Wednesday, April 30, 2008

TAKUKURU

Hamnazo?

Wanafanya mzaha wa hali ya juu!

Alichofanya huyo jamaa si haki. Jamaa keshashtakiwa anasubiri kwenda mahakamani kujibu mashtaka ya rushwa ya ngono.

Vingunge wa serikali walioiba Benki Kuu, Richmond, madini, na mabilioni sekta zingine, wapo mitaani wanadunda!!! Pamoja na ushahidi wa kutosha na unaojulikana (mfano Taarifa ya Tume ya Bunge ya Richmond) na kila mtu anajua, eti bado uchunguzi unafanyika!!! Hivi ndoano na nyavu za TAKUKURU ni za kukamatia dagaa vibua tu? Hawana ndoano na nyavu za kuvulia manyangumi na mapapa?

Hivi hii ni haki kweli?

TAKUKURU mmeshindwa na majukumuu yenu?

Kama mmeshindwa,

basi fanyeni kama walivyosema wahenga:

”Enda na uchao, sende na uchwao”

Bofya hapa: Mafisadi yaliyokubuhu

Imetumwa na

Jamaldeen Tacuma Bin Mazar E. Shariff Ibn Zenjibari

tacumajamaldeen@yahoo.co.uk




Kigogo wa Usalama katika Shule za St. Mary's jijini Dar es Salaam, Justus Joseph Mrefu, mapema wiki hii alinaswa na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) akifanya jaribio la kula rushwa ya ngono kwa binti (jina tunalihifadhi) kama kichocheo cha kumpatia ajira...

Tukio hilo la aina yale lilitokea katika nyumba ya kulala wageni inayojulikana kwa jina la Business iliyopo Tabata Bima jijini Dar es Salaam baada ya mtego uliowashirikisha waandishi wetu, binti husika pamoja na maafisa wa TAKUKURU.

Kwa mujibu wa binti huyo aliyefanikisha zoezi hilo, wiki chache zilizopita alifika katika Ofisi za Shule ya St. Mary's Tabata jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutafuta kazi ya kulea watoto yatima, lakini kigogo huyo alidai rushwa ya ngono ili ampatie ajira ya ulinzi ambayo alidai iko ndani ya uwezo wake.

“Mimi nilikwenda St. Mary kusaka ajira ya kuwalea watoto yatima, lakini nilipoongea na mlinzi getini alinitaka nikaongee na bosi wake, Justus Joseph Mrefu suala langu ambapo aliniambia kama kweli nataka kazi basi atanipa ya ulinzi kama nitakubali kufanya naye mapenzi.

“Nilifedheheshwa sana na maneno yake hivyo nikakubali kinafiki kisha tukapeana namba za simu, lakini nilipotoka hapo niliwasiliana na waandishi wa habari kwa lengo la kumfunza adabu mzee huyo,” alisema dada huyo.

Waandishi wetu walipopewa taarifa hizo walifanya mawasiliano na Maafisa wa Takukuru na kupanga mtego kabambe kwa kushirikiana na binti aliyeombwa rushwa hiyo.

Wanahabari wetu kwa kushirikiana na Maafisa wa TAKUKURU waliungana na binti huyo ambaye walimtaka awasiliane na Mrefu kuwa wakutane jioni ya Jumatatu wiki hii katika Gesti ya Business ili akamilishe sharti la kumpa mapenzi ili apate ajira.

Baada ya mawasiliano hayo, Mrefu alifika katika gesti waliyokubaliana na kuchukua chumba kilichokuwa kimeandikwa Tembo tayari kwa kwenda kupumzika na kimwana huyo.

Wakiwa chumbani, binti aliwasiliana na waandishi pamoja na Maafisa wa TAKUKURU mara baada ya jamaa kuvua nguo zake zote tayari kwa kuanza ‘shughuli’ ambapo chumba hicho kilivamiwa na kumkuta Mrefu kama anavyoonekana pichani.

Kufuatia tukio hilo, Mrefu alifikishwa katika Kituo cha Polisi Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salam ambapo habari za uhakika kutoka kituoni hapo zinadai kuwa, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mapema iwezekanavyo akikabiliwa na shtaka la kuomba rushwa ya ngono.




No comments: