Ikhtiari ya Mwaka Mpya
Innocent Mwesiga
HIVI karibuni, Seneta wa Jimbo la Connecticut, Joe Lieberman, aliamua kumuunga mkono mgombea urais kupitia tiketi ya chama cha Republican, Seneta John McCain. Lieberman alisema:"Inawashangaza wengi kuona Seneta anayejitambulisha na chama cha Democratic, akimuunga mkono mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican". Aliongeza: "Vyama vya siasa ni muhimu kwa Wamarekani, lakini si muhimu kuzidi mambo wanayoyaamini. Ama si muhimu kuzidi yatakayotokea kesho, au kuzidi maslahi ya Taifa la Marekani".
Binafsi, sitarajii Seneta McCain ashinde kiti cha urais eti kwa sababu tu ameungwa mkono na Seneta Lieberman. Hata hivyo, naamini na kuyatilia maanani maudhui ya ujumbe wa Seneta Lieberman kwa Wamarekani. Katika waraka wa leo, ningependa nishirikishane mangÍamuzi yangu ya ujumbe huu kama ikhtiari yangu ya mwaka mpya wa 2008.
Kwa muda mrefu, nimekuwa nikitatizwa na mazoea yanayojengeka katika mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania. Kwa kiwango cha juu, tumeshuhudia mivutano isiyo na kichwa wala miguu, baina ya kambi ya vyama vya upinzani na ile ya chama tawala. Jamii yetu inaanza kukubali utamaduni mbaya ambamo, wabunge au wasemaji wa vyama vya upinzani wanapotoa mapendekezo au kuzungumza jambo la msingi la kuikosoa Serikali, basi papo kwa papo, au kesho yake, wasemaji au wabunge wa chama tawala wanakurupuka na kupinga jambo hilo, hata kama ni muhimu kwa Taifa.
Vivyo hivyo, wabunge au wasemaji wa chama tawala wanapotoa mapendekezo au maelekezo ya maana kwa wananchi, basi wabunge au wasemaji wa vyama vya upinzani, ama wanakaa kimya bila kuunga mkono maelekezo ya Serikali, ambayo ni ya msingi kwa Taifa, au nao wanapinga bila kufanya tafakari ya kina, tena kwa mtindo wa papo kwa papo. Mazoea ya namna hii yameanza kuchukua taswira kama ya michezo ya kitoto ya kuvuta kamba. Nimefikia mahala pa kuamini kuwa hakuna tamko la maana litolewalo na chama tawala bila kupingwa na vyama vya upinzani. Au hakuna litokalo kinywani mwa vyama vya upinzani bila kupingwa na chama tawala.
Wasiwasi wangu ni kuwa tutafikia mahala (kama hatujafikia) ambako, chama tawala kitaweka kando mikakati ya kuwakomboa wananchi kutoka katika lindi la umasikini, na badala yake kitaendekeza mikakati ya kusubiri kupinga matamko ya vyama vya upinzani. Na hiyo ndiyo itageuzwa kuwa sera na mikakati rasmi ya chama tawala. Na vyama vya upinzani vitaachana na mikakati ya kuunganisha juhudi za wananchi za kujikwamua kutoka katika makucha ya utawala mbovu, na kuvizia matamko ya Serikali ili viyapinge. Na hiyo ndiyo itakuwa sera rasmi ya vyama vya upinzani.
Utafikiri katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, kazi ya chama tawala ni kupinga yasemwayo na vyama vya upinzani, na kazi ya vyama vya upinzani ni kupinga yasemwayo na chama tawala. Mivutano inayoendekeza ubishi usio na mantiki badala ya majadiliano ya hoja zinazowakilisha mawazo ya wananchi, inatoa mianya kwa makampuni ya kibeberu kuendelea kutamba, na mwishowe kuweka mazingira ya kuangamiza taifa.
Makampuni makubwa ya kibeberu yanaazima busara kutoka katika hadithi ya wezi waliokwenda kuiba nyumbani kwa mtu aliyemiliki mbwa wengi waliokuwa wanalinda mali yake. Badala ya kulinda mali ya mmiliki wao, na kuunganisha nguvu zitokanazo na wingi wao ili kuwakabili wezi, mbwa hao walishia kugombania mfupa uliorushwa kwao na wezi waliokuja kuiba mali ya mmiliki wao.
Ugomvi wa mbwa ulitoa mwanya kwa wezi kupora mali zote na kutimua mbio bila kusumbuliwa na wingi wa mbwa.
Mfano, ni mwaka uliomalizika wa 2007, wakati Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) Zitto Kabwe, alipowasilisha bungeni hoja ya kuundwa kamati teule ya Bunge kuchunguza mapitio ya mikataba ya madini na mazingira ya kusainiwa kwa mkataba mpya wa madini wa Buzwagi kulikofanywa na Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamagi (CCM) huko Uingereza mwezi Februari 2007.
Hata kabla Zitto hajawasilisha hoja yake, ambayo ni ya msingi, baadhi ya wabunge kutoka vyama tofauti, kikiwamo chama tawala, walikwisha kutoa dukuduku hadharani kuonyesha kutokuridhishwa na mikataba mbalimbali iliyosainiwa na Serikali. Mfano, Mbunge wa Same Mashariki (CCM) Anne Kilango Malecela, aliwachachamaria watendaji wa Serikali kuwa wamekuwa wakitia saini mikataba bila kumtanguliza Mungu na uzalendo kwa nchi yao (Uhuru, Juni 2007).
Ajabu, badala ya wabunge wa vyama vyote kuweka maslahi ya Taifa mbele, kwa kuungana ili kuridhia hoja ya kuundwa kamati teule ya Bunge kuchunguza mikataba ambayo wabunge wenyewe walikuwa na wasiwasi nayo, waliamua kuweka maslahi ya vyama mbele, kwa kushikamana na kuwajibika kivyama bila kuangalia kama mshikamano wao wa vyama ulikuwa ni muhimu kwa Taifa au la. Hata kama wabunge wa CCM waliamini kuwa hoja ya Zitto ilikuwa na mantiki na ilihitaji kuungwa mkono, lakini waliipinga kwa sababu moja tu, kwamba imetoka katika kambi ya upinzani.
Pengine maelezo yanayotoa mwanga wa ninachokiongelea yalitolewa na Mbunge Khalifa S. Khalifa wakati anachangia hoja ya Zitto bungeni aliposema: ñNi Bunge hili hili, na Wabunge hawa hawa katika mijadala mbalimbali wamekuwa wakilizungumzia jambo hilo labda wayafute maneno yao leo. Wamezungumza sana kuhusu mikataba ya madini. Kama tutakuwa tunakwenda katika mwenendo huo, hii ni hatari mno. Kwa sababu ni sisi wabunge, Bunge hili hili tumesema mikataba ya madini ina matatizo tunahitaji tuione, ina mambo mengi. Sasa kama leo imetolewa hoja ya kuundwa tume ya Bunge kutazama issue moja tu ya mkataba mmoja tu ilishakuwa tatizo kubwa, nasikitika sanaî.
Katika tukio jingine, Mbunge wa Bariadi Mashariki John Cheyo (UDP), alitoa pendekezo kwa Serikali kuweka mikataba katika tovuti ili kuondoa hofu ya kuwapo kwa rushwa katika mikataba hiyo, lakini kadiri ya mazoea tunayoyajenga, Waziri wa Katiba na Sheria, Mary Nagu alikataa ombi hilo kwa alichokiita kuwa ni kulinda maslahi ya Taifa katika mikataba hiyo (Majira, Agusti 2007).
Tunajenga mazoea kwa waziri, ambaye anaiwakilisha Serikali bungeni, na wakati huo huo amevaa joho la kuwawakilisha wananchi bungeni, anamwambia mwakilishi mwenzake wa wananchi kwamba, mikataba iliyosainiwa na Serikali kwa niaba ya wananchi itabaki kuwa siri ya Serikali na wananchi hawataruhusiwa kuiona. Kwa sababu kitendo cha wananchi kuona maslahi yao ni kinyume cha kulinda maslahi yao. Binafsi naamini kuwa Taifa linaundwa na wananchi. Ni vigumu kuongelea maslahi ya taifa bila kuongelea maslahi ya wananchi. Pengine, hakuna kitu kinaitwa maslahi ya Taifa, bali kuna kitu kinaitwa maslahi ya wananchi.
Kupuuzwa kwa maslahi ya wananchi ni kupuuzwa kwa maslahi ya Taifa. Nilidhani bungeni ni mahala pa kutetea maslahi ya wananchi, lakini pamegeuzwa kuwa uwanja wa malumbano baina ya chama tawala na vyama pinzani, hivyo kutoa fursa nzuri kwa makampuni ya kibeberu kuimarisha mirija yao ya kufyonza kila kilichopo ardhini.
Mara nyingi, hata Rais Jakaya Kikwete ameonekana kunasa katika mtego wa malumbano ya vyama vya siasa. Mfano, akiwa ziarani Norway, alimwambia Waziri wa Maendeleo na Ushirikiano wa Norway kuwa matatizo yanayojitokeza katika mikataba mbalimbali ambayo Serikali imeingia na wawekezaji, yanachangiwa na uwezo mdogo wa baadhi ya wataalamu wa Kitanzania wanaoshiriki katika majadiliano ya mikataba hiyo. Hivyo, aliiomba Serikali ya Norway kuwapatia mafunzo na mbinu za kisayansi wataalamu wa Tanzania zitakazowapa uwezo wa kujadiliana na wawekezaji huku wakiweka mbele maslahi ya Taifa.
Maneno ya Rais Kikwete kwa Waziri wa Norway yasingetiliwa shaka kama yangetolewa enzi za mikataba ya ulaghai kati ya mababu zetu na akina Karl Peters. Mfano, Chifu Abushiri aliporidhia kuchukuliwa kwa sehemu kubwa ya ardhi ya himaya yake, baada ya kupewa kipande cha nguo, tulifundishwa shuleni kwa msisitizo kuwa machifu waliojihusisha na vitendo vya namna hiyo walikuwa hawajasoma.
Baada ya miaka 46 ya uhuru, ni vigumu kuamini maneno ya Rais Kikwete yanayotutaka tukubali kuwa tatizo letu bado ni lilelile walilokuwa nalo mababu zetu. Tena wakati Rais Kikwete anaongea hayo maneno, Waziri wake wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, alikuwa anatia sahihi katika mkataba wa Buzwagi.
Waziri Karamagi aliwahi kuliambia Bunge wakati anahitimisha hoja ya makadirio ya matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2007/2008 kuwa, mkataba wa Buzwagi uliandaliwa Tanzania na wataalamu wa Kitanzania, na ukapitia taratibu zote zinazopaswa kufuatwa ikiwa ni pamoja na kuidhinishwa na kamati ya ushauri ya madini, na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Pamoja na ukweli kuwa nchi yetu imetumia fedha nyingi kuwasomesha wataalamu wanaoipitia mikataba kabla ya kusainiwa, lakini bado hakuna ufumbuzi wa kiini cha tatizo. Rais anaunda utitiri wa tume kwa lengo la kuridhisha wananchi na kuzima moto ulioanzishwa na vyama vya upinzani. Wakati mwingi, hata majibu yake katika masuala muhimu ya nchi yamelenga katika malumbano na vyama vya upinzani badala ya kutoa taswira halisi ya kinachoisibu nchi. Lakini yote tisa, kumi ni malumbano ya hivi karibuni kati ya vyama vya upinzani na chama tawala kuhusu umuhimu wa Katiba mpya. Binafsi naamini kuwa kiini cha matatizo tuliyonayo ni kupwaya kwa Katiba.
Hakuna shaka kwamba, Katiba inavipendelea vyama vya siasa kuliko inavyohifadhi haki za raia, ambazo zilikuwapo kabla ya vyama vya siasa, na hata kabla ya Katiba yenyewe kuundwa. Lakini vyama vya siasa vinavyopendelewa na Katiba, vimepoteza dira kwa kuendekeza malumbano. Wananchi waliofungwa pingu kikatiba hawawezi kusimamisha uporaji wa mali yao. Kiburi na fidhuli za watawala wetu za kuendekeza wizi, uporaji wa mali ya umma, rushwa, na ufisadi uliozidi kipimo, vinatokana na udhaifu wa ndani ya Katiba.
Hatuna budi kuanzisha mchakato wa kubadili Katiba ili kuirudisha Serikali na Bunge mikononi mwa wananchi kutoka mikononi mwa vyama vya siasa. Matatizo yetu yatatatuliwaæ; endapo wananchi watakuwa na haki ya kikatiba ya kuwaajiri wawakilishi wao, ambao ni wabunge, na kuwafuta kazi wakati wowote wasiporidhika na utendaji wao wa kazi, na si kusubiri wakati wa uchaguzi peke yake.
Endapo wananchi watakuwa na haki ya kikatiba, kupitia kwa wawakilishi wao, kumfuta kazi kiongozi yeyote wa kuteuliwa au kuchaguliwa, na hata kumfunga jela, kama amekiuka kanuni za uongozi ambazo wananchi watajiwekea.
Endapo kupitia kwa wawakilishi wao, wananchi watakuwa na haki ya kikatiba ya kumshitaki Rais, ama akiwa madarakani, au akiwa amekwisha kustaafu, kama amejihusisha na matendo yanayopingana na kanuni za uongozi watakazo kuwa wamejiwekea.
Endapo kikatiba, utashi wa wananchi utakuwa ni wa mwisho, na hakuna kiongozi atakaye kuwa na mamlaka ya kuupinga. Endapo haki za wananchi walizopewa na Mungu hazitawekewa masharti ya aina yoyote.
Watawala wanaujua fika udhaifu wa Katiba, lakini kwa sababu inawawekea mazingira mazuri na kuwakinga na maovu wafanyayo, wako tayari kuilinda kwa udi na uvumba. Lakini inapotokea kwamba baadhi yao wamewekwa kando, au wanapohamia vyama vya upinzani, basi ndipo wanapofichua udhaifu wake.Wanasimama juu ya Katiba na kuanza kuwavurumushia makombora wale waliobaki madarakani.
Mfano, Horace Kolimba alipokuwa Katibu Mkuu wa CCM, hakuwahi kutoa mapendekezo ya kubadili Katiba, lakini alipojiengua kutoka CCM, ndipo alipoanza kutoa matamko ya waziwazi ya kutaka Katiba ibadilishwe.
Pius Msekwa hakuwahi kutumia nafasi nzuri aliyokuwa nayo ya Uspika wa Bunge kushawishi mchakato wa kubadili Katiba. Ni majuzi tu alipokuwa benchi, ndipo alipoanza kutoa matamko ya waziwazi ya kutaka Katiba ibadilishwe. Sasa hivi amepata nafasi nzuri ya uongozi wa chama tawala, ambayo kwa maoni yangu, angeweza kutoa changamoto ya kuwashauri wanachama wa CCM ili waweze kuona alichokuwa anakiona ndani ya Katiba wakati yuko benchi. Hata hivyo, sitarajii kumsikia akiongelea tena suala la Katiba, isipokuwa kwa namna ya kulumbana na wapinzani.
Nashauri viongozi wa vyama vya siasa waache kutumia suala la Katiba kama daraja la kuwatimizia maslahi yao binafsi, au maslahi ya vyama vyao, badala yake waliangalie kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.
Kutokana na mienendo mibovu ya wale waliopewa dhamana ya kuongoza nchi, naamini mabadiliko ya Katiba ni suala la muda na hayahepukiki. Ama Serikali ikubali kushauriana na wananchi ili kuweka mazingira ya kuundwa kwa Katiba mpya (upendeleo wangu), kuepusha njia mbaya za kudai Katiba.
Katika kitabu: "Part of my soul went with Him", Winnie Mandela anaeleza kwamba Serikali ya Makaburu ilikataa makubaliano ya amani ya kurudisha haki na uhuru wa raia wa Afrika Kusini.
Anasema hicho ndicho kilichomsukuma aliyekuwa mume wake, Nelson Mandela, kwenda Ethiopia, pamoja na mambo mengine, kupata mafunzo ya kijeshi na kuanzisha tawi la jeshi la ANC, Umkhonto we Sizwe. Katika kitabu: " Long Walk to Freedom", Nelson Mandela anaeleza kuwa alitumia njia za kigaidi kupambana na Serikali ya Makaburu kwa sababu alifikia mahala akapata funzo kwamba; "It is the oppressor who defines the nature of the struggle" (tafsiri isiyo rasmi, dhulumati ndiye anayebainisha mwelekeo wa mapambano).
Anasema hicho ndicho kilichomsukuma aliyekuwa mume wake, Nelson Mandela, kwenda Ethiopia, pamoja na mambo mengine, kupata mafunzo ya kijeshi na kuanzisha tawi la jeshi la ANC, Umkhonto we Sizwe. Katika kitabu: " Long Walk to Freedom", Nelson Mandela anaeleza kuwa alitumia njia za kigaidi kupambana na Serikali ya Makaburu kwa sababu alifikia mahala akapata funzo kwamba; "It is the oppressor who defines the nature of the struggle" (tafsiri isiyo rasmi, dhulumati ndiye anayebainisha mwelekeo wa mapambano).
Labda inawezekana kuwa kuna hoja kwamba Serikali ya Tanzania ni ya kuchaguliwa na wananchi na wala si ya Wazungu wachache kama ilivyokuwa Serikali ya Afrika Kusini. Hivyo ni makosa kuhalalisha njia haramu za kigaidi kama zile za Mandela dhidi ya Serikali halali iliyochaguliwa na wananchi kama ya Tanzania.
Jibu la hoja hii ni kuwa, Mandela si tu kwamba alipinga Serikali ambayo haikuchaguliwa na raia wote wa Afrika Kusini, bali alipinga sera zilizosimamiwa na hiyo Serikali. Mandela alipinga sera zilizowanyangÕanya raia ardhi bila mafao ya maana. Sera za makampuni ya kibeberu za kuwatumikisha raia bila ujira wa maana. Sera za kazi na mifumo ya kodi iliyopendelea makampuni ya kibeberu dhidi ya makampuni duni ya raia wa Afrika ya Kusini.
Sheria zilizowapendelea watawala na kuwanyanyasa watawaliwa na ambazo zilitungwa bila mashauriano au ridhaa ya wananchi, na mengineyo. Umuhimu wa Serikali si tu jinsi ilivyoingia madarakani, bali inachosimamia. Pamoja na kwamba Mandela alipata tuzo ya Amani ya Nobel inayoheshimika duniani, lakini udhaifu wa kawaida wa kibinadamu ulimfikisha mahala akapiga teke uvumilivu wa kufikia makubaliano kwa njia ya amani na utulivu.
Ndiyo maana nadhani ni muhimu kwa vyama vya siasa nchini kuacha malumbano katika masuala ya msingi yanayohusu ujenzi wa nchi, na hasa yale ya kuwarudishia raia haki zao za msingi.
Kutoka Raia Mwema wiki ya kwanza ya 2008.
1 comment:
Kama tu ungejua yanayotekea Marekani hasemwi wala kuongelewa kwa uaminifu katika media na viundo mbinu. Kwani zapatikana nguvu kubwa zinazofanya kazi juu ya sheria.
Post a Comment