Mchwa wakila kila kitu, si
nyumba itawaangukia
na wao pia?
Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.
Mpenzi Frank,
Hali yako mpenzi? Vipi biashara yako? Hebu changamka dia wangu maana kwa jinsi mambo yanavyokwenda hapa naweza kukosa kazi siku yoyote. Si umemwona mwingine tena kaachia ngazi? Kang’ang’ania hadi kanin’ginia kisha hata vidole vilishindwa kazi. Ila tu, wenyewe wakiachia ngazi hapa hawachubuki ngozi hata kidogo. Wanaanguka kwenye sponji ili waweze kwenda kula vizuri visenti vyao.
Lakini bosi hana raha. Hata wenzie wanapokuja wanabaki kujiuliza nani mwingine atafuata. Ingekuwa timu ya mpira, nadhani tayari wangekuwa wameteremshwa daraja au hata kupigwa marufuku kuendelea kucheza. Wanne kutolewa kwa kadi nyekundu!!!! Timu gani hiyo?
Tena mpenzi, kila kadi nyekundu inaniongezea kazi maana wageni wa bosi wanafurika kila mmoja akiwa na ushauri wake kwa bosi. Na kila mmoja anategemea kufaidi msosi wa bosi! Wanabugia pombe na kutaka nyama choma juu yake. Ukiingia jikoni siku hizi utadhani baa ya mitaani inavyonukia harufu ya nyama.
Kaanza mwimbaji mmoja. Si yule ambaye amekuwa mtu wa kuheshimiwa kiasi kwamba ukimcheka ni kosa la uhaini. Ni mwingine mwenye bendi yake. Kaja kwa bosi eti anashtaki wanasiasa wanashusha hadhi ya sanaa.
‘Yaani mheshimiwa, hayo mambo yenu ya ‘usanii’ yanatuharibia kabisa. Nani kasema kwamba sisi wasanii ni waongo. Sisi tunachapa kazi kujitafutia visenti halali kwa kuwaburudisha watu. Lakini sasa kutokana na vitendo vyenu, usanii maana yake ni uongo, ni kuwadanganya watu. Kwa nini uongo usibaki kuitwa siasa tu, kama zamani.’
Nilifikiri bosi atakasirika lakini kumbe yule jamaa ni rafiki yake tangu zamani.
‘Wacha maneno yako wewe. Nani kasema siasa ni uongo?’
‘He rafiki yangu. Kwani hatuna akili. Tunasikiliza ahadi zenu duni wakati wa uchaguzi tunajua mnachezea ukweli tu.’
‘Si ndiyo maana ya usanii. Kwani tunasemaje kabla ya hadithi … hadithi njoo, na uongo njoo utamu kolea.’
‘Sawa kabisa. Bila uongo hakuna stori. Lakini uongo wetu unalenga kufichua ukweli zaidi. Watu wanajua sungura hawezi kuongea kama binadamu lakini katika kuongea kwake anawasaidia wasikilizaji kuangalia kwa namna tofauti. Lakini nyinyi wanasiasa mnapenda kudanganya kwa faida yenu tu, si kwa faida ya wasikilizaji.’
Kwa mara nyingine nilimwangalia bosi kwa wasiwasi nikitegemea mlipuko lakini bosi akaendelea kuchapa wiski yake bila wasiwasi.
‘Lakini nyinyi wasanii hamfanyi hivyo pia. Hebu angalia filamu zinazotolewa siku hizi. Si tu mnatia chumvi, bali mdalasini, iliki na hata pilipili kichaa.’
‘Sikatai lakini bado sitaki kazi yetu ya sanaa kuchafuliwa kwa kulinganishwa na mambo yenu ya siasa. Sanaa ni sanaa Bwana na kama baadhi yenu mnataka kusema uongo, au kutoa stori za kunusuru ngozi zenu, ibaki kuitwa siasa tu. Wasanii hatumo!’
Wakacheka na kuendelea na mambo mengine. Na hata mimi nilicheka niliporudi jikoni. Hebu angalia. Wanasiasa wanajidai bora kuliko wengine ndiyo maana wanalazimisha kuitwa waheshimiwa lakini kazi yao inadharaulika kuliko zote. Hawaoni hivyo? Nilimkumbuka yule jamaa darasani mwetu aliyepewa jina la ‘mwanasiasa’ kutokana na uongo wake.
Ghafla kengele ikalia tena. Nilianza kuchoma nyama tena harakaharaka maana nilijua nitaitwa wakati wowote. Baada ya dakika tano … ‘Hidayaaaaa!’
Kukimbilia huko sebuleni nikakuta marafiki zake wengine wawili. Wakati nawapa chupa zao za wiski (ukiwa kizito mpenzi hupewi glasi, wapewa chupa nzima waweze kujimiminia kwa wakati wako) wale jamaa wengine wakaanza.
‘Rafiki yangu tumekuja na ujumbe mzito. Twaweza kuongea?’
Bosi akacheka akimnyooshea kidole yule msanii.
‘Huyu fyatu huyu. Usiwe na wasiwasi. Tulisoma pamoja sekondari. Ni mwenzetu … hata kama analalamika kwamba sisi wanasiasa tunashusha hadhi ya sanaa.’
Kama kawaida alisahau kabisa kwamba mimi nipo. Kwani mimi ni mtu mbele yao?
‘Basi, sikiliza rafiki yetu. Tunajua wewe ni mheshimiwa mkubwa sana, tena waziri lakini lazima uangalie. Mabaharia wakianza kutupwa nje ya meli kwa sababu wanahatarisha meli yenyewe, ujue meli ina kasoro kubwa sana na inaweza kuzama wakati wowote.’
Bosi akacheka.
‘Acheni jamani. Meli ni imara kabisa. Huoni inavyobeba kila aina ya mtu?’
‘Ndiyo tatizo lenyewe. Meli inakosa mwelekeo maana kila mtu anataka ielekee mahali tofauti ambapo kuna maslahi zaidi kwake? Matokeo yake, meli inagonga miamba na itazama maana mabaharia wanafikiria mambo yao ya ulaji tu.’
‘Si mabaharia wote.’
‘Sawa lakini wenye nia njema wamefunikwa na walaji. Na meli ikizama wenye nia njema watazama nayo. Wakati wa kuondoka ndio huu rafiki yangu. Kwa nini uhusishwe na uozo wa wengine.’
Hapo msanii alicheka.
‘Si nilikuambia Bwana. Neno mheshimiwa limekuwa tusi.’
‘Ah wapi. Tumeshaondoa wabaya kwa kumwondoa huyu wa mwisho. Ni kweli hakupaswa kubaki lakini sasa kaondoka na yeye. Sote tulijua. Lakini sasa mambo shwari na utashangaa meli itakavyokwenda kwa kasi mpya.’
‘Haya Bwana usilalamike meli ikizama kwa kasi mpya. Angalia meli za majirani zetu huko Kenya, Zambia na Malawi. Walijaza mabaharia feki hivyohivyo hadi mwisho walizama na kupotea kabisa.’
Bosi alionekana kutafakari kidogo lakini papohapo msanii akaamka.
‘Hadithi hadithi …’
‘Hadithi njoo na uongo njoo utamu kolea.’
‘Hapo zamani za kale kulikuwa na kundi kubwa la mchwa. Hili kundi lilivamia nyumba ya mwananchi fulani na kuanza kufaidi mbao zote za nyumba. Mwananchi alijitahidi kupambana nao lakini hakuwa na dawa na wale mchwa walijua jinsi ya kujificha sana kiasi kwamba, ingawa aliwaona, alishindwa kuwapata. Basi mchwa waliendelea kula raha mstarehe na kila jioni mwananchi alisikia sauti ya mchwa wakitafuna, wakitafuna, wakitafuna. Hivyo mwisho mwananchi alikata tamaa ya nyumba yake na kuanza kujenga nyingine imara zaidi. Alivyowachoka mchwa hakusubiri hata nyumba mpya iishe akahamia.
Mchwa walimcheka.
‘Sasa tutatafuna sawasawa, bila hata kificho kisha tutahamia hii nyumba yake nyingine na kufaidi tena.’
Sasa wakati huu, nyumba ilikuwa imeshaanza kuyumbayumba, hasa wakati wa upepo mkali maana mbao nyingi zilikuwa karibu zimeisha. Mchwa wengine walianza kushtuka na kuwasihi wenzao waache kula kwa fujo namna hiyo. Na wadudu wengine ambao walikuwa wameweka nyumba zao hapo bila kutaka kula nyumba yenyewe nao walishtuka. Hasa buibui mmoja alijaribu kuwasihi.
‘Jamani acheni kula hivyo. Kwani ni busara kula nyumba unayoitegemea?’
Wakazidi kumcheka
‘Kwenda zako na wasiwasi wako. Tutabanana humuhumu. Utapata wapi nyumba nyingine nzuri kama hii?’
Wadudu wengine walipojaribu kuwashauri wahame ile nyumba, wakachekwa zaidi na zaidi ingawa wawili watatu mwisho walihama huku wakibezwa na mchwa. Lakini ukisindikiza mvua ya mawe. Kukatokea kishindo kikali na mwananchi alipochungulia akakuta nyumba ile imeanguka. Na ilivyoanguka kwa kishindo, hakuna hata mdudu mmoja aliyeponea. Walaji wakubwa, walaji wadogo na hata waliowakasirikia walaji, wote waliishia ndani ya nyumba ile. Hata muda wa kujuta kwa nini hawakuhama ile nyumba hawakuwa nao.’
Msanii kumaliza hivyo, akashika begi yake na kuondoka ghafla bila hata kusema neno zaidi. Bosi akabaki na marafiki zake akishangaa. Na wao pia walisema.
‘Unaona mzee? Kubaki ndani ya meli ambayo haina mwelekeo eti wewe utaweza kuweka mwelekeo ni ndoto ya mchana tu. Tafuta meli yenye mwelekeo kama hutaki kuzama.’
Wao nao wakaondoka na bosi akabaki peke yake hadi saa saba za usiku akiwaza. Nadhani yale maneno yalimwingia kwa nguvu.
Akupendaye kwa mwelekeo thabiti kabisa … na mwenye dawa ya kuangamiza mchwa yeyote anayetaka kuvamia
Hidaya
Kutoka gazeti la Raia Mwema wiki hii.
No comments:
Post a Comment