Saturday, April 19, 2008

AYA ZA AYAH

Nani haini?


Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.


Mpenzi Frank,


HABARI za maisha? Habari za kupigania maisha? Au tuseme kupigania uhai maana mafisi wa taifa wanataka kutunyan’ganya uhai kwa kutugeuza mizoga ili tuwe mboga kwao.

Ni ajabu sana hadi leo bado mafisi wanakula, mikampuni yao inakula, lakini sisi tunaendelea kuteseka. Wanatujali kweli? Tena nimeshangaa sana mabosi kudai eti hawana nguvu ya kuwakomesha mafisi kwa sababu mafisi wana hela sana.

Tuna serikali kweli? Au ni seri-laini? Au ni seri-oga? Mambo mengine yanakatisha tamaa. Watu wanaachiwa ili waneemeke halafu wanazidi kuachiwa tena kwa sababu wameneemeka kiasi kwamba noma haiwezi kuwafikia. Si bora tusiwe na serikali kabisa.

Lakini hayo sitaki hata kufikiria maana nikiangalia maisha ya neema ya bosi wangu na wenzie, najiuliza kwa nini tumpe marupurupu yote hayo kama hawezi kutetea maslahi yetu. Ana faida gani kwetu?

Tena juzi katoa mpya, kidogo azue mikiki na makeke nyumbani humuhumu. Alikuwa amerudi kutoka nchi ile ya nduli huku akifurahia maneno mapya ya kinduli.

‘Unajua mke wangu, yule jamaa anajua kazi yake sawasawa. Katangaza kwamba yeyote anayeambukizwa virusi vya UKIMWI si fisadi tu, ni haini kabisa. Amesaliti taifa.’

MB akashtuka, akamwangalia mume wake kwa jicho la ukali sana lakini hakusema neno. Ila BB, kama kawaida yake alidaka papo hapo.

‘Ni haini kwa vipi baba?’

‘Tumia akili mwanangu. Serikali imejitahidi. Imetumia pesa kibao kutengeneza vipindi vya redio, na mabango makubwamakubwa, kuwaambia watu kubadili tabia. Imegawa kondomu kila mahali. Imewaambia watu wasifanye ngono kabisakabisa. Na bado wanafanya tendo la uambukizo. Ni haini.’

‘Yaani baba hadi leo mafisi wanaendelea kula nchi yetu. Wametengeneza mikataba ya kufanya hata wajukuu wangu waendelee kunyonywa. Ili wale wao, wamesababisha walio wengi washinde na njaa, au tuseme washindwe na njaa lakini wao si haini. Haini ni yule ambaye ameambukizwa katika kutafuta maisha kwa sababu mafisi wakubwa wamekula matarajio yake yote?’

Bosi akatingisha kichwa.

‘Yaani wewe mwanangu kazi yako kukosoa tu. Kwani mimi nimesema kwamba mafisadi ni wazuri? Naongelea watu wengine sasa. Hata hapa tunaiita ngono zembe. Sasa mwenzetu amesema si ngono zembe bali ni ngono haini.’

‘Lakini baba ninachojaribu kukuambia ni kwamba ngono hizi nyingi zinatokana na ufisi wa hawa wengine. Hebu angalia hali ya sisi vijana …

Baba alishusha pumzi kwa nguvu.

‘Ohoo umeanza vijana vijana … vijana vijana. Kwani hatuwasomeshi?’

‘Zaidi ya nusu ya vijana wa umri wangu hawapo shule.’

‘Kosa la nani? Tumehangaika kuwajengea shule. Kwa mfano, jimboni mwangu, tumejenga shule 15 mpya. Sasa kama tumewaletea maji na wanakataa kunywa nilaumiwe mimi?’

‘Lakini maji yanachoteka?’

‘Una maana gani?’

‘Walimu wapo? Vitabu vipo? Kukaa kwenye dawati kwenye darasa si elimu.’

Bosi akaanza kukasirika.

‘We kinda la juzi usianze kunifundisha kazi yangu. We unajua nini kuhusu magumu ya utawala? Acha kutuona wajinga. Tunajua madawati na madarasa ni hatua ya kwanza. Sasa tunaelekea kwenye hatua nyingine.’

Lakini BB akishaanza labda Osama ataweza kumsimamisha, au yule Osama wa Marekani aliyekuja kutukalia kwa siku nne.’

‘Ni kweli baba, sikatai. Ninachosema tu ni kwamba hayo yalipaswa kuandaliwa kabla ya kushurutisha watu wote wapeleke watoto wao mashuleni. Ni sawa na kuwaita watu kwenye harusi wakati ambapo chakula kimenunuliwa tu, hakijapikwa. Wala moto haujawashwa. Kabla hakijapikwa wengine wengi watakuwa wameondoka. Utawalaumu?’

‘Achana na hayo. Na mimi nakuambia nikisikia na wewe umepata hili gonjwa na wewe nitakuita haini pia.’

Bosi alianza kuondoka kwa ghadhabu kama kawaida yake. Mara nyingine nashangaa kwa nini hapati vidonda vya tumbo wakati anakaa na hasira hizi kila siku. Lakini kabla hajaweza kwenda mbali ghafla mama bosi akaamka.

‘Unamwambia mwanao nini? Wewe na vihawala vyako ndio haini. Ni haini wa familia yetu. Ni haini wa ndoa yetu. Na wewe na wenzio mnafisadisha kila kitu ili mweze kuwa mahaini zaidi.’

Lo mpenzi! Nilidhani kuta zitaanguka. Bosi alipogeuka alikuwa mweusi afadhali mkaa lakini kabla hajaweza kusema neno, MB keshaendelea.

‘Toka hapa fisadi mkubwa wewe. Unafikiri mimi sijui pitapita zako? Unatumia kondomu na wewe? Haini mkubwa, mkubwa kabisa.’

Kisha MB kakaa chini na kuanza kulia kwa nguvu. BB alijaribu kumbembeleza lakini mimi niliona si vizuri nishuhudie mambo hayo maana waweza kulaumiwa tu baadaye kwa kuona tu. Hivyo nilijisunda zangu kimyakimya hadi jikoni nikakaa huko hadi MB kaniita baadaye kabisa.

Nilipofika kwake, nikaendelea kana kwamba sijui kitu. MB alijaribu kunidadisi.

‘Ulimwona baba yako akiondoka.’

‘Hapana mama nilikuwa jikoni. Kwani alisahau begi yake?’

MB kaniangalia kwa ukali lakini mimi niliendelea kufanya ukaguzi wa mbali wa makucha yangu ya miguu hadi MB kaonekana karidhika. Lo, mitembo igombane mimi nyasi ninyanyasike?

Lakini ukifikiria mpenzi BB alisema ukweli. Cheki yule rafiki yangu Mwanaharusi. Kumaliza shule tu wazazi wameshamshurutisha na lizee la miaka 55 eti akitoa hela nyingi wataweza kuwalisha wadogo zake wote.

Alipokataa kwamba yeye si kitegauchumi na wao hawawezi kuwekeza kwake wakampiga vibaya sana. Na alipokimbia na kuja mjini kazi iliyopatikana ilikuwa kazi ya ndani tu na ndani hukohuko bosi wake kambaka.

Sasa ana katoto ka mwaka mmoja na UKIMWI juu. Uhaini uko wapi? Hapo nakubaliana na MB kwamba haini ni wale wenye uwezo wanaoharibu nchi kwa kuwaharibu watoto wa nchi yetu. Wakishughulikiwa uhaini wao, sitabisha.

Eniwei, kwa kumaliza mchapo bosi hakurudi hadi saa nane za usiku. Kelele zilizokuwapo zikaniamsha hata na mimi. Lakini sijui mwisho ilikuwaje zaidi ya kwamba baba akawa anachechemea kesho yake na mama akavunjika mkono. Hapo sasa! Nitafanya udaku bila hata futari.

Akupendaye daima bila hata chembe cha uhaini,

Hidaya


mabala@gmail.com


Kutoka Raia Mwema wiki hii



No comments: