*'Magaidi' ziara ya Bush waachiwa
Na Gladness Mboma na Eben-Ezery Mende
Na Gladness Mboma na Eben-Ezery Mende
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Bw. Laurence Masha ameibuka na kumtetea mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Bw. Ridhiwani Kikwete kufuatia kuhusishwa kwake na ufisadi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutokana na ajira yake.
Kuhusishwa kwa Bw. Ridhiwani kumekuja baada ya gazeti moja (sio Majira ), kudai mtoto huyo ameajiriwa na anafanya kazi kwenye kampuni inayodaiwa kushiriki kusajili Kampuni ya Deep Green Finance Ltd ( DGF) inayotuhumiwa kukwapua mabilioni ya fedha katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Gazeti hilo linalotolewa kila wiki, lilidai kuwa na taarifa kwamba Kampuni ya Mawakili ya IMMA Advocates and Co. anayofanya kazi Bw. Ridhiwani, ndio ilisadia usajili wa DGF inayotuhumiwa kuchota sh. bilioni 8 kutoka BoT.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bw. Masha alisema alishtushwa na taarifa zilizochapishwa na gazeti hilo na kumhusisha Bw. Ridhiwani na ufisadi wa BoT.
Akifafanua jambo hilo,Bw. Masha alisema wakati akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya DGF inayousishwa na ufisadi huo, walikuwa na utaratibu wa kuchukua wanafunzi wa mazoezi katika fani ya sheria kila mwaka.
"Wanafunzi walioonekana wanafanya vizuri katika mazoezi kampuni ilikuwa ikiwaajiri watano kila mwaka, ambapo Bw. Ridhiwani ni miongoni mwa wanafunzi waliofanya vizuri na kuajiriwa na kampuni hiyo,"alisema Bw. Masha.
Alisema kuajiriwa kwa Bw. Ridhiwani kulifanyika wakati Baba yake ( Rais Kikwete) hajawa Rais na wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Bw. Masha aliongeza kuwa wakati Bw. Ridhiwani anajiriwa katika kampuni hiyo, Baba yake alikuwa hajaonesha dalili zozote za kutaka kuchukua fomu za kugombea urais.
Alisema kinachoonekana sasa ni kwamba huenda baadhi ya watu hawataki mtoto huyo aendelee kuwepo kwenye nafasi hiyo kwa dhana kwamba kuwepo kwake hapo,'kuna mkono' wa baba yake.
"Inashangaza sana watu wanataka tumfukuze Ridhiwani kwa sababu baba yake amekuwa Rais, kwa mantiki hiyo mtoto wa Rais aajiriwe katika ofisi zipi ? "alihoji Bw. Masha.
Akizungumzia mtoto wa Rais wa Zanzibar, Bi. Fatuma Karume ambaye naye anafanyakazi kwenye ofisi hiyo, alisema kuwepo kwake katika ofisi hiyo kulitokana na uwezo mkubwa wa utendaji alionao.
Bw. Masha alisema awali, Bi. Fatuma alikuwa akifanya kazi kwenye kampuni yake na walikuwa wakisaidiana mambo madogo madogo na baadaye kampuni hiyo iliamua kumchukua baada ya kuafikiana.
Alisema kutokana na taarifa zilizotolewa na gazeti hilo kampuni hiyo inaangalia hatua gani itachukua dhidi ya tuhuma hizo na kwamba yeye hawezi kuzungumzia sasa kwa sababu hahusiki kwa kuwa kuna uongozi mwingine.
Akizungumzia kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw. Masha alisema watu wengi wamekuwa wakihoji kupewa wadhifa huo mzito katika umri mdogo.
Aliwataka watu hao kutambua kuwa yeye alianza kuongoza kampuni kubwa nchini tangu mwaka 1991 .Alisema utendaji wake mzuri wa kazi ndio ulimfanya aonekane anafaa kuongoza nchi katika umri wake wa sasa wa miaka 38.
"Leo hii ukiniuliza ni kwa nini nimeteuliwa kuwa waziri sina jibu,sikujiteua mimi na jibu hilo lipo katika ngazi ya uteuzi, wakaulizwe walioniteua,"alisema Bw. Masha.
Wakati huo huo watu tisa wanaotuhumiwa kutaka kufanya ugaidi wakati wa ziara ya Rais George Bush wa Marekani nchini mwezi uliopita, wameachiwa huru.
Waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Masha alisema watuhumiwa hao wa ugaidi waliachiwa huru Februari 18 mwaka huu baada kufanyiwa uchunguzi wa awali.
Alisema pamoja na kuachiwa huru, bado taratibu za uchunguzi zinaendelea na itakapobainika kuwa walitaka kujihusisha na vitendo hivyo vya kigaidi hatua za kisheria dhidi yao zitachukuliwa.
Bw. Masha alisema waraka aliotumiwa na Waislamu kuhusiana na watuhumiwa hao,ataujibu na kufafanua kwamba awali hakuwza kuujibu kutokana na waraka huo kusambazwa kwenye vyombo vya habari.
"Hawa watu walionitumia barua kutaka msaada wangu, walikuwa hawahitaji msaada wenyewe, ila walikuwa wananifikishia taarifa,"alisema Bw. Masha.
Alisema kuwa hata hivyoanajiandaa kuijibu barua hiyo kwa sababu inamhusu na inahitaji majibu.

1 comment:
Hive, kama Waziri wa nchi, ambaye kwanza aliomba kuwa mbunge, na kisha akateuliwa kuwa Waziri, na hajui ni kwa nini ameteuliwa kuwa waziri, hasa wa nafasi nyeti kama Waziri wa Mambo ya Ndani- si ni ajabu hiyo?
Senata Kennedy aliulizwa, ni kwa nini unataka kuwa Rais wa Marekani akashindwa kutoa jibu la maana. Na akshindwa vibaya mnno katika kinyanganyiro cha uteuzi kupitia Democrats. Sasa huyu Waziri wetu anafanya nini?
Anatakiwa kujiuzulu-maana hata kazi anayoifanya haju anatakiwa ku-deliver nini.
Hii ndiyo hasara ya kuteua marafiki kuwa katika ngazi kubwa za uongozi.
Si ajabu hata na Rais naye hajui ni kwa nini aliomba kuwa Rais, maana kama unaomba nafasi kubwa kama ya u-Rais alafu kichwani umejaza fikra za kujaza marafiki serikalini, itakuwa hakuna tofauti na club ya marafiki. Na hii ndiyo sababu nadhani mpaka leo Kikwete anaendelea kumpamba Lowassa wakati anajua wazi kuwa ni Fisadi mkubwa. Ni aibu lakini tufanyeje wakati watu wengi waliangalia sura.
Inabidi tutafute watu wakutupa pole tu, labda tutafarijika.
Post a Comment