Tuesday, April 01, 2008


Hatima ya Mwafaka sasa

kwa wananchi



Mwandishi Wetu, Musoma

Daily News; Tuesday,April 01, 2008 @00:01

KIKAO cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeamua kuirudisha ajenda ya suala la Mwafaka kati ya chama hicho na Chama cha Wananchi (CUF), kwa wananchi wa Zanzibar ili watoe maoni yao.

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa alisema juzi usiku kuwa chama hicho kinaamini kupeleka suala hilo kwa wananchi ndiyo njia pekee na sahihi ya kufikia Mwafaka unaokubalika kwa wananchi wote.

Uamuzi huo wa NEC utachelewesha upatikanaji wa ufumbuzi wa kudumu juu ya mpasuko wa kisiasa visiwani humo. Mazungumzo ya kutafuta Mwafaka huo yamedumu kwa miaka miwili baada ya kuanza Januari 17, mwaka juzi.

Nacho CUF kimesema kutokana na uamuzi huo wa CCM, kitatoa tamko rasmi leo. Makubaliano ya kuundwa kwa Serikali ya Mseto yaliwekwa wazi na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharrif Hamad ambaye aliwahutubia wanachama wa chama chake na kusema kuwa wamekubaliana kuundwa kwa Serikali ya Kitaifa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Baada ya kauli hiyo, Katibu Mkuu wa CCM Yussuf Makamba aliahidi kutoa tamko baada ya kikao hicho cha NEC ambacho kimefanyika katika Kijiji cha Butiama ambako ni nyumbani kwa Baba wa Taifa na mwasisi wa chama hicho, Mwalimu Nyerere.

Lakini taarifa iliyotolewa juzi usiku baada ya kumalizika kwa vikao vya NEC, na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, ilisema chama hicho kimeamua kupeleka rasimu hiyo ya makubaliano kwa wananchi ili watoe maoni yao kama wanakubaliana nayo au la.

Msekwa alisema NEC imefikia uamuzi huo baada ya kusoma mapendekezo yaliyoko rasimu juu ya muundo wa serikali mpya ya Zanzibar utakavyokuwa kutokana na rasimu hiyo ya Mwafaka.

“Kama mapendekezo yaliyoko kwenye Mwafaka yatakubaliwa ni wazi kuwa kutakuwa na mabadiliko katika Serikali ya Zanzibar hivyo tumeona njia pekee na sahihi ni kurudi kwa wananchi wa kisiwa hicho kupata maoni yao kabla ya utekelezaji wa makubaliano hayo,” alisema Msekwa.

Katika kikao hicho cha siku mbili, NEC ambayo imeielekeza timu ya majadiliano ya chama hicho kukutana na CUF ili kupitia rasimu hiyo tena kabla ya umma wa wananchi kutoa maoni yake.

Hatua ya CUF kuchukulia rasimu hiyo kama ajenda imetafsiriwa na wachambuzi wa mambo kuwa ilikuwa njia sahihi kwa Seif kurejesha umaarufu wake ambao ulishaanza kupotea.

Msekwa akielezea hali hiyo alisema CCM inalaani hatua ya CUF kutangaza rasimu hiyo ya Mwafaka kabla ya vyama vyote kufikia makubaliano ya pamoja. Alisema chama chake kimesikitishwa na uamuzi huo wa CUF ambao alisema unaweka mazingira magumu ya kuaminiana baina ya vyama hivyo.

Wakati huo huo, NEC imeagiza serikali zitunge sheria ya kutenganisha uongozi na biashara kwa viongozi waliomo ndani ya vyombo vya dola. Kikao hicho kilitamka kuwa kuchanganya uongozi na biashara kimekua chanzo cha migongano ya maslahi na ukiukwaji wa maadili na miiko ya uongozi.

Kwa upande wa maadili, chama hicho kimesisitiza viongozi wake wasiwe sehemu ya maovu kwani kufanya hivyo kunajenga chuki kwa chama na serikali zake. Pia kimewaagiza wabunge wake washiriki kwa ukamilifu katika kuhakikisha Bunge kinakuwa chombo cha kusimamia serikali katika utendaji wake.

NEC pia imebaini kuporomoka kwa nidhamu na maadili ya chama hivyo imeagiza hatua zianze kuchukuliwa zenye lengo la kurudisha nidhamu na mshikamano katika kuendesha shughuli za chama. Hatua hizo ni kuvunja makambi ndani ya chama, kutokomeza vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa chama dola na uchujaji makini wa wagombea wakati wa uchaguzi.


No comments: