Monday, April 21, 2008



Mkataba wa Rites

umeiumbua Serikali



na Abdulwakil S. Saiboko

NCHI zilizoendelea duniani kote zina mambo kadhaa ambayo kwayo zinajivunia, ni mjumuisho wa mambo mengi sana katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Ndio kusema, wanapozungumzia demokrasia wanahakikisha inatekelezwa kwa kiwango cha juu kabisa na wanapozungumzia huduma za jamii wanajitahidi kuhakikisha zinapatikana katika viwango ambavyo vinaridhisha kabisa.

Sifa hizo kwa nchi zinazoendelea zinakuwa kinyume, hasa zikichangiwa na kuwapo hali mbaya ya kiuchumi, ukame, vita na majanga mengine mengi. Wapo wanaodai kwamba bado sisi katika baadhi ya sekta tupo nyuma kuliko walikokuwa Waingereza miaka ya 1700. Hii yawezekana ni kweli kwa kuwa vielelezo vipo. Lakini pia inakatisha tamaa kwani ikiwa hivyo ndivyo, basi kuna kila dalili kwamba sisi pengine tusifike kabisa kwenye hatua ya kuitwa nchi iliyoendelea milele.

Tunapoitupia ukope nchi yetu kwa mfano tunaona kuna upungufu mwngi wa kiutendaji ambao tayari Serikali imeanza kuushughulikia, lakini bado kasi iliyopo ni ndogo na ukweli ni kwamba matatizo haya ya kiutendaji haswa kwenye utumishi wa umma yanaipeleka pabaya nchi na mustakbali wa wananchi kwa ujumla.

Suala ambalo hivi karibuni limekuwa likifukuta ni mikataba mibovu ambayo viongozi wetu Mawaziri wa wanaisaini bila kuzingatia maslahi ya mikataba husika kwa wananchi na Serikali kwa ujumla. Mikataba kama Richmond, IPTL na mingineyo mingi imeshalalamikiwa vya kutosha.

Wakati tunazungumzia suala la Richmond, limeibuka jengine la Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ambalo zamani likijulikana kama TRC, imeripotiwa na vyombo kadhaa vya habari nchini kwamba mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Rites ya India wa kukodisha injini 25 za treni ni kitanzi kingine kwa Serikali ya Tanzania. Mgogoro kwenye mkataba huo nao unazungumziwa kuwa unatokana na masharti magumu yaliyomo kwenye mkataba husika, ambayo kwa kiasi kikubwa yanaibana Serikali.

Mkataba huo unaitaka Serikali kulipia gharama zote za matengenezo iwapo injini hizo zitaharibika zikiwa kazini, na zinajumuisha za kusafirisha injini hizo hadi India kwa matengenezo kama itabidi kufanya hivyo kwa kushindwa kuzitengenezea hapa Tanzania.

“Mkataba huo umekadiria gharama za kusafirisha injini moja ya treni kutoka Tanzania hadi India kuwa ni dola 35,000 za Marekani sawa na Sh milioni 41 na gharama za kusafirisha injini zote 25 kwenda India ni dola 1,435,000 za Marekani sawa na Sh 1,025,000,000,” ilisema moja ya habari juu ya mkataba huo.

Hiki ni kiwango kikubwa, hasa ikizingatiwa kwamba mkodishaji ambaye hapa ni Serikali atalazimika kusafirisha injini zote 25 kurudisha India mara baada ya mkataba kuisha. Hizi ni gharama ambazo hazikuwa na msingi wowote wa kuwapo kwa kuwa ni suala la kujiongezea matatizo kwenye Taifa kama hili ambalo tayari linamatatizo lukuki ya kutatua.

Hata hivyo kinachoshangaza zaidi ni kwamba mkataba huu wa TRL unailazimu Serikali kugharamia vitu vingi kwa masharti kwamba Rites ndio watakuwa wasambazaji pekee wa vipuri hivyo. Hiki ni kitendawili kingine cha mikataba mibovu ambayo kwa karne hizi haipaswi kuwapo, suala zima la kufaidika kwa pande mbili “win-win situation” hapa halifikiwi.

Suala linaloshangaza zaidi ni kwamba baadhi ya wafanyakazi wa TRL waliohojiwa wamethibitisha kabisa kwamba injini hizo za kukodi zina uwezo mdogo wa kufanya kazi kiasi ambacho kinaiweka sekta hiyo kwenye matatizo ya kukwama kwa treni mara kwa mara. Hii ni ishara tosha kwamba kuna ukosefu wa umakini kwa kuwa kinachohitajika ni kupiga hatua mbele na suala la kukodi injini zenye uwezo mdogo kuliko zilizokuwapo awali linalengo la kuturudisha nyuma kimaendeleo.

Wenzetu kwenye nchi zilizoendelea wanajitahidi kuhakikisha wanafanya mambo makubwa zaidi ya pale walipo sasa ili wajipatie uhakika wa ushindani kwenye nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii, wakati huo sisi ndio kwanza tunaingia mikataba isiyo na tija. Mambo kama haya yanasababisha tunyoosheane vidole kila uchao, japo tunaambiwa kwenye vitabu vya dini kwamba kabla hujasimama kusema aibu za mwenzako, utazame za kwako kwanza, lakini kwenye hili hatuna budi kuzitizama na kuzinyoshea aibu kama hizi vidole kwa kuwa zinakusudia kuliangamiza taifa.

Wapo wanaodai kwamba ni kweli mkataba huo una upungufu wake lakini huwezi kuibana Serikali kwa kuwa ulisimamiwa na maofisa wa Serikali mpaka mwisho, hoja hii ingekuwa na msingi hapa kama tungekuwa na viongozi waaminifu na wenye uzalendo kwa nchi yao.

Tunaposema hivi ni sawa na kufumba macho wakati wa kutia saini mikataba, bila kujali kwamba wananchi wanateseka.

Alipoteuliwa tena kuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge alipata upinzani kutoka kwenye vyombo vya habari kadhaa nchini na kwa wananchi kwa ujumla wakidai kwamba hakustahiki kurejeshwa kwenye Baraza la Mawaziri, tena kwenye wizara nyeti kama hiyo ya Miundombinu. Ni wizara ngumu na yenye mikataba mingi, lakini tayari watu walianza kugusia utata wa mkataba wa Rites. Wakubwa waliamua kufunga macho wakautia saini na kuendelea nao tu licha ya kuelewa kwamba hauna maslahi kwa nchi.

Tumekosa kabisa wivu wa maendeleo na tunashindwa kuendelea kwa sababu hiyo, kwa mfano wakati wenzetu wanajenga barabara za kupita juu na chini ya aridhi, sisi mpaka leo tumeshindwa hata kujenga daraja la kuiunganisha Kiganboni na Sehemu nyingine za Jiji la Dar es salaam, tumeshindwa hata kuboresha usafiri wa pale kivukoni matokeo yake tunacheza kamari na maisha ya watu.

Kuna kipindi kulitolewa kauli kwamba malori yote yaliyojengewa bodi za mabasi yangesimamishwa mara moja kwa kuwa ni hatari kwa usalama wa raia. Lakini wakati huo huo Serikali inamiliki treni ambazo humo ndani ukiingia ni kama mahabusu na injini zake ndizo hizo zina utata, na hapo tumeingia mkataba na kampuni ya kigeni ili kuboresha huduma, sasa utajiuliza hapa nani anaweza kumsimamia mwenzake wakati sekta binafsi na Serikali wote ni hawajiwezi? Mikataba yote ipitiwe na ikibidi ifumuliwe.

abduwakils@indiatimes.com
0755656517



No comments: