Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Leo imefikia siku ya kuuaga mwaka 2007 na kuukaribisha mwaka 2008. Naungana na Watanzania wenzangu tuliobahatika kufika siku hii ya leo kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa wema na rehema zake kwetu. Kwanza, tunamshukuru kwa kutujaalia uhai hivyo kutuwezesha kumaliza mwaka 2007 salama. Wapo wenzetu wengi hawakupata bahati hii. Pili, tunamshukuru kwa kuendelea kuijaalia nchi yetu amani, umoja na utulivu. Ametuvusha salama hata katika nyakati ambazo nchi yetu ilipitia katika mazingira magumu na tete. Tumuombe aijaalie nchi yetu baraka na neema tele mwaka ujao wa 2008.
Ndugu Wananchi;
Binafsi yangu, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa mambo mawili. Kwanza, kwa kunijaalia uhai na afya njema, mimi na familia yangu. Pili, namshukuru kwa kuniongoza vizuri na kuniwezesha kuitumikia nchi yetu na nyinyi Watanzania wenzangu kwa salama na kwa uwezo wangu wote. Napenda pia kuitumia fursa hii kuwashukuru tena wananchi wenzangu wote wa Tanzania kwa imani yenu kubwa kwangu na kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali yetu. Uelewa wenu mzuri wa mambo mbalimbali ya nchi yetu, msaada wenu na ushirikiano wenu mzuri ndivyo vilivyotuwezesha kuzikabili vyema changamoto mbalimbali zilizoikabili nchi yetu katika mwaka huu tunaoumaliza leo. Naomba tuendelee hivyo katika mwaka 2008.
Mapitio ya Mwaka 2007 na Matarajio kwa Mwaka 2008
Mwaka tunaoumaliza leo kama ilivyokuwa mwaka jana 2006 ulikuwa na mambo mengi mazuri na ya mafanikio. Pia ulikuwa na magumu yake na changamoto zake. Napata faraja moyoni mwangu kwamba mambo mengi tuliyokusudia kuyafanya mwaka huu tumeweza kuyafanya tena mengi tumeyafanya kwa ufanisi wa kiwango cha kuridhisha. Changamoto kuu nyingi nilizozizungumza katika hotuba yangu ya mwaka wa jana zimepatiwa ufumbuzi. Bahati mbaya changamoto moja ambayo haijapata ufumbuzi ni suala la bei kubwa ya mafuta ya petroli. Bei kubwa ya mafuta imekuwa chanzo kikubwa cha kuongeza ugumu wa maisha nchini. Siyo tu kwamba hatujapata ufumbuzi wake lakini ukubwa na ukali wa tatizo umekuwa mbaya zaidi sasa kuliko ilivyokuwa Desemba, 2006. Bei ya mafuta Desemba, 2006 ilikuwa dola 62.3 kwa pipa na mwezi huu wa Desemba, 2007 ni dola 97.12 kwa pipa. Bahati mbaya hatuna uwezo wa kuzifanya bei hizo zipungue. Lakini, lililo baya zaidi ni kuwa bei kubwa ya mafuta ndicho kichocheo kikubwa cha kuongezeka kwa gharama za maisha.
Hali ya Chakula
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu hali ya chakula ilikuwa nzuri. Mavuno yalikuwa mazuri karibu nchi nzima na ilipatikana ziada ya nafaka. Sehemu ya ziada hiyo imenunuliwa na Hifadhi ya Chakula ya Taifa (SGR). Hadi kufikia tarehe 11 mwezi huu (Desemba) SGR ilikuwa na akiba ya tani 142,295.981 za chakula zikiwemo tani 135,129.646 za mahindi na tani 7,166,335 za mtama. Kazi ya ununuzi wa nafaka bado inaendelea katika baadhi ya mikoa yetu ikiwemo Iringa, Ruvuma na Dodoma.
Hali ya Mvua za Vuli
Hatuna budi kuwapongeza wakulima kwa kazi nzuri waifanyao. Kadhalika tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia mvua nzuri zilizoleta tija hii katika kilimo mwaka huu. Tuendelee kumuomba atujaalie mvua nzuri mwaka ujao 2008. Bahati mbaya mwaka huu mvua za vuli ambazo hunyesha kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba hazikuwa nzuri katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Pwani, Morogoro na Dar es Salaam. Hali hiyo itasababisha mazao ya vuli kuwa kidogo au kukosekana kabisa katika baadhi ya maeneo. Aidha, inaashiria hatari ya kuwepo tatizo mwakani hasa iwapo mvua za masika nazo hazitakuwa nzuri katika mikoa hiyo. Hivyo tumuombe Mwenyezi Mungu ajaalie mvua za masika ziwe nzuri mwaka ujao. Napenda pia kutumia nafasi hii kuwasihi wakulima kutokukata tamaa kwa sababu ya kukosekana kwa mvua za vuli bali wajiandae kwa kilimo cha mvua za masika. Inshaalah Mwenyezi Mungu atujaalie rehema zake ili mwakani mvua ziwe nzuri.
Hali ya Uchumi
kubwa ya kushughulikia mwaka 2008 ili gharama za maisha ziwe nafuu.
Natambua ugumu uliopo hasa kwa vile bei za mafuta ziko juu na dalili ya kushuka ni ndogo. Hata hivyo hatuna budi kuhakikisha kuwa uzalishaji wa chakula na bidhaa nyingine hapa nchini unaongezeka ili uhaba wake usije ukachangia kupanda kwa mfumuko wa bei kama ilivyokuwa kwa bei ya saruji hivi karibuni.
Maendeleo ya Elimu
Mwaka 2007 umeendelea kuwa mzuri kwa upande wa elimu. Elimu ya msingi tumefikia asilimia 97 ya watoto wenye umri wa kwenda shule kuwa darasani kutoka asilimia 96 mwaka 2006. Taarifa ya watoto kutofanya vizuri mtihani wa darasa la VII imenifadhaisha. Nakubaliana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuwa tufanye uchunguzi wa kina na makosa yarekebishwe.
Kata nyingi nchini zimeendelea kutekeleza mpango wa ujenzi wa shule za sekondari za kata. Kwa ajili hiyo shule mpya 1,090 zimesajiliwa na jumla ya watoto 448,448 wameweza kujiunga na elimu ya sekondari kote nchini. Idadi hii ambayo inajumuisha wanafunzi katika shule za Serikali na binafsi ni kubwa kuliko ya mwaka 2006 ambayo ilikuwa 345,441.
Wakati tukiwapongeza wananchi na viongozi kwa mafanikio haya, napenda kuahidi kuwa Serikali inatambua wajibu wake kuhusu upatikanaji wa walimu, vitabu na vifaa vya maabara na vingine vya kufundishia. Tunaahidi kuwa tutaendelea kutimiza wajibu wetu katika mwaka ujao 2008 kama tulivyofanya mwaka huu. Kubwa zaidi ni makusudio yangu kufanya tathmini ya mpango mzima wa upanuzi wa elimu ya sekondari nchini kwa kushirikisha wadau. Lengo la tathmini hiyo ni kupima mwendo wetu: tulipo sasa na kule tuendako ili tuwe na mikakati na mipango bora zaidi.
Kwa upande wa elimu ya juu, nafurahi kwamba chuo Kikuu cha Dodoma kimeanza. Bado tunayo kazi kubwa ya kukijenga. Tutaendelea kwa kasi zaidi mwaka ujao. Katika mwaka ujao pia ni makusudio yetu kulifuatilia kwa karibu suala la mikopo ya wanafunzi kwa nia ya kurekebisha kasoro zilizopo.
Huduma ya Afya
Mwaka ujao tunatarajia kuanza utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi. Mpango ambao shabaha yake ni kusogeza huduma ya afya karibu na wanapoishi watu. Utekelezaji wake utaongeza zahanati vijijini na vituo vya afya katika Kata. Kufanikiwa kwa mpango huu kunategemea ushirikiano wa wananchi. Nawaomba wananchi wenzangu tutumie maarifa yale yale tuliyoyatumia kufanikisha ujenzi wa Sekondari kufanikisha mpango huu.
Hali ya Kisiasa
Tunaumaliza mwaka 2007 nchi ikiwa tulivu kisiasa na hali ya amani na usalama imeendelea kutawala. Nawashukuru viongozi na wanachama wenzangu wa vyama vya siasa kwa kudumisha utamaduni wa kushindana bila kupigana. Huo ndiyo msingi mama wa demokrasia ya vyama vingi. Kukingiana ngumi, kupigana au kufanya ghasia ni matendo yaliyo kinyume na misingi ya demokrasia. Tuzidi kumuomba Mungu aendelee kutuwezesha kudumisha utamaduni huo na nchi yetu iendelee kuwa kisiwa cha amani barani Afrika.
Nachelea kutukanana, kupakana matope na kudhalilishana kusije kuwa sehemu ya utamaduni wa siasa za Tanzania. Tutakuwa tumejifikisha mahali pabaya na kuifanya shughuli ya siasa kukosa thamani. Siasa ni shughuli tukufu lazima iendeshwe kwa misingi hiyo. Kutukanana ni kinyume cha utukufu huo.
Ndugu Wananchi;
Kama nilivyoahidi katika salamu zangu za mwaka mpya mwaka jana, tumedhamiria katika mwaka 2008 kuendelea kujenga mahusiano mazuri ya kisiasa na kijamii ili kuimarisha umoja, maelewano na mshikamano miongoni mwetu. Kwa sababu za msingi kabisa karibu mwaka wote huu tumeutumia kwa mazungumzo kati ya CCM na CUF. Nia yetu ni kumalizia haraka pale paliposalia katika mazungumzo hayo. Aidha, baada ya hapo tuwe na mawasiliano ya karibu na vyama vingine vya siasa. Yapo mengi ya kuzungumza kwa maslahi ya nchi zetu na vyama vyetu.
Hali ya Usalama
Ndugu Zangu, Wananchi Wenzangu;
Hali ya usalama wa nchi yetu nayo imeendelea kuwa nzuri. Navipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri waifanyayo ya kulinda mipaka na uhuru wa nchi yetu pamoja na mali ya raia wa Tanzania. Vita dhidi ya ujambazi imeimarika na mafanikio yanazidi kupatikana. Ingawa bado kuna matukio ya ujambazi ya hapa na pale lakini Jeshi la Polisi sasa limejenga uwezo mzuri wa kukabiliana na uhalifu huo.
Katika mwaka tunaouanza kesho tumedhamiria kuimarisha zaidi Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola katika mapambano dhidi ya ujambazi, biashara ya madawa ya kulevya, rushwa na vitendo vingine vyote vinavyotishia amani na usalama wa watu wetu.
Ndugu Wananchi;
Miongoni mwa mambo yaliyonisikitisha sana mwaka huu ni ongezeko la makosa ya ubakaji, mauaji na ajali za barabarani. Hadi Novemba, 2007 makosa ya ubakaji yalikuwa yameongezeka na kufikia 8,000 kutoka 3,946 mwaka 2006. Makosa ya mauaji yaliongezeka kutoka 2,309 mwaka 2006 hadi 3,144. Makosa ya ajali za barabarani yaliongezeka kutoka 15,560 mwaka 2006 hadi 15,650 mwaka 2007.
Ubakaji
Mauaji
Ajali za Barabarani
Ajali za barabarani ni nyingi mno na hasara yake ni kubwa kwa taifa. Katika mwaka ujao tuchukue hatua thabiti zitakazosaidia kupunguza ajali za barabarani hasa zinazosababishwa na uzembe wa madereva, magari mabovu yasiyostahili kuwa barabarani na usimamizi usioridhisha kwa upande wa wahusika. Miongoni mwa hatua ambazo hatuna budi kuchukua ni pamoja na zifuatazo:
(a)Kuhakikisha kuwa mtu anayepewa leseni ya kuendesha gari amepata mafunzo stahiki katika taasisi au vyombo vinavyotambulika. Tuache udereva wa kubahatisha.
(b)Madereva wazembe na wale wenye kumbukumbu za kuwa wakosaji sugu wafutiwe leseni za udereva wanapokutwa wamefanya kosa. Namtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Jeshi la Polisi walifanyie kazi agizo hili. Kama hapana budi sheria za sasa zifanyiwe marekebisho au sheria mpya itungwe.
(c)Kuhakikisha kuwa magari yanayotembea barabarani yana kiwango stahiki cha uzima. Magari mabovu na yasiyokuwa na sifa stahiki yasiruhusiwe kutembea barabarani.
(d)Wahusika na usimamizi wa sheria za usalama barabarani na uendeshaji wa shughuli za usafirishaji watimize ipasavyo wajibu wao. Hapa nina maana ya kwanza, Polisi wa Usalama Bararani (Traffic Police) wawe wakali, waache mazungumzo na madereva wazembe na wahalifu nyuma ya magari. Wanaofanya hivyo wachukuliwe hatua mara moja. Pili ni SUMATRA watimize ipasavyo wajibu wao kuhusu usalama wa vyombo vya usafirishaji wa abiria na mizigo. Na tatu, TANROADS wahakikishe ubora wa barabara hasa katika maeneo ambayo ajali hutokea mara kwa mara.
Mapambano Dhidi ya UKIMWI
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Napenda kuelezea furaha na shukrani zangu kwa jinsi watu walivyoitikia Kampeni ya Upimaji Virusi vya UKIMWI kwa hiari. Hadi kufikia tarehe 15 Desemba, 2007 kwa nchi nzima watu 3,004,701 walikuwa wamepima, kati yao wanaume ni 1,365,926 na wanawake ni 1,638,775. Hii inaamaanisha kuwa asilimia 72 ya lengo limefikiwa. Jambo la kutia moyo ni kuwa watu wanazidi kujitokeza. Inaelekea ujumbe sasa umewafikia wengi.
Matokeo ya upimaji yametupa taarifa nzuri kuhusu hali ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini. Taarifa inaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi ni asilimia 4.9 badala ya asilimia 7 ya mwaka jana. Hili ni jambo jema lakini bado asilimia 4.9 ya Watanzania kuwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI ni kubwa mno. Hatuna budi kuendelea kuwa makini na kuchukua tahadhari stahiki.
Nawaomba ndugu zangu tuazimie kuwa katika mwaka ujao tutazidisha mapambano dhidi ya maradhi haya. Kwa wale ambao hawajapima wajitokeze kupima. Pili, kwa wote kuamua kwa dhati kuepuka kupata maambukizi. Bado naamini na napenda sote tuamini hivyo kuwa Tanzania Bila UKIMWI inawezekana.
Uhusiano wa Kimataifa
Mwaka 2007 ulikuwa mwaka wa mafanikio makubwa kwa Tanzania katika medani ya kimataifa. Tumeshuhudia Watanzania kadhaa wakipata nafasi za juu katika vyombo vya kimataifa. Tulianza mwaka vizuri kwa kushuhudia dada yetu Dr. Asha-Rose Migiro akiteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi yake Februari, 2007. Ilikuwa fahari kubwa kwa nchi yetu na heshima kubwa kwake na taifa letu. Tuendelee kumuombea na kumuunga mkono afanikiwe. Mpaka sasa mambo yanakwenda vizuri. Anaibeba vizuri heshima ya Afrika na Tanzania.
Ndugu Wananchi;
Uhusiano wetu na wabia wetu wa maendeleo uliendelea kuimarika. Imani yao kwa Serikali na nchi kwa ujumla iliendelea kuwa nzuri. Tumepata mafanikio ya kutia moyo kwa upande wa misaada ya maendeleo na msamaha wa madeni. Ukilinganisha na mwaka 2006 misaada ya maendeleo imeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.9 hadi shilingi trilioni 2.5 mwaka huu wa fedha 2007/2008.
Kwa upande wa Marekani tunafurahi kwamba mchakato uliotuchukua miaka miwili ulikamilika Desemba 12, 2007, baada ya Bodi ya Mfuko wa Milenia wa Serikali ya Marekani kufanya uamuzi wa mwisho na kuafiki Tanzania ipate msaada wa dola 698 milioni. Kinachosubiriwa sasa ni Bunge la Marekani kutenga fedha hizo ili Januari, 2008 zipatikane na utekelezaji uanze wa miradi iliyokusudiwa ya miundombinu ya barabara, maji na umeme. Msaada huo utatusaidia sana kutatua matatizo ya barabara mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Tanga na Zanzibar. Pia itatumalizia tatizo la umeme Kigoma na Kasulu. Vile vile itatupunguzia matatizo ya maji katika miji na maeneo kadhaa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa misamaha ya madeni nafurahi kusema kuwa mwaka huu umekuwa mzuri. Juhudi zetu za kupata misamaha ya madeni tunayodaiwa na baadhi ya nchi au taasisi zimeweza kuzaa matunda ya kutia moyo. Tumepata msamaha mkubwa wa madeni kutoka Serikali ya Japani pale Januari 30, 2007 walipoamua kutusamehe deni la karibu shilingi bilioni 595.5.
Tatizo kubwa kwa upande wa kutafuta msamaha wa madeni ambalo bado tunalo ni kwa nchi na taasisi za nchi ambazo si wanachama wa Paris Club. Nchi hizo ni Iran, Iraq, Algeria na Brazil ambazo kwa pamoja wanatudai kiasi kinachofikia dola bilioni moja.
Ni makusudio yangu na wenzangu Serikalini kuwa mwaka ujao tuelekeze nguvu zetu za mazungumzo katika nchi hizo kutafuta nafuu ya madeni hayo. Kwa hakika ni makubwa mno na uwezo wetu wa kulipa ni mdogo.
Wenyeji wa Mikutano ya Kimataifa
Kutokana na sifa na heshima tuliyojijingea, mwaka 2008 nchi yetu imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa mikutano mitatu mikubwa na muhimu ya kimataifa. Mikutano hiyo ni:
(a)Mkutano wa Uzinduzi wa Shughuli za Mwaka wa Sayari Dunia kwa Bara la Afrika.
(b)Mkutano wa Utalii wa Bara la Afrika; na
(c)Mkutano wa Nane wa Sullivan.
Mikutano hiyo kufanyika hapa nchini ni jambo la faraja kubwa. Mikutano hiyo ina hadhi kubwa kimataifa, inashirikisha watu wengi na kuvutia macho na masikio ya dunia pamoja na vyombo vya habari vya kimataifa pale inapofanyikia. Hivyo basi kwetu sisi ni fursa nzuri ya kuitanganza nchi yetu kwa utalii na uwekezaji. Pamoja na hayo ni ukweli kwamba watu wapatao 4,000 watakaoshiriki wanaongeza mapato ya utalii kwa taifa letu.
Napenda kuitumia nafasi hii kuwaomba Watanzania wenzangu kujiandaa vyema kuwapokea wageni wetu hao. Watanzania tunayo sifa ya ukarimu, naomba tuendelee kuionyesha kwa wageni wetu hawa. Tunatarajia ushiriki wa Wakuu wa Nchi na Serikali katika shughuli ya Uzinduzi wa Mwaka wa Sayari Dunia na Mkutano wa Nane wa Sullivan.
Mkutano wa Sullivan ni jukwaa linalokutanisha Waafrika walioko Barani Afrika na ndugu zao wenye asili ya Kiafrika walioko Marekani. Katika mikutano ya Sullivan washiriki huzungumzia masuala ya kuinua maendeleo ya Bara la Afrika kwa uwekezaji, biashara, elimu na teknolojia. Mwaka huu agenda kuu ni kuendeleza utalii, miundombinu na hifadhi ya mazingira, mambo ambayo yana umuhimu wa aina yake kwa maendeleo ya Tanzania.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2005 Umoja wa Mataifa ulitanganza kuwa mwaka 2008 utakuwa Mwaka wa Sayari Dunia kufuatia uamuzi uliofanywa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kikao chake cha 60 mwezi Desemba, 2005. Chimbuko la uamuzi huo ni pendekezo la Tanzania lililowasilishwa na kukubaliwa kwanza na Mkutano Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mapema mwaka 2005 na baadaye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Uzinduzi wa shughuli za Mwaka wa Sayari Dunia utafanyika kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza itakuwa ni uzinduzi wa kimataifa utakaofanyika Paris, Ufaransa kwenye Makao Mkuu ya UNESCO mwezi Februari, 2008. Awamu ya pili itakuwa ni kwenye ngazi ya kanda. Kwa kanda ya Afrika nchi yetu Tanzania imeteuliwa kuwa mwenyeji wa shughuli hiyo kunako Mei, 2008.
Ndugu Wananchi;
Sisi Watanzania tunao wajibu maalum katika jambo hili. Kwanza kwamba sisi ndiyo tuliobuni wazo hili na wenzetu wakatukubalia. Isitoshe Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin Mkapa ndiye Mlezi wa Mwaka wa Sayari Dunia. Pili, sisi tumepewa dhamana ya kuwa wenyeji wa sherehe maalum za uzinduzi wa Mwaka wa Sayari Dunia. Kwa sababu hizo lazima Watanzania tuwe mstari wa mbele katika utekelezaji wa malengo ya Mwaka wa Sayari Dunia. Aidha, tuhakikishe kuwa shughuli ya uzinduzi wa Mwaka wa Sayari Dunia kwa Kanda ya Afrika itakayofanyika hapa kwetu inakuwa na mafanikio makubwa.
Madhumuni ya Mwaka wa Sayari Dunia
Madhumuni ya kuwa na Mwaka wa Sayari Dunia ni kutoa fursa kwa mwanadamu kuichambua na kuitafakari kwa kina hali ya dunia tunayoishi kwa nia ya kujiweka tayari kuchukua hatua za kuifanya kuwa mahali salama na bora pa kuishi. Lengo la kufanya uchambuzi na tafakuri hizo ni kwanza, kutambua kwa ufasaha mazuri, mabaya na changamoto zilizopo. Na pili, kutafuta njia muafaka ya kukabili changamoto hizo kwa maana ya kudumisha na kuendeleza mazuri upande mmoja na kurekebisha kasoro upande mwingine.
Ni ukweli usiofichika kwamba hali ya sasa ya mazingira ya dunia hairidhishi na muelekeo wake si mzuri hata kidogo. Mazingira yamechafuka sana. Kama hatua madhubuti za kurekebisha mambo hazitachukuliwa sasa, hali itakuwa mbaya zaidi katika miongo michache ijayo. Wanadamu na viumbe vingine watakosa mahali palipo salama pa kuishi na hata uhai wao unaweza kutoweka. Ukweli ni kwamba baadhi ya viumbe tayari vimeshatoweka.
Ndugu Wananchi;
Matendo yetu na shughuli zetu wanadamu ndicho chanzo cha madhara ya kimazingira yanayoisibu dunia yetu leo. Mwanadamu hana budi kubadilika. Aache tabia na matendo yake mabaya na kuchukua hatua za kurekebisha makosa na kuboresha mazingira ya Sayari Dunia. Matumizi ya maarifa ya sayansi dunia yamesisitizwa katika kufanya uamuzi na utekelezaji wake.
Kutakuwepo na programu maalum ya kuelimisha jamii inayolenga pia wanasiasa na watu walioko kwenye nafasi za kutoa maamuzi. Lengo ni kuwapa maarifa ya elimu ya sayari dunia na jinsi ya kuitumia kujiletea maendeleo na kuinua kiwango cha ubora wa maisha ya wananchi. Mafunzo maalum yatatolewa kwa waandishi wa habari na walimu kuhusu mambo yahusuyo Sayari Dunia na mazingira ili wao wasaidie kuelimisha jamii pamoja na vijana mashuleni.
Mabadiliko ya Tabia-Nchi
Ndugu Wananchi;
Miongoni mwa mambo muhimu yatakayochambuliwa na kutafakariwa katika Mwaka wa Sayari Dunia ni suala la mabadiliko ya tabianchi (Climate Change) au mabadiliko ya hali ya hewa kama wengi tulivyozoea (Hii hata Waziri Mkuu wa Norway ameigusia kwenye salamu zake za mwaka 2008, hapo cini). Nafurahi kwamba suala hili litapewa uzito unaostahili kwani unapozungumzia uharibifu wa mazingira kielelezo chake na kiini chake pia ni mabadiliko ya tabianchi.
Ndugu zangu, Wananchi Wenzangu;
Hakika mabadiliko ya tabianchi ni tishio kubwa kwa maisha na uhai wa mwanadamu. Walio hatarini zaidi ni sisi katika nchi maskini kwa sababu ya uwezo mdogo wa rasilimali, utaalamu na teknolojia za kukakabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lakini hata hizo nchi zilizoendelea nazo ziko mashakani kwani hata kwao majanga ya asili yameongezeka. Isitoshe duniani tunategemeana: athari ya upande mmoja hugusa upande mwingine.
Ndugu Wananchi;
Chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi ni kuongezeka kwa joto duniani. Kuongezeka kwa joto duniani kunasababishwa na kuongezeka kwa gesijoto (greenhouse gases) kwa kiwango kikubwa mno kuliko kinachohitajika kuwezesha uhai na mifumo ya dunia kuwa katika hali yake ya asili.
Gesijoto husika hapa hasa ni gesimkaa (carbon-dioxide), methani (methane) na nyinginezo ambazo zinatokana na shughuli za mwanadamu katika kujiletea maendeleo. Shughuli kuu zinazohusika kuzalisha gesijoto kwa wingi ni viwanda, vyombo vya usafirishaji, ufyekaji misitu, uchomaji moto ovyo (mioto kichaa) na kilimo kisichoendelevu. Ili kuinusuru dunia na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, mwanadamu hana budi achukue hatua za kuzuia kuongezeka zaidi kwa gesijoto duniani na kupunguza kiasi cha gesijoto kilichopo sasa ili kirejee kwenye viwango salama.
Huo ndiyo wajibu wa nchi zetu na watu wote duniani. Kufanya hayo ndiyo madhumuni na maagizo makuu ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (The UN Framework Convention on Climate Change) wa mwaka 1992 na Itifaki ya Kyoto (Kyoto Protocol) ya mwaka 1997.
Ndugu Wananchi;
Athari za mabadiliko ya tabianchi na sisi tumezipata na tunaendelea kuzipata. Misimu ya mvua haitabiriki siku hizi. Majanga ya mafuriko na ukame yameongezeka. Tunazikumbuka athari za mafuriko ya mvua za El-Nino za mwaka 1997/98. Tunakumbuka adha ya ukame wa 1993/94 na wa 2005/06 ambao ulikuwa mkali kuliko wowote uliowahi kuikumba nchi yetu kwa miaka mingi.
Theluji katika kilele cha Mlima Kilimanjaro inazidi kupungua (Hii hata Waziri Mkuu wa Norway, kwenye salamu zake za mwaka 2008 ameitaja, angalia hapo chini). Wataalamu wanasema kuwa mlima wetu huo umepoteza asilimia 80 ya theluji yake katika kipindi kifupi cha miaka 50 iliyopita. Kina cha maji katika Ziwa Victoria kimepungua kwa mita 2.57 kati ya mwaka 1965 na 2006. Kisiwa cha Maziwe katika pwani ya Pangani kimezama kutokana na kuongezeka kwa usawa wa bahari.
Aidha, visima vya maji baridi katika baadhi ya maeneo ya Pwani kama vile Bagamoyo havitumiki tena kwa sababu ya kuongezeka kwa maji ya bahari. Maradhi ya malaria sasa yameenea hata katika maeneo ya milimani na yenye baridi kama vile Lushoto, Amani, Rungwe na Kitulo ambako zamani hayakuwepo. Sababu ni ongezeko la joto linalowezesha mbu kuishi.
Ndugu zangu;
Orodha ya mambo yanayodhihirisha athari za mabadiliko ya tabianchi hata hapa kwetu ni ndefu itoshe leo kutaja hayo. Lakini la muhimu ni kuwa tunao wajibu na sisi kama walio nao wenzetu wa mataifa yaliyoendelea wa kuchukua hatua za kuzuia ongezeko la joto na kupunguza kiasi cha joto kilichopo. Tunao wajibu wa kuzuia uharibifu wa mazingira na kuboresha palipo haribika.
Mengi ya yale tunayowajibika kufanya yamo katika maudhui ya nyaraka kuu tatu:
(a)Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004;
(b)Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (National Adaptation Programme of Action) 2006; na
(c)Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji (2006).
Hivi sasa Serikali iko mbioni kuandaa Waraka wa nne yaani Mkakati wa Hatua za Haraka za Kuhifadhi Mazingira ya Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa.
Mimi naamini tukitekeleza ipasavyo yaliyoagizwa katika mipango na mikakati hiyo Tanzania itakuwa nchi salama kuishi sisi na vizazi vijavyo. Haya shime tutekeleze. Wakati ni huu. Hatuna muda zaidi wa kupoteza. Napenda kusisitiza kuwa katika kufanikisha malengo ya Mwaka wa Sayari Dunia tuazimie kuwa huo uwe ndiyo mchango wetu mkubwa.
Hitimisho
Ndugu Wananchi; Watanzania Wenzangu;
Napenda kuhitimisha salamu zangu za mwaka mpya kwenu kwa kuwashukuru tena nyote kwa imani yenu kubwa kwangu na kwa serikali ninayoiongoza. Mimi na wenzangu serikalini tunafarijika sana kwa ushirikiano mkubwa mnaotupa katika utekelezaji wa jukumu letu la msingi la kuwatumikia.
Tunapouanza mwaka mpya kesho, nataka kuwahakikishia tena kuwa tumedhamiria kwa dhati kuwatumikia kwa moyo wetu wote na nguvu zetu zote. Tutajitahidi kwa kadri ya uwezo aliotujaalia Mwenyezi Mungu kushirikiana nanyi katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa matatizo yanayolikabili taifa letu na kuimarisha kasi ya kuleta maendeleo nchini mwetu. Naamini kwa pamoja tutashinda.
Baada ya kusema hayo, nawatakieni nyote heri na fanaka ya mwaka mpya 2008. Sote tusherehekee kwa amani na utulivu.
Mungu Ibariki Afrika;
Mungu Ibariki Tanzania.
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment