Wednesday, January 09, 2008

Serikali kuwachunguza wafanyabiashara wa Kiasia


Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.


na Kulwa Karedia

SERIKALI imesema itaanza msako mkali dhidi ya wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia waliozagaa katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, ili kubaini uhalali wa kazi zao wanazofanya.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana kuhusu mafanikio ya wizara yake, Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, John Chiligati, alisema ataviagiza vyombo vyote vinavyohusika kushughulikia suala la wafanyabiashara hao mara moja.

"Tumekuwa tukipata taarifa za kuwapo kwa wafanyabiashara wenye asili ya Kiasia wakifanya biashara zilizokuwa zikilalamikiwa na wazawa, hasa eneo la Kariakoo, jijini," alisema Chiligati.

Alisema kupitia idara mbalimbali za serikali zikiwamo Idara ya Uhamiaji, Kituo cha Uwekezaji na Mamlaka ya Utoaji wa Leseni za Biashara (Brela), wataendesha msako huo, ili kubaini vibali vya wafanyabiashara hao.

"Kwa kutumia idara hizi za serikali tutafanya uchunguzi wa watu hawa na kama waliingia nchini wakitaka vibali vya utalii kisha wakageuka kuwa wafanyabiashara watakuwa wamekiuka sheria za nchi … lazima vibali vyao vichunguzwe," alisema Chiligati.

Alisema ikibainika kuwa wafanyabiashara hao wamejiandikisha TIC na kisha kujiamulia kufanya kazi nyingine, wanavunja sheria zilizopo kwa vile hawaruhusiwi kufanya hivyo.

Akizungumzia mafanikio ya wizara yake kwa miaka miwili iliyopita, Chiligati alisema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kumaliza migogoro ambayo imekuwa ikiibuka sehemu mbalimbali za kazi kwa kuunda Kamisheni ya Mamlaka ya Afya na Usalama Mahala Pa Kazi (OSHA).

"Baada ya kuundwa kwa kamisheni imefanikiwa kupokea migogoro 4,810 na kati ya hiyo 2,864 imetatuliwa. Hili ni jambo kubwa la kujivunia kwa kweli," alisema.

Mafanikio mengine ni wizara yake kuanzisha kituo cha kusaidia Watanzania kupata ajira nchi za nje ni wale wa hapa nchini vituo vimefunguliwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.

Kuhusu sekta binafsi wafanyakazi wake kulipwa mishahara mipya, Chiligati alisema sekta zote zimetakiwa kulipa kima cha chini sh. 300,000 kuanzia mwezi huu.

"Napenda kurudia wito wangu kwamba kama sekta yoyote itakaidi agizo hili ni heri wafunge makampuni yao," alisema Chiligati.

Kuhusu ajira, Chiligati alisema hadi sasa jumla ya ajira 41,390 zimetolewa katika mpango wa kutoa ajira milioni moja hadi Septemba 2007 kati ya ajira milioni moja zilizoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete wakati akiingia madarakani.

Kwa upande wa mikopo kwa wjasiriamali, Chiligati alisema katika awamu ya kwanza jumla ya sh. bilioni 31.55 zilitolewa huku wajasiriamali 21,133 wakinufaika.

Alisema mbali na hayo, pia serikali imezindua awamu ya pili ya mikopo yenye thamani ta sh. bilioni 10.5 ambayo sasa itatolewa kupitia benki za NMB, CRDB, Benki ya Akiba Commecial (ACB), Benki ya Posta Tanzania, Benki ya Ushirika Kilimanjaro, Benki ya Azania, Kagera Farmers Co-operative Bank, SCCULT (1992) Ltd, Benki ya Wananchi wa Mbinga, Ufundi, Benki ya Uchumu Commecial, Pride Tanzania, Presidential Trust Fund na Dunduliza

Kutoka Tanzania Daima.

No comments: