sasa wanaishi kwenye hoteli za kitalii zilizopo Kigamboni.

Wakati huo huo, habari kutoka Arusha zinaeleza kuwa machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Kenya, yamesababisha kushuka kwa mapato yanayotokana na utalii katika mkoa huo.

Hali hiyo imezikumba kampuni mbalimbali za utalii kutokana na wageni wengi wanaotoka nchi za Ulaya kuamua kuahirisha safari zao kutokana na mauaji yanayoendelea Kenya kuwatia hofu ya usalama wao.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO), Mustafa Akunai, alisema hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kufutwa kwa safari nyingi za ndege nchini Kenya.

Akunai alisema asilimia 40 ya watalii wote wanaofika hapa nchini hushuka nchini Kenya katika Uwanja wa Kenyata na makampuni ya utalii kuwafuata wageni hao nchini humo kuja kuanza ziara ya utalii hapa nchini.

Katika hatua nyingine, wageni wengi raia wa Kenya, hususan wenye asili ya Kiasia, wameingia kwa wingi mjini Arusha tangu kuanza kwa vurugu nchini Kenya.

Wakenya hao jana majira ya saa 12 jioni walikutana katika eneo la wazi jirani na jengo la CCM Mkoa wa Arusha wakiwa na majadiliano ya wao kwa wao.

Jitihada za kumpata Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Arusha, Kabugumira, zilishindikana lakini mmoja wa maofisa wake aliyekuwepo ofisini hapo alisema wageni wengi wanaoingia hivi sasa kutoka nchini Kenya wanaingia kihalali.

Aidha, inaelezwa kuwa zaidi ya Wakenya 343 wakiwemo wanawake na watoto wameripotiwa kuingia mkoani Tanga juzi kutokana na vurugu zinazoendelea nchini mwao.

Inaripotiwa kuwa magari mawili aina ya Toyota Hiace, yakiwa na raia 17 wa nchi hiyo, yalikamatwa na kurudishwa Kenya yalipojaribu kuingia nchini kinyemela.

Akizungumza na gazeti hili, Naibu Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Tanga, Epafra Masaki, alikiri kuongezeka kwa raia wa Kenya wanaoingia nchini katika siku za hivi karibuni.
Wakati huo huo, Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema) kinatarajia kufanya maandamano ya amani kuunga mkono harakati za wapenda amani nchini Kenya.

Maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika Dar es Salaam kesho, yatashirikisha wafuasi na viongozi wa vyama vyote vya siasa na wapenda maendeleo nchini.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, Erasto Tumbo, maandamano hayo ni kulaani mauaji yanayoendelea nchini Kenya.

Pia Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (UAMSHO) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maimamu (JUMAZA) zimelaani mauaji hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar, Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Muhdin Zubeir Muhdin, alisema mauaji hayo yamepoteza maisha ya wananchi wengi wakiwemo kina mama na watoto wadogo wasio na hatia.

Taarifa hii imeandaliwa na Irene Mark, Happiness Katabazi, Anna Makange, Tanga, Ramadhani Siwayombe, Arusha na Saada Said, Zanzibar.

Kutoka Tanzania Daima.

No comments: