Thursday, January 10, 2008


Rais Kikwete amfukuza kazi

Daudi Balali.


na Irene Mark

SEHEMU ya tuhuma za ubadhirifu ndani ya Benki Kuu (BoT) zilizotolewa na wapinzani, zimebainika kuwa ni kweli na Rais Jakaya Kikwete amemfukuza kazi Gavana wa BoT, Daudi Balali, kutokana na ubadhirifu huo.

Kufukuzwa kazi kwa gavana huyo ambaye kwa sasa anaelezwa kuwa yupo nchini Marekani kwa matibabu, kunatokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kusikitishwa na kukasirishwa kwa Rais Kikwete, na ugunduzi wa kuwapo kwa ukiukwaji wa makusudi wa sheria, kanuni na taratibu za uuzaji wa madeni kwenye Akaunti ya Madeni ya Malipo ya Nje (EPA).

"Baada ya kuipitia taarifa ya Mdhibiti Mkuu wa Serikali na mkaguzi wa nje, yaani Kampuni ya Ernst & Young, Mhe. Rais amesikitishwa na kukasirishwa sana na taarifa za kuwepo vitendo vya ukiukwaji wa makusudi wa sheria, kanuni na taratibu za uuzaji wa madeni ya nje vilivyofanywa katika taasisi muhimu na nyeti kama vile Benki Kuu," alisema Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo wakati akisoma tamko rasmi la serikali mbele ya wanahabari jana.

Luhanjo alisema Rais Kikwete amemwondoa Balali katika nafasi hiyo na mara moja amemteua Profesa Benno Ndulu, aliyekuwa Naibu Gavana kuchukua nafasi ya Balali ambaye amekuwa akiandamwa na tuhuma nzito za ubadhirifu tangu katikati ya mwaka jana.

Katika tamko hilo linaloweza kuchukuliwa kuwa ni ushindi kwa wapinzani ambao wamekuwa wakishinikiza kuwapo kwa ubadhirifu mkubwa ndani ya BoT, Luhanjo alisema uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha hizo ulifanywa na kampuni ya kimataifa ya ukaguzi ya Ernst & Young.

Kwa mujibu wa Luhanjo, hasira hizo za Rais Kikwete zinatokana na kubainika kuwa, kampuni 22 zililipwa zaidi ya sh bilioni 133 isivyo halali kupitia akaunti ya EPA.

"Uchunguzi umebaini kuwa, jumla ya sh 133,015,186,220.74 zililipwa katika kampuni 22 zisizokuwa na nyaraka, ama zenye nyaraka batili na nyingine usajili wake haupo kwa Msajili wa Makampuni (BRELA)," alisema Luhanjo.

Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Bencon International Ltd, VB & Associates Company Ltd, Bina Resorts Ltd, Venus Hotel Ltd, Njake Hotel &Tours Ltd, Maltan Mining Company Ltd, Money Planners & Consultants na Bora Hotels & Apartment Ltd.

Kampuni nyingine ni B.V. Holdings Ltd, Ndovu Soaps Ltd, Navy Cut Tobacco (T) Ltd, Changanyikeni Residential Complex Ltd, Kagoda Agriculture Ltd, G&T International Ltd, Excellent Services Ltd, Mibane Farm, Liquidity Services Ltd, Clyaton Marketing Ltd, M/S Rashtas (T) Ltd, Malegesi Law Chambers (Advocates, Kiloloma and Brothers na KARNEL Ltd.

Aidha, miongoni mwa fedha hizo, kiasi kingine kinachofikia sh 90,359,078,804 kililipwa kwa kampuni nyingine 13 zilizotumia kumbukumbu, nyaraka na hati za kughushi.

Taarifa hiyo ya maandishi ya Luhunjo ilizitaja kampuni hizo 13 ambazo hazikustahili kulipwa kiasi chochote cha fedha ni; Bencon International Ltd of Tanzania, VB & Associates Company Ltd of Tanzania, Bina Resorts Ltd of Tanzania, Venus Hotel Ltd, Njake Hotel &Tours Ltd, Maltan Mining Company Ltd, Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment Ltd, Ndovu Soaps Ltd, Navy Cut Tobacco (T) Ltd, Changanyikeni Residential Complex Ltd na Kagoda Agriculture Ltd.

Aidha, ukaguzi huo ulibaini kuwepo kwa kampuni tisa zilizolipwa jumla ya sh 42,656,107,417, fedha ambazo hazikustahili kulipwa kwa sababu hazikuwa na nyaraka zilizoonyesha stahili za malipo hayo, hali iliyowafanya wakaguzi washindwe kuhakiki uhalali wake.

Alizitaja kampuni hizo kuwa ni; G&T International Ltd, Excellent Services Ltd, Mibane Farm, Liquidity Service Ltd, Clayton Marketing Ltd, M/S Rashtas (T) Ltd, Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloloma and Brothers na Karnel Ltd.

Pamoja na hayo, Luhanjo alisema kampuni mbili kati ya 22 ambazo ni Rashtas (T) Ltd na G & T International Ltd hazikuwa na kumbukumbu za usajili wake kwa BRELA.

Kutokana ubadhirifu uliobainika katika ukaguzi huo, Kikwete ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu kukutana haraka ili kujadili taarifa ya ukaguzi na kuchukua hatua za kinidhamu kwa maofisa wanaotuhumiwa kuhusika na kulisababishia hasara taifa.

Pamoja na hatua hiyo, rais amesimamisha shughuli za ulipaji wa madeni kupitia akaunti ya EPA, hadi taratibu za uhakiki wa kampuni hizo utakapotengenezwa.

Rais pia amemwagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuongoza kazi ya uchunguzi wa tuhuma za kampuni na wahusika na kuwa uchunguzi huo uwe umekamilika katika kipindi cha miezi sita.

Katika kuifanya kazi hiyo, Mwanasheria Mkuu atashirikiana na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Pamoja na mambo mengine, Mwanasheria Mkuu na timu yake wanatakiwa kuhakikisha kuwa fedha zote zilizolipwa isivyo halali kwa kampuni hizo zinarudishwa serikalini.

Aidha, Luhanjo aliwataka watu wengine wenye taarifa za ziada kuhusu ubadhirifu huo, kuziwasilisha kwa timu hiyo yenye wajumbe wanne.

Tuhuma za ufisadi na ubadhirifu wa BoT zilitolewa hadharani na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2007/08 na baadaye akawasilisha hoja binafsi bungeni ya kutaka kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kulichunguza suala hilo.

Katika tuhuma hizo, Dk. Slaa alinukuu taarifa kadhaa kutoka katika mtandao wa intaneti zilizokariri baadhi ya majina ya watu, akiwamo Balali, na kuorodhesha jinsi ambavyo wamekuwa wakihujumu fedha za umma kupitia BoT. Uamuzi ambao ulitiliwa shaka na baadhi ya viongozi serikalini.

Hata hivyo, siku chache baadaye, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kwa nyakati tofauti walikiri kuwa serikali ilikuwa na taarifa kuhusu tuhuma katika akaunti ya EPA na wakaahidi kuwa zitafanyiwa kazi na kampuni ya kimataifa.

Kwa upande wake, wakati kikao hicho cha bajeti kikiendelea, Lowassa aliwahi kukaririwa akisema kuwa tuhuma hizo zinashtua na kuwa serikali ilikuwa inazifanyia kazi kwa umakini.

Kana kwamba hiyo haitoshi, Septemba 15, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam, Dk. Slaa alitaja orodha ya majina ya viongozi kadhaa wa serikali, Balali akiwamo, akiwatuhumu kwa ufisadi.

Akizungumzia tuhuma hizo, Dk. Slaa ambaye pia ni Mbunge wa Karatu, alimtaja Balali kuhusika katika ubadhirifu wa fedha za serikali kupitia akaunti ya EPA.

Kuundwa kwa EPA kulitokana na upungufu wa fedha za kigeni serikalini kati ya miaka ya 1970 na 1990 hivyo, BoT ilipewa jukumu la kusimamia matumizi ya fedha za kigeni kwa niaba ya serikali.

Kabla ya jukumu hilo kukabidhiwa rasmi BoT, kazi za EPA zilifanywa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Lakini, Juni 1998 iliamuliwa kuwa kazi za EPA zifanywe na BoT.

Kutoka Tanzania Daima.

No comments: