Wednesday, January 30, 2008

Tunataka viongozi wa kesho

wajifunze nini kutokana

na somo hili?


JINA MRADI
Ben Mkapa - Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira
Juma Kapuya - Mgodi wa dhahabu Maisha bora baada ya kustaafu.
N. Karamagi - Kampuni ya kushughulikia makontena bandarini (TICTS)


JINA MRADI
Julius Nyerere - Hakuna mradi aliomiliki
Joseph Warioba - Hakuna mradi aliomiliki Maisha magumu baada ya kustaafu.

Timothy Apiyo - (aliwahi kuwa Katibu Mkuu ofisi ya Rais) hakuna mradi anaomiliki


Ni jambo lililo wazi kwamba kama somo lililoko hapo juu litawaingia akilini vijana wetu wanaotarajiwa kuwa viongozi wa nchi hii kesho, watakachoelewa ni kwamba mara waingiapo madarakani cha kwanza kufanya ni kugawana watakachokikuta ndipo waanze kuwafikiria wengine, (Self centered philosophy) na kwamba uaminifu mwisho wa siku hataulipa! Na watajifunza hili kwa mifano hai ya watu waliokuwa waaminifu wakati wa utendaji wao, maisha yao yalikuwaje baada ya kustaafu? Kuna wakati hatuongei lakini matendo yetu yanasema zaidi ya maneno, nina uhakika kwa haya tunayofanya leo tukiwa madarakani tunawafundisha vijana wetu kitu kimoja tu; KUCHOTA na kuondoka. Jambo ambalo kwa hakika sio jema.

Unategemea nini vijana wetu wanaoingia makazini leo, iwe ni serikalini au kwenye mashirika ya Umma kama watajifunza kuwa mfano wa mzee Timothy Apiyo, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais kwa miaka mingi lakini mwisho wa siku amekuwa akiishi maisha ya kimasikini kutokana na uaminifu wake kazini. Vijana wetu watajifunza nini watakapoiangalia familia ya Hayati Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekaa madarakani kwa miaka ishirini na minne lakini hakujilimbikizia mali yoyote na hata nyumba Butiama akajengewa kama msaada na Jeshi la Wananchi kwa sababu hakutaka kuwa fisadi na leo hii familia yake inaishi maisha kama ya Mtanzania mwingine yeyote? Wakati kama mzee huyo angekuwa fisadi, kwa muda mrefu aliokaa madarakani sisi leo hii tusingekuta kitu!

Wapo wapi viongozi wa mfano wake? Wapo wapi viongozi wa mfano wa mzee Rashidi Mfaume Kawawa aliyekaa madarakani kwa muda mrefu akiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu? Wapo wapi viongozi wanaoingia madarakani kwa nia ya kuwatumikia wananchi? Watu wa aina hii huwa hawakosi, najua wapo lakini wamemezwa na kuvunjwa moyo! Hebu fikiria ni wafanyakazi wangapi serikalini leo ambao watakuwa tayari kusimamia maslahi ya nchi hata wanapoingizwa kwenye majaribu ya rushwa, pale watakapokumbuka kwamba Dk. Daudi Ballali na timu yake walichota zaidi ya shilingi bilioni 133? Inahitaji moyo na wenye moyo huo ndio watakaoijenga nchi hii.

Ndugu zangu, Kazi yetu kubwa Watanzania ni kupambana na ufisadi kwa gharama yoyote na bila woga kwa faida yetu, watoto, wajukuu na watoto wa wajukuu zetu.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Kutoka: Global Publishers



No comments: