Na Elias Mhegera
UAMUZI wa kuhamishia makao makuu ya Chama na Serikali mjini Dodoma ulifanyika katika awamu ya kwanza ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Hata hivyo, hivi karibuni Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda ameonyesha ugumu wa azma hiyo kutekelezwa.
Inabidi tukiri sasa, kwa mwenendo wa mambo ulivyo, inaonekana katika mambo ambayo yanaweza kuingizwa katika kumbukumbu kuwa ni maamuzi yanayoonekana kuitatiza sana Serikali basi ni uamuzi huo.
Kwa miaka kadhaa Serikali imekuwa ikitoa maelezo kwamba uamuzi wa kuhamia Dodoma bado upo pale pale, lakini kivitendo inaonekana hilo limeshindikana na badala yake kuna kila ishara kwamba serikali imedhamiria kubakia jijini Dar es Salaam.
Je, ni kwa nini basi Serikali isitangaze tu kwamba uamuzi wa kuhamia Dodoma umebatilishwa? Maana yangu ni kwamba kuendelea kuahidi jambo ambalo una uhakika kwamba huna uwezo wa kulitekeleza kunaweza kukushushia heshima yako na pia kuwafanya watu wasiamini ahadi zako nyingine.
Nitatoa mifano michache kuhusiana na maamuzi yasiyotekelezwa na ambayo yanawanyima haki wananchi katika ujumla wao. Mojawapo ya maamuzi ambayo ni lile la uamuzi uliotolewa mwezi Mei, 2006 na Mahakama Kuu uliopitishwa na jopo la majaji watatu Amir Manento, Salum Massati, na Thomas Mihayo, ukiruhusu kuwapo kwa wagombea binafsi katika chaguzi zetu.
Upo pia mlolongo wa matukio ya maamuzi yenye utata na yasiyozingatia maslahi ya Taifa. Kwa mfano uteuzi wa watu wenye kashfa sehemu moja na kuwapeleka sehemu nyingine, hilo limewahi kujitokeza ambapo mmoja wa walioteuliwa kuwa balozi wetu nchini Marekani aliwahi kuhusika katika uagizaji wa kivuko kibovu ambacho hatimaye kilisababisha kuangamia wa maisha ya Watanzania.
Upo ule mpango wa usafiri kwa wanafunzi wa Dar es Salaam, zoezi hilo liliratibiwa na Jumuia ya Umoja wa Vijana wa CCM. Matokeo yake mradi huo uliwanufaisha wajanja wachache ambao waliufilisi mradi huo na mpaka leo watu hao bado wanapeta na nyadhifa nzito serikalini.
Miaka kadhaa nyuma aliyepata kuwa waziri katika Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Bw. Jackson Makweta aliamua kuisafisha wizara yake kutokana na tuhuma za uuzwaji wa skolashipu za nje hata hivyo uamuzi huo ulimtokea puani kwani yeye ndiye aliyesafishwa na kuanzia wakati ule hajapata kuingia tena katika Baraza la Mawaziri.
Lakini Je, tumefanya tathmini ya kina kuhusu baadhi ya wale 'aliowasafisha’ katika wizara yake si baadhi yao ndiyo hao hao ambao leo wanatuhuma za kuhujumu mali ya umma? Kumbe basi jitihada zake zilistahili kuungwa mkono badala ya kupingwa.
Majowapo ya mambo ambayo Serikali imekuwa na kigugumizi cha kuyatekeleza ni pamoja na mapendekezo ya kuwashirikisha wapinzani katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Mapendekezo ya awali yalipitishwa katika mazungumuzo ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuia ya Madola Chifu Emeka Anyouku.
Serikali pia haikuchukua hatua zinazostahili kwa wale wote ambao walituhumiwa kuhusika katika vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa Watanzania ndani ya nchi yao wenyewe katika kuwahamisha wakazi wa Bulyanhulu ili kupisha ujenzi wa mgodi wa dhahabu mwaka 1996. jambo hilo liliiabisha nchi miongoni mwa jumuiya ya kimataifa kwa mujibu wa jarida la 'Africa Confidential,' toleo namba 18, Septemba 2001.
Katika tafakuri yangu leo, nimebaini kuwa ucheleweshaji wa uamuzi wa kuhamia Dodoma umesababisha baadhi ya watu kujinufaisha kwa kuiba mamilioni ya pesa ambazo zilitolewa kwa ajili ya Mamlaka ya Uendelezaji wa Makao Makuu Dodoma (CDA) na bado Serikali itaendelea kuingia hasara kubwa kwa kupekeka miradi, ofisi na programu mbalimbali za kiserikali, lakini viongozi wote wako Dar es Salaam.
Wahenga walionya kuwa la kuvunda halina ubani, hivi vigugumizi vya maamuzi nyeti vitaendelea kuligharimu taifa hasara nyingi na kubwa iwapo hatutafikia mahali na kusema sasa basi kila jambo na lihitimishwe au iwekwe bayana kuwa limeshindikana na wahusika waombe radhi. Najua mko Butiama, jifunzeni, Mwalimu alipata kukiri makosa yake kadhaa, alikuwa muungwana!
*Mwandishi wa makala haya anapatikana kupitia baruapepe: mhegeraelias@yahoo.com. Simu: 0754 826272
2 comments:
Yes, I am Elias Mhegera, an author of the article. I appreciate that others can see sense in my argument.
From,mhegeraelias@yahoo.com
Mhegera,
Tupo wengi tunaokubaliana na mawazo yako, aluta continua! Abravo Africano!!!
Post a Comment