Mkapa, waziri wake waanikwa
WAJIUZIA MGODI WA BILIONI 4/- KWA MILIONI 700/- TU
NYARAKA mpya zilizopatikana hivi karibuni zinaonyesha kwamba rais mstaafu Benjamin Mkapa na waziri wake wa nishati na umeme Daniel Yona, waliuza kampuni ya umma ya Kiwira Coal Mines Limited kwa kampuni yao binafsi kwa milioni 700/- tu mwaka 2005 wakati thamani halisi yam god huo ilikuw abilioni 4/-Kwa mujibu wa rekodi sahihi za serikali ambazo gazeti hili limefanikiwa kuziona, mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira uliojengwa na serikali katika miaka ya 1980 kwa fedha kutoka serikali za China na Tanzania uligharimu kiasi cha bilioni 4.29/-, Upembuzi uliofanywa na mwnajiolojia wa Kichina mwishoni mwa miaka ya 1970 ulionyesha kwamba mgodi huo ulikuwa na hazina ya makaa ya tani milioni 35.14, na hazina iliyothibitishwa ya tani milioni 22.14.
Katika ubinafsishaji wenye utata wa mgodi huo wa makaa ya mawe, ambao ulifanikiwa kwa usiri mkubwa, serikali iliuza hisa kwa kampuni ya Tanpower Resources Company Limited, kampuni binafsi iliyoanzishwa na Mkapa, Yona na ndugu zao w karibu.
Wakitumia nyadhifa zao ndani ya serikali wakati huo, Mkapa na Yona waliharakisha ubinafsishaji wa mgodi huo na kuhakikisha kwamba ulitakiwa kuuzwa kwa bei ya kutupa kwenye kampuni yao binafsi, vyanzo mbalimbali vimeeleza.
Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) Ilisaini makubaliano na kampuni ya Tanpower Resources mnamo juni 8, 2005, ya kuuza asilimia 70 ya hisa za mgodi huo wa makaa ya mawe kwa kampuni hiyo ya Mkapa na Yona.
Lakini, Tanpower Resources haraka iliongeza umiliki wake hadi kufikia asilimia 85 na mnamo Machi 2006 ikaingia katika mkataba wenye utata wa dola za Marekani milioni $271.8 (takriban bilioni 340/-) na shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) kwa ajili ya kuzalisha megawati 200 za umeme ambazo ungeingizwa kwenye gridi ya taifa.
Asilimia 15 zilizobaki za umiliki wa mgodi wa Kiwira ndizo pekee mpaka sasa zinazomilikiwa na serikali Nyaraka za serikali zinaonyesha kwamba serikali iliuza mgodi huo kwa bei ya kutupa kwa tanpower Resources kwa kiasi cha milioni 700/-, huku kampuni hiyo ikipewa muda mrefu wa malipo.
Imebainika kwamba kampuni hiyo ilitakiwa kulipa milioni 70/- siku ya kusaini makubaliabo hayo, huku kiasi kilichosalia ambacho ni milioni 630/- kikitakiwa kulipwa ndani ya miezi sita tangu kusainiwa kwa makubaliabo hayo.
Mkataba wa ubinafsishaji wa mgodi huo wa makaa ya mawe ulisainiwa kwa niaba ya serikali na Mwenyekiti wa PSRC, John Rubambe, na mwanasheria wake mkuu, M. Mahanyu.
Kwa upande mwingine, meneja mkuu wa zamani wa mgodi huo, Adam Salim Abdu, na meneja wa fedha na utumishi, Ramadhan Idabu, walisaini makubaliano hayo kwa niaba ya Kiwira Coal Mines Ltd.
Walioiwakilisha Tanpower Resources kwenye utiaji saini huo wa mkataba wenye utata walikuwa Evans Mapundi na Wilfred Malekia.
Mapundi na Malekia wanamiliki hisa ndani y a Kiwira kupitia kampuni yao ya Universal Technologies Limited, ambayo pia ipo chini ya mwamvuli wa Tanpower Resources. Mapundi na Malekia pia wako kwenye bodi ya wakurugenzi ya Kiwira yenye wajumbe sita.
Uchunguzi uliofanywa kwa kuongozwa na nyaraka mbalimbali kutoka wakala wa usajili wa kampuni na liseni (Brela) umeonyesha kwamba Tanpower Resources ulikuwa ni mkakati na mpango wa pamoja baina ya mkapa na Yona, ulioanzishwa mwishoni mwa kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya tatu wakati Mkapa alipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania na Yona akiwa waziri wa nishati na madini.
Wakati kampuni hiyo ikisajiliwa mwaka 2004. wakurugenzi wake wa kwanza walikuwa ni mke wa rais wa wakati ule, Anna Mkapa; waziri wa nishati na madini wa wakati huo Daniel Yona; Nicholas Mkapa (mtoto wa Mkapa); Joseph Mbuana (baba mkwe wa Nichola Mkapa); na Evans Mapundi.
Kama ilivyowahi kuripotiwa na KULIKONI na gazeti dada la THISDAY, Yona, ambaye aliongoza wizara ya nishati na madini katika serikali ya awamu ya tatu chini ya Mkapa, na mwanawe, Danny Yona, walikuwa wanahisa wakubwa wa baada ya kampuni ya Kiwira kubadili jina na kuitwa Kiwira Coal and power Limited chini ya mwavuli wa Tanpower Resources Company Limited.
Wao wanawakilishwa na kampuni ambayo haifahamiki sana, lakini yanye nguvu ya Tanpower Resources kupitia kampuni yao binafsi ya DEVCONSULT LIMITED, mbayo Yona (waziri wa zamani) mkubwa anamiliki hisa asilimia 90 na Yona mdogo anamiliki asilimia 10 zilizosalia.
Uchunguzi wa gazeti hili tayari ilishaeleza kwamba mkapa na mkewe, Anna Mkapa, wana hisa kwenye kampuni ya Kiwira kupitia kampuni yao binafsi ya Anbem Limited, ambayo ilisajiliwa mwaka 1999 huku wanahisa hao wakiwa wanaisa wakuu wakati wakingali Ikulu.
Mbali ya hisa zinazomilikiwa na Anbem Limited, imeelezwa pia kwamba mtoto wa Mkapa, Nicholas Mkapa pia ana hisa zake kwenye kampuni ya Kiwira kupitia kampuni ya Fosnik Enterprises Limited ambayo anamiliki yeye na mkewe, Foster Mbuna kwa asilimia 50-50.
Wakati huo huo, baba mkwe wa Nicholas Mkapa, Joseph Mbuna, pia ni mwanahisa wa Kiwira Coal and Power Limited mgodi ambao uko mkoani Mbeya
Mbuna, ambaye hisa zake katika kapuni hiyo zinapitia kampuni yake ya Choice Industries Limited ambayo yeye ndiye mmiliki mkuu, kwa sasa ndiye mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Kiwira
Coal and Power Limited, ambapo Nicholas Mkapa ni mmoja wa wakurugenzi.
Kama ilivyo kwa kampuni za Anbem Limited, DEVCONSULT Limited na Fosnik Enterprises Limited, Choice Industries Limited pia ipo chini ya mwanamvuli wa Tanpower Resources.
Ilifahamika baadaye kwamba Kiwira Coal and Power Limited ilipewa kwa mizengwe nyongeza ya eneo lenye hazina kubwa ya makaa ya mawe ambalo awali lilikuwa likimilikiwa na serikali.
Vyanzo vya ndani zinaeleza kwamba eneo la Kabulo linalodhaniwa kuwa na makaa ya mawe ambalo pia lipo mkoani Mbeya ulipo mgodi wa kiwira lilitwaliwa kutoka shirika la Madini la Taifa (Stamico), linalomilikiwa na serikali, na kukabidhiwa kwa wamiliki wa Kiwira.
Tafiti zilizowahi kufanywa kwa mwongozo wa serikali yenyewe zinaonyesha kwamba eneo la Kabulo, ambalo lipo katika mkondo wa bonde la Ufa la Afrika Mashariki, kusini magharibi mwa Tanzania, limethibitika kuwa na hazina ya tani milioni 14 za makaa ya mawe.
(Imetolewa na Kulikoni, issue no 294, Jumatano April, 2, 2008)
1 comment:
Tafadhali nisaidieni
Hivi huyu Nicholas Mkapa ni yule yule Nicholas Merinyo au watu tofauti? Ni kwa sababu magazeti yanatumia majina yote haya kama mtoto wa Mkapa mwenye hisa katika Kiwira. Asante
Post a Comment