
'Chenge akamatwe, afilisiwe'
* Wataka aachie ubunge
*Dkt.Slaa azidi kung'aka
Na Reuben Kagaruki
*Dkt.Slaa azidi kung'aka
Na Reuben Kagaruki
WANASIASA nchini wamemtaka aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu, Andrew Chenge, na wengine waliotajwa kwenye orodha ya ufisadi wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa vile kujiuzulu peke yake hakutoshi.
Wameenda mbali zaidi kwa kutaka ajiuzulu hata ubunge na kutaka mali zake alizojilimbikizia zikamatwe na baada ya kesi ikibainika hakuzipata kwa njia halali zitaifishwe.
Akizungumza na gazeti hili leo Mwanasheria wa CHADEMA na wakili wa kujitegemea, Tindu Lissu, amesema Chenge anatakiwa akamatwe na kushitakiwa kwa sababu ni mhalifu kama walivyo wahalifu wengine.
"Chenge alitakiwa akamatwe kwa sababu ni mhalifu kama walivyo wahalifu wengine, tunao ushahidi wa kutosha," amesema Lissu. Amesema kujiuzulu kwa Chenge kumechelewa kwani alitakiwa kufanya hivyo tangu alipotajwa kwenye orodha ya mafisadi katika mkutano uliofanyika Mwembe Yanga miezi nane iliyopita.
Amesema anashangaa ni kwa nini Rais Kikwete hakumchukulia hatua tangu alipotajwa wakati mikataba mingi mibovu imepitia mikononi mwake akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willbroad Slaa, amesema tangu alipotajwa kwenye orodha ya aibu ya mafisadi miezi nane iliyopita alitakiwa awe amejiuzulu na kukamatwa. Amesema haitoshi kujiuluzu uwaziri bali anafanye hivyo hata kwa ubunge.
Dkt. Slaa amesema anaungana na wale wote wanaotaka kwenda kupekua fomu za tamko la mali na rasilimali alizonazo Chenge kwani sheria ya maadili ya viongozi inaeleza wazi kuwa iwapo kiongozi hakujaza au kutoa taarifa zisizo za kweli moja kwa moja anapoteza wadhifa wake ikiwa ni pamoja na ubunge.
Dkt. Slaa amewataka viongozi wengine waliotajwa kwenye orodha ya mafisadi na kutishia kwenda kumshitaki mahakamani wajiuzulu wote kwani kung'oka mmoja mmoja hakutoshi. Amesema viongozi wengine wanaotakiwa kujiuzulu mara moja ni Katibu Mkuu Hazina, Gray Mgonja na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Basil Mramba.
Mwenyekiti wa TPP-Maendeleo, Peter Mziray, amesema sheria ya maadili imeeleza wazi kuwa kiongozi anapovunja sheria hiyo anapoteza wadhifa wake hivyo ana imani kuwa hata Chenge hana sifa ya kuendelea kuwa mbunge na ameitaka Tume ya Maadili kuweka wazi fomu za Chenge kwani kuendelea kukaa kimya kunaibua maswali mengi yasiyo na majibu.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party, Augustino Mrema, amesema Rais Kikwete, alitakiwa kumtimua Waziri Chenge kwa dharau "Tatizo rais wetu ni mwoga, kujiuzulu kwake hakuna busara yoyote ni fedheha na aibu kubwa kwa CCM," amesema Mrema.
Amesema ni jambo la kusikitisha kuona mawaziri wanne wanajiuzulu nyadhifa zao ndani ya kipindi cha miaka miwili na nusu. Amesema kitendo alichokifanya Chenge si cha kishujaa bali ni mwendelezo wa vitendo vya kifisadi. Ameshauri Rais Kikwete awaondoe mafisadi wote waliotajwa kwenye mkutano wa Mwembe Yanga na kuteua watu waadilifu.
Gazeti moja maarufu la Uingereza liitwalo The Guardian siku chache zilizopita, lilichapisha habari na kuzisambaza kwenye mtandao wa intaneti likiweka wazi kwamba Chenge anachunguzwa kwa kuchimbia sh. bilioni moja kwenye akaunti yake iliyoko nje ya nchi anazodaiwa kuzipata kwa njia ya ufisadi.
Gazeti hilo likasema kwamba taasisi moja makini ya kuchunguza makosa ya jinai nchini Uingereza ijulikanayo kwa kimombo kama Serious Fraud Office (SFO) inafanya uchunguzi ili kuona kama zinahusiana na zile zilizotolewa kwa njia ya rushwa katika ununuzi wa rada ya kijeshi.
SFO inachunguza tuhuma kwamba vigogo wa serikali ya Tanzania na wafanyabiashara kadhaa nje na ndani ya nchi, walikula njama kununua rada ya kijeshi kutoka Uingereza kwa sh. bilioni 70 mwaka 2002 kiasi ambacho ni karibu mara dufu ya bei yake halisi.
Katika dili hilo, inadaiwa kwamba kampuni ya BEA Systems ambayo ndio ilikuwa dalali katika biashara hiyo mbovu, ilitoa hongo ya jumla ya dola za Marekani bilioni 12 ili kuwapoza maafisa wa serikali wafanye juu chini kuhakikisha kwamba Serikali ya Tanzania inanunua rada hiyo kwa bei mbaya.
Maafisa wa SFO walitinga nchini mwezi huu na kumpekua Chenge jijini Dar es Salaam na kisha kuhojiana naye kuhusu tuhuma hizo kabla ya kwenda Uingereza na kukuta amechimbia sh. bilioni moja kwenye akaunti yake. Chenge amekiri kwamba kweli pesa hizo ni zake.
Chenge mwenyewe aliporejea kutoka ziarani Ulaya wiki iliyopita alilalamika kwamba anasingiziwa na maadui zake kisiasa na kwamba hakupata pesa hiyo kwa ufisadi bali kwa mihangaiko yake mwenyewe na kwa maana hiyo asingeweza kujiuzulu kwa sababu tuhuma hizo zilikuwa bado zinachunguzwa.
Baada ya kubanwa na waandishi wa habari kuhusiana na tuhuma hizo, aliziita shilingi bilioni moja zilizokutwa kwenye akaunti yake katika akaunti binafsi nchini Uingereza kwamba ni vijisenti, lakini akaja kuomba radhi baadaye kwamba kwa lugha yao ya kisukuma neno vijisenti lina maana na pesa, iwe ndogo au nyingi.
Chenge amejiuzulu wakati taifa likiwa kwenye mjadala mzito kuhusu tuhuma za ufisadi zinazowahusisha moja kwa moja viongozi wa serikali wakiwamo wanasiasa wakongwe akiwemo waziri mkuu aliyejiuzulu pamoja na mawaziri wengine wawili kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Habari hizo zimekuja wakati viongozi wengi wa Afrika wakishutumiwa kuweka mabilioni ya dola kwenye mabenki ya nje ya nchi huku Waafrika wakiendelea kukosa pesa ambazo zingewasaidia kuboresha maisha yao.
No comments:
Post a Comment