
Kashfa ya Mkapa,
Yona yatikisa Bunge
* Mbunge CCM adai wamejiuzia mgodi wa bil.4/- kwa mil.70/-
* TANESCO inawalipa shilingi milioni 146 kila siku
* Ajipanga kuibua upya hoja ya kuuzwa nyumba za serikali
Na Joseph Lugendo, Dodoma
* TANESCO inawalipa shilingi milioni 146 kila siku
* Ajipanga kuibua upya hoja ya kuuzwa nyumba za serikali
Na Joseph Lugendo, Dodoma
UPEPO mbaya wa kashfa za ufisadi unazidi kumwandama Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamini Mkapa baada ya Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Bw. Aloyce Kimaro (CCM) kumshambulia bungeni rais huyo na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Daniel Yona akidai walijuzia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira wenye thamani ya sh. bilioni 4 kwa sh. milioni 70.
Mbunge huyo alitoa kauli yake juzi usiku wakati akichangia hoja kuhusu Muswada wa Sheria ya Umeme wa 2008 na kuongeza kuwa kama jambo hilo lilikuwa sahihi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Adam Malima naye aunde kampuni ya kuchukua gesi ya Mkuranga.
"Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachina waliwekeza sh. bilioni 4 pale Kiwira lakini mwaka 2004 Yona ( Bw. Daniel ) na Rais Mstaafu wakaanzisha Kampuni ya Tan Power Resource," alisema Mbunge huyo ambaye pia anajiandaa kuwasilisha hoja binafsi bungeni wiki hii juu ya uuzwaji wa nyumba za serikali.
"Viongozi hawa waliamua kujiuzia mgodi wa Kiwira bila kutangaza tenda na kinyume na utaratibu kwa sh. milioni 700, na wakalipa malipo ya awali ya sh. milioni 70 tu," alisema Bw. Kimaro.
Bw. Kimaro alisema baada ya kujiuzia mgodi huo na kutoa kiasi hicho cha fedha, waliingia mkataba na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kinyume cha utaratibu na sasa wanalipwa mamilioni kila siku.
"Mwaka 2006 bila utaratibu, wakaingia mkataba na TANESCO na sasa
wanalipwa sh. milioni 146 kila siku," alisema Bw. Kimaro na kuongeza kuwa
malipo hayo yanaongeza mzigo kwa wananchi kwa kulipa bei ya juu ya umeme na kuhoji kama kitendo hicho ni cha uadilifu.
"Huku si kukiuka maadili ya uongozi. Hawa vijana tunawaonesha maadili gani ya kuiga? Kama ni hivyo kule Mkuranga nako, Malima aunde kampuni achukewe gesi," alisema Bw. Kimaro huku akishangiliwa na wabunge.
Aliwataka wabunge wenzake wasikubaliane na mambo kama hayo ili kutimiza ahadi waliyotoa wakati wa kampeni za uchaguzi ya 'Maisha bora kwa kila Mtanzania' na kumtaka Rais Jakaya Kikwete akumbuke hauli yake kwamba urais wake hauna ubia na mtu.
"Tufike mahali tuseme inatosha, Rais Kikwete alisema hana ubia na mtu kwenye urais wake sasa inakuwaje hawa watu wanaomvuta koti asiweze kutekeleza ahadi ya Maisha bora kwa kila Mtanzania ?" Alihoji Bw. Kimaro.
"Sasa na yeye aseme basi, watu hawa waendelee kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria na ukifika wakati wa bajeti waziri atuletee jibu, akikosa asilete bajeti yake," alisema Bw. Kimaro.
Alipendekeza kifungu cha 31 cha muswada huo kinachozuia kampuni zenye mikataba na TANESCO kuingia katika biashara ya kuuza umeme kwa miaka mitano ijayo, kiongezewe kipengele au kiundiwe kanuni ambayo itazuia wamiliki wa kampuni husika kubadilisha umiliki wao kwa kuwapa watoto wao ili waweze kuuza umeme kabla ya muda huo.
Vilevile alitahadharisha kuwepo kwa watu ambao katika mapambano ya kuinua uchumi wa nchi wamejiweka tayari kukimbia nchi ikiwa hali haitakuwa nzuri.
"Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu katika vita hii ya uchumi wanapiga
kelele lakini mguu mmoja ndani mwingine Uingereza au Kanada, hawa lazima tuwaache Tanzania wapike chakula na kusafisha mestini (chombo cha kulia chakula jeshini)," alisema Bw. Kimaro.
Wimbi la ufisadi linazidi kupamba moto huku baadhi ya wananchi na wanasiasa wa upinzani wakiwaelekezea kidole viongozi na wanasiasa kwa kujiuhusisha na jambo hilo.
Juzi viongozi wa kambi ya upinzani walianza mchakato wa kutaka kuhakiki mali za vigogo mbalimbali, katika Ofisi ya Tume ya Maadili ili kujua utajiri walio nao waliupata kihalali au la.
Hivi karibuni aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Miundombinu Bw. Andrew Chenge alilazimika kujiuzulu kutokana na kashfa ya kudaiwa kumiliki mamilioni ya fedha nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment