Saturday, April 19, 2008



Chenge aomba radhi


* Ni kwa kauli yake ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Jumatano
* Asema hakuwa na maana mbaya, usukuma wake umemwathiri
* Asisitiza hana nia ya kuvishitaki vyombo vya habari vilivyomwandika

na mwandishi wetu

WAZIRI wa Miundombinu, Andrew Chenge, amewaomba radhi Watanzania kwa kuziita fedha zaidi ya Sh bilioni moja zilizokutwa kwenye akaunti yake nchini Uingereza 'visenti'.

“Sikuwa na maana mbaya, pengine nimeathirika na utamaduni wa Kisukuma, kwetu sisi tumezoea kusema vijisenti, visichana na vitu kama hivyo, nawaomba radhi Watanzania kama wamenielewa vibaya,” alisema Chenge.

Chenge aliomba msamaha huo jana jioni jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga semina ya mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA) katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski.

Chenge alisema kutokana na kuathiriwa na kabila lake la usukuma, alijikuta akitoa kauli hiyo, akiamini kuwa alikuwa hajakosea na akasema kama kuna Watanzania wameudhika na kauli hiyo, anawaomba radhi.

Chenge pia alisema hana kinyongo na wala hana nia ya kuvishitaki vyombo vya habari vilivyoandika habari hizo kama inayoandikwa na baadhi ya watu.

“Sina ugomvi na vyombo vya habari na wala sina nia ya kuwashitaki watu walioandika habari hizo kwa kuwa naamini walikuwa wakitekeleza majukumu yake,” alisema.

Alikuwa akizungumza hayo kutokana na kauli aliyoitoa Jumatano wiki mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akitokea China alikokuwa ameongozana na Rais Jakaya Kikwete katika ziara yake ya siku sita.

Chenge alikaririwa na vyombo vya habari akikiri kuchunguzwa na taasisi moja ya upelelezi ya Uingereza ya Serious Fraud Office (SFO) kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kampuni ya BAE Systems ya Uingereza ili kufanikisha ununuzi wa rada ya serikali mwaka 2002.

Mbali na kugoma kujiuzulu kutoka katika nafasi yake, Chenge pia aligoma kutoa maelezo juu ya namna alivyopata fedha hizo, akisema kwanza anasubiri uchunguzi dhidi yake ukamilike ndipo atatoa maelezo ya namna alivyopata fedha hizo.

Gazeti la The Guardian la Uingereza liliandika Aprili 12, mwaka huu kwamba jumla ya pauni za Kiingereza 507,500, ambazo ni sawa na zaidi ya Sh bilioni moja zilikutwa kwenye akaunti ya benki moja iliyopo katika kisiwa cha Jersey nchini Uingereza.

Gazeti hilo lilisema akaunti hiyo ilikuwa ikichunguzwa ili kupata uhakika wa wapi fedha hizo zilitoka na kwamba iwapo ingegundulika kuwa zilitoka BAE Systems, angechukuliwa kuwa mmoja wa mashahidi dhidi ya maafisa wa kampuni hiyo wanaotuhumiwa kutumia rushwa kushawishi ununuzi wa rada hiyo.

Baada ya habari hizo, viongozi kadhaa wamejitokeza kumtaka ajiuzulu uwaziri ili kupisha uchunguzi huo unaoendeshwa na SFO.

Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba aliyemtaka Rais Kikwete amwajibishe kwa kumwondoa katika Baraza la Mawaziri.



No comments: