
Chenge agoma kujiuzulu,
asema ni tuhuma za vijisenti
WAZIRI wa Miundombinu, Andrew Chenge, jana alirejea nchini akitokea China na kukataa kujibu tuhuma za ufisadi wa mabilioni ya shilingi anazodaiwa kuzihifadhi katika akaunti nje ya nchi.
Chenge ambaye aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam jana saa 9:00 alasiri na ndege ya Emirates alisema kwa sasa hawezi kuzungumza lolote kwa vile tuhuma zilizotolewa dhidi yake zinachunguzwa.
"Unapotuhumiwa, uchunguzi unafanyika. Na kwa kanuni na taratibu za uchunguzi, siruhusiwi kuzungumza. Kwa sasa ni mapema mno. Tuvipe nafasi vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yake," alisema Chenge na kuongeza:
"Ninaheshimu na nitaendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya uchunguzi".
Hata hivyo, Chenge ambaye alizungumza mbele ya jopo la waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi, huku akitetemeka na kujikanganya katika kauli, alisema tuhuma zilizotolewa dhidi yake, ni nzito kupita kiasi, hivyo, hawezi kuzijibu kwa kukurupuka, badala yake anaviachia vyombo vya uchunguzi vifanye kazi yake.
"Hoja ya msingi hapa, ni kwamba, nimelipwa fedha na kampuni ya BAE System (ya Uingereza) katika ununuzi wa rada. Tuhuma hiyo ni nzito kweli kweli na siyo ya kupopoa," alisema Chenge.
Alisema taarifa za kutuhumiwa kwake, alizipata akiwa na Rais Jakaya Kikwete China na amerejea nchini kwa taratibu za kawaida na si kwa kukatiza ziara kutokana na kuelemewa na tuhuma zilizotolewa dhidi yake.
"Nafurahi kurudi nyumbani. Tulikuwa China na Rais na ametuwakilisha vizuri. Tulipokuwa China, ndio tukasikia hizo tuhuma za vijisenti," alisema Chenge.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu tuhuma zinazomkabili za kujilimbikizia zaidi ya Sh24bilioni katika akaunti nje ya nchi kuziita vijisenti, Chenge alisema: "Kila mtu ana viwango vyake na ana haki ya kusema anavyotaka. Na mtu akikutuhumu, unajua nafsini mwako".
Pia hakuwa tayari kabisa kujibu tuhuma za kusaini mkataba wa kampuni ya kuzalisha umeme ya IPTL alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), badala ya kushauri, na pia kujibu tuhuma kuhusu mabilioni ya fedha anayodaiwa kuyahifadhi nje ya nchi kama aliyaorodhesha kwenye Tume ya Maadili ya Viongozi, badala yake, alisema: "Yote yaliyosemwa na kuandikwa, mimi siyafahamu".
Alipoulizwa kama yuko tayari kujiuzulu wadhifa wake ili kwa vile ameshatuhumiwa na ili avipe nafasi vyombo vinavyochunguza tuhuma zinazomkabili kufanya kazi yake kwa uhuru, Chenge alisita kutamka suala hilo, badala yake aliishia kusema: "Myonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni" bila kufafanua.
Awali, alisema atatumia fursa ya kuwapo kwake nchini kutafakari tuhuma zote zilizotolewa dhidi yake kisha atawasiliana na mwanasheria wake ili kuangalia uwezekano wa kuvichukulia hatua za kisheria vyombo vya habari alivyodai kwamba, vilivuka mipaka katika kuandika na kutangaza tuhuma dhidi yake.
Alisema atafanya hivyo kwa kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi yake, ni nzito na zimelenga kumchafulia jina.
Tuhuma dhidi ya Chenge za kujilimbikizia fedha hizo, ziliibuliwa na gazeti la The Guardian linalochapishwa nchini Uingereza katika toleo lake la Jumamosi wiki iliyopita ambalo lilieleza kuanza kwa uchunguzi dhidi ya waziri huyo, kutokana na akaunti yake kukutwa na zaidi ya dola 1 milioni.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, taasisi ya kuchunguza makosa makubwa ya jinai nchini humo ijulikanayo kwa jina la Serious Fraud Office (SFO), inatarajia kuanza upya kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo ili kuangalia iwapo zina uhusiano wowote na zile zinazoaminika kutolewa kwa njia ya rushwa wakati Tanzania iliponunua rada ya kijeshi kutoka nchini humo kwa paundi milioni 28, ambazo ni sawa na Sh70bilioni, mwaka 2002.
Gazeti hilo lilieleza katika kuwa uchunguzi huo wa SFO unatarajia kuanza katika kipindi cha wiki sita zijazo.
Kwa mujibu wa habari hizo, uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba, moja ya mambo yanayofuatiliwa ni kujua iwapo fedha hizo zinazoaminika kuwa za Chenge, zilizowekwa katika akaunti moja iliyoko katika Kisiwa cha Jersey zina uhusiano wowote na zile zinazoaminika kutoka katika Kampuni ya BAE System, inayotuhumiwa kuinyonya Tanzania kwa kuiuzia rada hiyo kwa bei kubwa kuliko ilivyotakiwa.
The Guardian katika habari yake hiyo iliyowekwa katika mtandao wa intaneti, liliripoti kuwa taarifa hizo zinakuja ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kwa kushirikiana na SFO na taasisi za uchunguzi za Uswisi na Jersey zilipoanza kuchunguza kuhusu kashfa nzima ya ununuzi wa rada.
Gazeti hilo lilimkariri Chenge akikiri kwamba fedha hizo ni mali yake na akatumia fursa hiyo kukanusha kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha hizo na kashfa nzima ya ununuzi wa rada, uliofanywa wakati yeye akiwa AG katika serikali ya awamu ya tatu.
Siku moja baada ya kuibuliwa kwa tuhuma hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, alikaririwa na gazeti hili akisema kuwa taarifa rasmi zikifika serikalini kuhusiana na tuhuma hizo, sheria itachukua mkondo wake na kuonyesha kushangazwa kwake iwapo Chenge alizipata fedha hizo kihalali au la.
Siku moja baadaye, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kumtaka Rais Jakaya Kikwete amsimamishe kazi Waziri Chenge na awekwe chini ya ulinzi, wakati uchunguzi wa kina wa mali zake ndani na nje ya nchi unafanyika.
Profesa Lipumba alisema anamfahamu vema Waziri Chenge na kwa hiyo, mshahara na marupurupu ya serikali anayolipwa, havimuwezeshi kulimbikiza kiasi hicho cha fedha katika akaunti.
Kabla ya gazeti la The Guardian kuibua tuhuma hizo, Septemba 15, mwaka jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, walimtaja Chenge katika orodha ya vigogo 11, wakiwamo viongozi kadhaa wa serikali nchini wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi wa mabilioni ya shilingi za walipakodi.
Baadaye, Septemba 19, Waziri Chenge aliliambia gazeti hili kuwa walioibua hoja ya ufisadi dhidi ya viongozi wa serikali kama wakipata au kama wana ushahidi, yeye binafsi anatoa ruksa waupeleka katika vyombo husika vya dola ili ufanyiwe kazi.
Hata hivyo, Chenge alithibitisha kwamba yeye ni mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Tangold, ambayo Inamilikiwa na serikali na kwamba hakuna kifungu cha sheria kinachomzuia kuwa mkurugenzi.
"Nasubiri nipate hizo tuhuma kwa maandishi maana siwezi kuzungumza tu bila kuziona, lakini kama ni ukurugenzi Tangold, mimi siyo kwamba niliwahi kuwa mkurugenzi, ni mmoja wa wakurugenzi hadi sasa. Hii ni kampuni ya serikali, tatizo nini?" alihoji Chenge na kuongeza:
"Lakini kama mtu ana ushahidi wa tuhuma za ufisadi, jamani tunavyo vyombo vyetu, si wapeleke zikafanyiwe kazi," alisema Chenge.
Waziri huyo alisema hapendi malumbano, isipokuwa yote yaliyozungumzwa atahitaji kuyaona kwa maandishi na uonyeshwe ushahidi wa yeye kuhusika moja kwa moja na ufisadi uliotajwa.
Februari 12, mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete alitangaza Baraza jipya la Mawaziri baada ya Februari 7, kulivunja baraza la awali ambapo baadhi ya mawaziri na manaibu mawaziri waliachwa na kumteua Chenge kuendelea na wadhifa wake katika Wizara ya Miundombinu.
Hata hivyo, uteuzi wa Chenge kuendelea na wadhifa aliokuwa nao katika wizara hiyo, ulizua mjadala mkali kutoka kwa wananchi, ambao wakidai kuwa hafai kutokana na kuhusika kwake na mikataba mibovu akiwa Mwanansheria Mkuu katika serikali ya awamu ya pili na ya tatu.
Pia baadhi ya wananchi walisema tangu ashike wadhifa huo mwaka 2005 hakuna mabadiliko katika ujenzi wa barabara zaidi ya mafanikio na ufanisi vilivyoachwa na serikali ya awamu ya tatu, ambayo John Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi.
Pamoja na malalamiko hayo ya wananchi, Waziri Chenge aliwaambia waandishi wa habari kuwa hawezi kujiuzulu kutokana na maneno ya watu na kwamba suala la yeye kuendelea kukaa katika baraza hilo aulizwe Rais Kikwete ambaye ndiye aliyemteua.
Chenge alisema hayo mara tu baada ya kuapishwa na Rais Kikwete kuendelea kuiongoza wizara hiyo katika sherehe za kuwaapisha mawaziri katika Ikulu ya Chamwino, mjini Dodoma Februari 13, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment