Wednesday, February 06, 2008


Buzwagi yachunguzwa


* Ujenzi wa maghorofa BoT pia wamulikwa
* Pia umo mkataba wa makaa ya mawe Kiwira

* Waziri Marmo asema kazi bado inaendelea


na godfrey dilunga, dodoma

SERIKALI unafanya uchunguzi wa mikataba mbalimbali iliyoibua maswali miongoni mwa wananchi, ukiwamo mkataba wa mgodi wa dhababu wa Buzwagi, ambao ulivuma sana katika vyombo vya habari mwaka jana.

Mkataba huo ambao utiaji saini wake mjini London Uingereza ndio ulioibua maswali mengi, ulivuma katika vyombo vya habari baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, kuuibua na kisha kusimamishwa ubunge baada ya kupatikana na hatia ya kulidanganya Bunge.

Pamoja na mkataba wa Buzwagi, mikataba mingine inayochunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni ujenzi wa maghorofa pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Philip Marmo, ndiye aliyelieleza Bunge mjini hapa jana kuwa uchunguzi wa mikataba mbalimbali ambayo imepigiwa kelele na wananchi unafanywa, ingawa hakueleza wazi wazi uchunguzi huo utakamilika lini.

Marmo, alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM).

Mkataba wa Buzwagi ni moja ya sababu za adhabu ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge aliyopewa Zitto wakati wa Mkutano wa Nane wa Bunge.

Mkataba huo ulitiwa saini hotelini, jijini London, Uingereza, Februari mwaka jana, katika mazingira ya kutilia shaka na kuibua maswali juu ya uharaka wa mkataba wenyewe kiasi kwamba ikaamuliwa usainiwe hotelini nje ya nchi.

Kabla ya kuuliza swali, Dk. Chegeni alitoa maelezo akisema suala la rushwa limechukua sura mpya siku za karibuni na kusababisha manung’uniko katika jamii, licha ya jitihada za kupambana na rushwa zinazofanywa na TAKUKURU.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Dk. Chegeni alitaka kujua hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kashfa nzito za rushwa kubwa zinazohusisha taasisi kama ujenzi wa maghorofa pacha ya Benki Kuu, mikataba ya madini na nishati.

Pia mbunge huyo alitaka kujua ni watu wangapi wamefikishwa katika vyombo vya sheria wakihusishwa na ufisadi huo na Serikali inatoa wito gani kwa jami dhidi ya rushwa serikalini na katika vyama vya siasa.

Akijibu, Waziri Marmo alisema Serikali kupitia TAKUKURU, ilianza uchunguzi wa mikataba mbalimbali na kutaja baadhi ya tuhuma ambazo taasisi hiyo inazifanyia kazi.

Kwa mujibu wa Marmo, kati ya tuhuma hizo ni mkataba huo wa Buzwagi na mkataba wa ukaguzi wa hesabu za kampuni za uchimbaji madini, kati ya kampuni ya Alex Stewart Assayers na Serikali.

“Mkataba mwingine ni wa uchimbaji dhahabu katika eneo la Buzwagi, Shinyanga, kati ya kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick na Serikali ya Tanzania na mkataba wa machimbo ya makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya,” alisema.

Aliendelea kujibu akisema; “Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa inafanya uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za Serikali katika mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya Benki Kuu.”

Hata hivyo, alisema hakuna mtu yeyote hadi sasa aliyefikishwa mahakamani, kwa kuwa uchunguzi katika kashfa hizo unaendelea na hakutaja uchunguzi huo utakamilika lini na kama kuna muda maalumu ambao TAKUKURU imepewa ili kukamilisha uchunguzi huo.

“Kwa upande wa vyama vya siasa, jamii inatakiwa kufahamu kiongozi anayechaguliwa katika misingi ya rushwa atakuwa madarakani kwa manufaa binafsi na si kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Ni wajibu wa wanachama wa vyama vya siasa kusimamia ipasavyo mapato na matumizi ya fedha katika vyama vyao, ili kudhibiti ubadhirifu wa fedha hizo, na wawe na ujasiri wa kuwanyima kura wagombea wanaowarubuni kwa kuwapa rushwa au zawadi na ahadi zisizotekelezeka,” alisema.

Kuhusu viongozi wa siasa, Waziri Marmo alisema viongozi hao wana wajibu wa kuweka na kusimamia mikakati ya kuzuia na kupambana na rushwa ndani ya vyama vyao.


No comments: