Monday, April 07, 2008


Kikwete aiwakilisha Afrika barani Asia, Ulaya

RAIS JAKAYA Kikwete aliondoka nchini jana, kwenda India kuwakilisha bara la Afrika katika mikutano itakayofanyika Asia na Ulaya.

Taarifa ya Ikulu ilisema jana kuwa ziara itamfikisha Kikwete katika nchi nne zikiwamo mbili za Asia na nyingine mbili za Ulaya.

Katika hatua ya kwanza ya ziara hiyo, taarifa hiyo ilieleza kuwa Kikwete akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), ataliwakilisha bara hilo katika mkutano wa kwanza kati ya wakuu wa nchi hizo na India.

Mkutano huo wa siku mbili utafanyika New Delhi, India kuanzia kesho. Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine wa Afrika watakaoshiriki katika mkutano huo ni mwenyekiti wa AU aliyemaliza muda wake, Rais John Kuffour wa Ghana na Mwenyekiti wa Umoja wa New Partnership for Africaճ Development (NEPAD), Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi na viongozi wa nchi waanzilishi wa NEPAD.

Viongozi hao ni Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria, Umaru Yar´dua wa Nigeria, Abdoulaye Wade wa Senegal, Thabo Mbeki wa Afrika Kusini na Hosni Mubarak wa Misri. Viongozi wengine watakaohudhuria mkutano huo ni wawakilishi wa jumuiya nane za uchumi za bara la Afrika zinazotambuliwa na AU.

Jumuia hizo ni Umoja wa Uchumi wa Nchi za Kiarabu za Maghreb, Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Sahel-Sahara na ile ya Uchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas).

Nyingine ni Jumuia ya Uchumi ya Nchi za Afrika ya Kati, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) na Jumuiya ya Inter-Governmental Authority and Development (IGAD).

Akitokea India, taarifa hiyo ilieleza kuwa Rais Kikwete atakwenda China kwa ziara ya kiserikali ya siku nne kwa mwaliko wa Rais Hu Jintao.

Rais Kikwete atawasili China Aprili 11, hiyo ikiwa ni ziara yake ya kwanza ya kiserikali nchini humo tangu aanze muhula wake wa uongozi, Desemba 21, 2005. Hata hivyo, Rais Kikwete alipata kufanya ziara ya kikazi nchini China ambako alihudhuria mkutano wa wakuu wa nchi wa Ushirikiano wa China na Afrika uliofanyika Novemba 2006.

Wakati wa ziara yake China, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Hu Jintao mjini Sanya, jimbo la Hainan. Pia, atakutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao.

Baada ya ziara ya China, Rais Kikwete atakwenda Copenhagen, Denmark kwa siku mbili ambako atashiriki mkutano wa kwanza wa Tume ya Kuendeleza Ushirikiano na Afrika ambao ameombwa na kukubali kuwa mjumbe wake.

Tume hiyo iliyoundwa na Waziri Mkuu wa Denmark, Anders Fogh Rasmussen, itaelekeza nguvu zake katika kutatua matatizo ya Afrika katika maeneo ya vijana na ajira. Tume hiyo itafanya mikutano mitatu kabla ya kutoa ripoti na mapendekezo yake.

Akitokea Denmark Aprili 16 , Kikwete atakwenda London, Uingereza, ambako anatarajiwa kuzindua Mtandao wa Watanzania waishio Uingereza (Tanzania Diaspora).


No comments: