Saturday, March 22, 2008

Mgonjwa asimulia yaliyompata saluni

WIKI moja baada ya HabariLeo Jumapili kuchapisha habari ya kuenea kwa saluni za kuchua ambazo zimegeuzwa madanguro baadhi ya watu waliokwenda kwa maelekezo ya madaktari wamelalamikia hatua ya wahudumu wa saluni hizo kulazimisha kufanya ngono.

Kwa mujibu wa baadhi ya watu waliowahi kukutana na hali hiyo walisema hata kama mtu anakwenda kwa huduma ya kuchua kwa ajili ya matatizo ya viungo vya mwili kama madaktari wanavyowaagiza, lakini wahudumu katika saluni hizo wengi wao wakiwa wanawake wamekuwa wakiwashawishi wateja kufanya ngono.

Mkazi mmoja wa jijini Dar es Salaam akizungumza na HabariLeo Jumapili alisema yeye binafsi alikuwa na matatizo ya mgongo na baada ya kupata huduma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, daktari alimshauri akapate huduma ya kuchua.

Alisema kutokana na maagizo ya daktari alijaribu kwenda katika saluni ambazo zimesambaa maeneo mbalimbali ya jiji na kila sehemu alipata huduma ya kuchuliwa mgongo, lakini mwisho wa huduma hiyo alikuwa akiulizwa kama anataka kufanya ngono baada ya kuchuliwa kwa malipo zaidi.

“Mimi pia nilipitia kama saluni nne hivi baada ya kushauriwa na daktari, nilikwenda ya kwanza kuchua mgongo mhudumu akaniuliza kama nataka huduma nyingine… na bila kutarajia nikamuuliza huduma nyingine ni nini? Ndipo nilipoelezwa kuwa kuna huduma ya ngono kama nataka.

Ilibidi nibadilishe saluni ile kwa kuwa mimi mtu mzima si vizuri kuingia kwenye ngono bila kutarajia, lakini kila saluni niliyokwenda kuchua mwisho wa yote ilikuwa ni kuniuliza kama nataka kufanya ngono. “Nilijikuta nikienda kama saluni nne hivi ili kuona kama ni tofauti, lakini zote utaratibu ulikuwa hivyo nikaona bora nijiachie tu, ” alisema.

Kwa mujibu wa shuhuda huyo hali hiyo ilimtia woga akaamua kuachana kabisa na saluni hizo kwa kile alichokieleza kukwepa vishawishi ambavyo vingemtumbukiza katika mambo yasiyofaa na hivi sasa anahudumiwa Muhimbili.

Alitaja baadhi ya sehemu zinazopatikana huduma hizo kuwa ni pamoja na maeneo ya kufanyia mazoezi ya viungo, katika baadhi ya saluni kubwa maeneo ya Masaki na hata mahoteli makubwa ya hapa jijini Dar es Salaam.

Aidha uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na gazeti hili kwa wiki kadhaa uligundua kuwa baadhi ya saluni hizo ambazo kwa kawaida zilikuwa zikiendesha huduma za kunyoa nywele na kusafisha uso maalumu kwa wanaume, sasa zimekuwa zikitoa huduma za masaji katika eneo lolote la mwili analotaka mteja.

Lakini pia kuna saluni nyingine ambazo ni maalumu kwa ajili ya kuchua na kukanda mwili, lakini zote zinatoa huduma zinazofanana katika kufanya masaji, huduma inayoonekana kupendwa na watu wa rika zote hapa jijini Dar es Salaam ingawa kwa baadhi ya watu wamekuwa wakipata woga na kuamua kuachana na saluni hizo kwa kuogopa vishawishi.

Pia baadhi ya wawekezaji wameamua kufungua huduma hizo kwa kuwafuata wateja nyumbani kwao kwa gharama ambazo wataelewana na bila woga wasichana wanaofanya shughuli hiyo huwa tayari kwa ngono.

Chanzo: Habari LEO

No comments: