
yapo pia Tanzania-Uchambuzi
Na Elias Msuya
INGAWA kugombea madaraka na hata watu kuuana kwa ajili hiyo si jambo la ajabu wala jipya kutokea katika historia ya mwanadamu, lakini kutokana na maendeleo ya kifikra na mabadiliko ya kiitikadi vitendo vya kikatili na wizi katika kupata madaraka si vitendo vinavyoweza kustahmiliwa tena.
Wakati wa falsafa za akina Marchiavelli za kuwa mfalme anapaswa atumie nguvu zote alizo nazo kulinda ufalme wake zimeppitwa, hivi sasa ni wakati wa matakwa ya wananchi, wakati wa demokrasia ya kina Plato lakini iliyoboreshwa zaidi.
Matukio ya kutisha na kusikitisha yanayosababishwa na siasa na uchu wa madaraka yameshtadi duniani. Nchini Pakistan kiongozi wa upinzani ambaye pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo katika vipindi viwili aliuawa mara baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara huko Rawalpindi. Yanayotokea nchini Kenya nayo hayapendezi kutokea katika zama hizi za demokrasia.
Matukio haya yamedhihirisha jinsi ambavyo wenye madaraka wanavyoisigina demokrasia.
Nchini Kenya hali si shwari. Tume ya uchaguzi ikamtangaza Mwai Kibaki wa PNU kuwa ndiye mshindi wa kinyang'anyiro cha urais na ndani ya saa moja, akaapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya kwa kipindi cha pili.
Hali iliyopo Kenya ni tete na yenye utata mkubwa, hata Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ECK) Samuel Kivuitu
Akasema kwamba hajui vipi Kibaki ameshinda. Hata watazamaji wa uchaguzi wa kimataifa wameupa dosari kubwa uchaguzi huo jinsi ulivyoendeshwa hasa katika kipengele cha kutangaza matokeo yasiyolingana na idadi ya wapiga kura katika baadhi ya vituo.
Kama vile haitoshi, Kivuitu anatoka na tamko la kuwa alishinikizwa kutangaza ushindi wa Kibaki. Akaongeza kusema kwamba wakati alipopeleka hati ya ushindi Ikulu tayari Jaji Mkuu alikuwa Ikulu akisubiri kumwapisha Kibaki haraka haraka. Huku si ndiyo kupora madaraka kwa kuisigina demokrasia?
Emilio Mwai Kibaki alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2002 kwa tiketi ya NARC aliwaahidi Wakenya kwamba angetaka kutawala kwa muhula mmoja tu wa miaka mitano. Lakini kama alivyowahi kuuliza Mwalimu Nyerere, kwamba Ikulu kuna biashara gani? Labda suala hilo watujibu watu wanaopenda kung´ang´ania madaraka, kuna nini huko?
Kutokana na ushindi wa Kibaki wenye utata, hali usalama ya Kenya kwa sasa ni mbaya. Kuna mauaji ya kutisha na uharibifu wa mali usiomithilika. Wananchi wameshindwa kuvumilia sasa wanaingia mitaani kumpinga Kibaki.
Hali hii imewafanya viongozi wa mataifa mbalimbali kusita kuutambua ushindi wa Kibaki na sasa wanawashauri Kibaki na Raila Odinga watafute suluhu. Suala la kuvurugwa kwa demokrasia ni pana sana, huenda chanzo chake kikubwa ni viongozi hasa wa vyama vinavyotawala kuwa na uroho wa madaraka.
Wanapoingia madarakani kamwe hawataki kutoka. Wanachofanya ni kutumia nguvu za dola ili kujihalalishia madaraka. Wanapoingia madarakani wanaunda kambi ya
ushindi kwa kutumia vyombo vya dola ambavyo hupora sauti ya wananchi.
Kwa mfano tume za uchaguzi nyingi barani Afrika haziko huru. Rais anaunda mwenyewe tume ya uchaguzi na vyombo vya dola humhakikishia ushindi.
Kwa hayo yote, Watanzania tunayo ya kujifunza; usiginaji wa demokrasia tunaousikia kwa wenzetu, hata hapa Tanzania upo. Yanayowapata wenzetu yawe funzo kwetu.
Demokrasia pia husiginwa bungeni. Bunge letu linaongozwa na spika ambaye ni mwanachama wa CCM. Amejaa ushabiki wa chama kiasi ambacho hajali usawa wa siasa anachoangalia ni maslahi ya chama chake tu hata kama hayawasaidii wananchi. Wabunge wa vyama vya upinzani wanapuuzwa na kuburuzwa hata kama wana
hoja za msingi. Hii ni hatari kwa uhai wa demokrasia.
Tunapoanza kumnyooshea kidole Kibaki tuanzie kwetu wenyewe. Kwani yanayoendelea Kenya yana tofauti gani na yanayotokea Zanzibar? Toka nchi hii imerudisha mfumo wa siasa za vyama vingi huko Zanzibar kumekuwa na hali ya machafuko kila mara baada ya uchaguzi mkuu.
Yaliyotokea mara baada ya uchaguzi wa mwaka 1995 tunayajua na ndiyo sababu kuu ya upande wa upinzani hadi leo kudai kuwa walinyang´anywa ushindi.
Hali kadhalika uchaguzi wa mwaka 2000 ambao ulisababisha machafuko baada ya wana CUF kuandamana Januari 21, 2001 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 40 na wengine kukimbilia Mombasa Kenya kama wakimbizi, tunachoendelea kusema ni kwamba umelitia doa taifa, lakini hakuna hatua zozote madhubuti zinazochukuliwa kurekebisha kasoro. Uchaguzi wa mwaka 2005 nao haukuacha kulalamikiwa. Labda hiyo ndiyo kawaida kwa wapinzani kulalamikia uchaguzi lakini inakuwaje katika mazingira ya ushindi wa utatanishi?
Wako wanaoona kwamba tatizo la migogoro mingi ya kisiasa barani Afrika ni kuwapo kwa katiba mbovu zisizokwenda na wakati. Hivyo sasa wakati ufike tuanze kushughulikia tatizo badala ya kushughulikia matokeo.
Elias Msuya ni mchangiaji wa makala wa Gazeti la Mwananchi.
Simu ya mkononi: 0754 897 287
No comments:
Post a Comment