Thursday, January 31, 2008


Rais kuhudhuria kikao

cha Umoja wa Afrika


RAIS Jakaya Kikwete aliondoka nchini jana mchana kwenda mjini Addis Ababa, Ethiopia, kuhudhuria kikao cha 10 cha wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika (AU), kinachoanza leo na kumalizika Jumamosi wiki hii.

Ajenda kuu ya kikao cha mwaka huu ni “Maendeleo ya Viwanda katika Afrika”, mada inayolenga kuchochea mawazo mapya miongoni mwa mataifa wanachama wa AU kuhusu maendeleo ya Afrika yanavyoweza kusukumwa mbele kwa kutumia uzalishaji wa viwandani.

Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana imesema kikao hicho pia kitamchagua mwenyekiti mpya wa AU. Kwa kawaida Mwenyekiti wa umoja huo hupatikana kwa njia ya mzunguko wa kikanda.

Kwa mujibu wa utaratibu, mwenyekiti huyo mpya anatakiwa kutoka nchi za mashariki mwa Afrika. Eneo lenye nchi 14 za Burundi, Comoro, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Madagascar, Mauritius, Rwanda, Seychelles, Somalia, Sudan, Tanzania na Uganda.

Mbali na kumchagua mwenyekiti wa AU ambaye huwa ni mkuu wa nchi mojawapo wanachama wa umoja huo, nafasi inayoachwa wazi na Alpha Omar Konare wa Mali anayemaliza muda wake, kikao hicho pia kitamchagua Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Afrika.

Miongoni mwa ripoti zitakazowasilishwa na kujadiliwa kwenye kikao hicho ni pamoja na ile ya Kamati ya Mawaziri iliyopewa jukumu la kutoa mapendekezo kuhusu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Afrika.

Ujumbe wa Rais kwa kwenye kikao hicho unamshirikisha Mama Salma Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Basil Mramba na Waziri wa Biashara, Viwanda, Masoko na Utalii wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Samia Suluhu Hassan. Rais na ujumbe wake utarejea Dar es Salaam Jumatatu ijayo.

Chanzo: Gazeti la Mtanzania, Alhamisi 31.01.2008



No comments: