Siri mpya mamilioni ya
Chenge ughaibuni
*Si visenti vyake tu, kuna mabilioni zaidi
*Wapinzani waapa kulikagua faili lake kesho
*Jimboni kwake moto,aitwe akajieleze
Na Hassan Abbas
KASHFA ya kumiliki akaunti yenye mamilioni ya fedha ughaibuni inayomuandama Waziri wa Miundimbinu, Mwanasheria Andrew Chenge imeingia katika hatua nyingine baada ya siri kadhaa kunaswa na gazeti hili kuhusu visiwa vya Jersey, Uingereza iliko akaunti yake hiyo.
Kufuatia waandishi David Leigh na Rob Evans wa gazeti la Guardian la Uingereza kuibua siri juu ya Chenge kuwa na akaunti hiyo yenye mamilioni kwenye visiwa hivyo, Majira Jumapili sasa limebaini kuwa kuwa visiwa hivyo vinasifika kwa wanasiasa kuweka 'fedha chafu.'
Hali hiyo imeifanya ripoti moja ya kimataifa ya Serikali ya Marekani kuvitaja visiwa hivyo kuwa ni 'kitovu cha fedha chafu za wanasiasa.'
Kwa mujibu wa ripoti iitwayo International Narcotics Control Strategy Report, iliyotolewa hivi karibuni na Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo, kisiwa cha Jersey ni moja ya maeneo yaliyo rahisi kwa biashara haramu ya fedha na ambako wanasiasa na viongozi wengi wa umma hupata mwanya wa kuweka fedha zao 'haramu.'
Kisiwa hicho kipo katika nchi 20 'nyeusi' zilizoorodheshwa kuwa za hatari katika biashara ya fedha haramu na pia ambako viongozi huona kuna urahisi wa kuhamishia fedha zao huku viongozi wa kisiwa hicho wakifurahia faida wanayoipata kutokana na biashara hiyo ya fedha.
Katika ripoti hiyo kisiwa hicho kimeonekana kwenda 'kula sahani moja,' na nchi zenye rekodi mbaya katika udhibiti wa fedha haramu ambazo ni Guernsey, visiwa vya Man, Afghanistan, visiwa vya Cayman, Saiprasi, Liechtenstein, Pakistani, Uingereza, Ufaransa na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Kwa mujibu wa tovuti ya Serikali ya visiwa hivyo, biashara ya fedha ndicho chanzo kikuu cha mapato ya visiwa vya Jersey lakini suala la namna fedha nyingi hasa kutoka nje zinavyoingizwa visiwani humo, kumeifanya nchi hiyo ijitazame upya kwa kuchukua tahadhari kadhaa ikiwemo kuanzisha idara ya kudhibiti fedha haramu.
Viongozi wa Idara ya Kudhibiti Fedha Haramu visiwani humo wanaangalia nyendo za fedha nyingi zilizoko visiwani humo, wamelithibitishia Majira Jumapili katika taarifa yao.
Wakati visiwa hivyo vikiwa kwenye orodha hiyo nyeusi, pia shaka juu ya uamuzi wa Waziri Chenge kuwekeza fedha nyingi kwenye visiwa hivyo, inazidi kuongezeka baada ya kubainika kashfa nyingine nzito inayowakabili baadhi ya viongozi wa Serikali na watendaji wengine ya kuhusika katika vitendo vya siri vya kuwafanyia ukatili na udhalilishaji watoto ikiwemo ubakaji kwenye jengo walimokuwa wakitunzwa kwenye jumba moja la Serikali.
Zaidi ya malalamiko 150 yamepokewa na kuifanya jamii ya visiwa hivyo kuingia kwenye mjadala mzito kutokana na matukio hayo ya aibu.
"Unakwenda kulala usiku, ukiwa usingizini ghafla unasikia mikono yako inashikwa na kufungwa kwa nyuma na kisha unajikuta ukibakwa," anakumbuka Peter Hannaford, mmoja wa wahanga wa vitendo hivyo.
Kadhia hiyo iliyozidi kuviweka visiwa hivyo katika ramani yenye utata na kutia shaka zaidi inapobainika kiongozi wa umma popote duniani amewekeza huko, jana imeingia katika hatua nyingine baada ya gazeti la Jersey Evening Post la visiwani humo kueleza kuwa sehemu ya uchunguzi huo imesitishwa.
Katika hatua nyingine sasa imebainika kwa nini Waziri Chenge alidiriki kuziita sh. bilioni moja alizoziweka visiwani humo kuwa ni vijisenti, gazeti hili limebaini kuwa kiasi cha fedha kilichowekwa visiwani humo na watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa kutoka nchi kadhaa kinafikia sh. trilioni 500 mpaka kufikia Desemba mwaka jana.
Takwimu zilizopatikana visiwani humo zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2007 pekee kiasi cha sh. trilioni 44 ziliwekwa kwenye akaunti mbalimbali za nchi hiyo hivyo kuifanya bilioni moja ya Chenge, kwa viwango vya 'vigogo' waliowekeza huko kuwa ni 'vijisenti.'
Ripoti kutoka visiwa hivyo zinaonesha kuwa wanasiasa, wafanyabiashara na 'wasanii' wengine wameendelea kuweka sana fedha zao huko wakifaidika na kinga muhimu zinazotolewa na visiwa hivyo ambavyo pia uchunguzi wetu umebaini kuwa vinasheria kali zinazolinda usiri wa wanaowekeza.
Naye mwandishi wetu George Boniphace kutoka Bariadi, Shinyanga ambako ni sehemu ya jimbo la Bw. Chenge (CCM-Bariadi Mashariki), anaripoti kuwa baadhi ya wapigakura jimboni humo, wamesema watatoa hukumu yao mwaka 2010 katika uchaguzi mkuu.
Wakizungumza na gazeti hili wiki hii wananchi hao wameonesha kuumizwa na kauli ya Bw. Chenge kuwa fedha hizo nyingi zlizonazo huko ughaibuni ni 'vijisenti.'
Wamesema hawakutegemea kusikia kauli hiyo kutoka kwa kiongozi huyo anayejua vyema shida za wananchi wake na wanaiona kuwa ni ya kuwadhalilisha wapiga kura hao.
Jana vyombo mbalimbali vya habari vilimnukuu Bw. Chenge akiomba radhi kwa namna ambavyo neno 'vijisenti' lilivyopokelewa na wananchi mbalimbali.
Lakini wananchi waliozungumza na gazeti hili walisisitiza kuwa mbali ya mbunge wao huyo kuomba radhi wananchi bado anapaswa kwenda jimboni humo ili kueleza ukweli wa yale anayohusishwa nayo kuliko kuendelea kujibu kuopitia vyombo vya habari.
"Sisi ndiyo wapiga kura wake katika jimbo la Bariadi Mashariki na mbunge huyo anatuwakilisha sisi pamoja na umma wa watanzania kwa nafasi ya uwaziri hivyo hana budi kufunga safari hadi jimboni mwetu ili apate baraka zetu vinginevyo hata sasa hivi bungeni anajiwakilisha yeye mwenyewe," alisema Bw. Ndaki Mabula wa kijiji cha Igegu, Bariadi Magharibi.
Wananchi hao wamesononeshwa na vitendo vya baadhi ya wanasiasa kuonekana wakihubiri kwa maneno utawala bora huku wao wenyewe wakiwa wa kwanza kufanya matendo tofauti.
Wakati wakizungumzoa kashfa inayomkabili mbunge huyo, wananchi hao pia wamekumbushia kutokamilika kwa miradi mingi hasa ya barabara na ujenzi wa mitaro ya kupitishia maji.
Wamelalamikia kuwa baadhi ya kampuni zilizopewa zabuni ya ujenzi zimeonesha kutokuwa na uwezo na hivyo kuifanya wilaya hiyo kuendelea kuwa na kero mbalimbali.
Wametoa mfano wa tenda ya ujenzi wa kutengeneza barabara kutoka Bariadi hadi Lamadi kwa kiwango cha lami kuwa ni moja ya miradi inayosuasua.
Uchunguzi wa gazeti hili Bariadi mjini hasa kutoka ofisi ya CCM Wilaya hadi ofisi za Halmashauri ya Wilaya, umeonesha kuwa eneo hilo na hata mitaro yake imekuwa ikijengwa kwa kiwango cha chini kiasi kwamba mvua zinazoendelea zimeharibu sehemu iliyojengwa.
Kutoka Dar es Salaam, Reuben Kagaruki anaripoti kuwa viongozi wa vyama vya upinzani kesho wanatarajia 'kuandamana' hadi kwa Katibu wa Tume ya Maadili ya Viongozi kudai fomu za tamko la mali za viongozi wa umma zikiwemo za Bw. Chenge, Rais Mstaafu, Bw. Benjamin Mkapa, aliyekuwa Gavana wa benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Daud Balali na wale wote waliotajwa kwenye orodha ya ufisadi ili kujua mali walizojilimbikizia.
Uamuzi huo ulitangazwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba wakati akihotubia umati mkubwa wa watu walioshiriki maandamano ya chama hicho kupinga kile kinachodaiwa CCM kukataa mapendekezo ya makubaliano ya muafaka.
Alisema sheria inawapa wananchi haki hiyo hivyo viongozi wa vyama vya upinzani watakwenda kudai fomu hizo ili kujiridhisha juu ya mali alizozitaja Bw. Chenge na kujua aliandika akaunti zake zina kiasi gani.
"Tungekuwa na Serikali makini inayowajibika hivi sasa Bw. Chenge angekuwa polisi anapelekewa dona," alisema Profesa Lipumba. Alisema inashangaza kuona Bw. Mkapa naye amekuwa bubu tangu taarifa za ufisadi zilipoanza kuripotiwa.
Kuhusu mazungumzo ya muafaka alisema Rais Kikwete atajisafisha iwapo tu atasaini makubaliano yaliyofikiwa kati ya CCM na CUF, vinginevyo CCM itaonekana inafanya usanii 'kuzidi ule wa mwimbaji wa taarabu katika kikundi la TOT Plus, Bi. Khadija Kopa.'
Alisema alichokifanya Rais Kikwete kinafanana pia na kile kilichofanywa na kiongozi wa kikundi cha LRA cha Uganda , Bw. Joseph Konny, aliyekubalia 'kimsingi' kutilia saini mkataba wa amani na Rais Yoweri Mseven, lakini ilipofika wakati wa kutiliana saini aliingia mitini na kuibuka na madai mapya.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad, alisema kinachotakiwa sasa ni Rais Kikwete kumkutanisha na Rais wa Zanzibar Aman Abed Karume, vinginevyo hakuna kitakachoeleweka.
Naye Gladness Mboma anaripoti kutoka jijini Dar es Salaam kuwa,baadhi ya vikundi vya kijamii hasa vinavyoshughulikia matatizo ya akina mama, vimembana Bw. Chenge na kumtaka kama anaona fedha alizoweka nje ya nchi ni ndogo, azitoe kwa ajili ya kuwasaidia wenye shida.
Kauli hiyo ilitolewa juzi, Dar es Salaam na Bibi Gemma Akilimali ambaye ni mjumbe katika Kikundi cha Kutetea Usawa wa Afya kwa Wote.
Bibi Akilimali alionesha kushangazwa na kauli ya Bw. Chenge ya kuita sh. bilioni moja alizonazo ughaibuni kuwa ni 'vijisenti,' fedha ambazo, anasema zingeweza kusaidia kununulia vifaa, dawa za wajawazito na kufanyia miundo mbinu kwa baadhi ya hospitali nchini.
"Fedha zilizochukuliwa na mafisadi zingeweza kusaidia na kutunza wanawake wajawazito, zikiwemo 'vijisenti' vya Bw. Chenge," alisema.
Akizungumzia Bajeti ya afya anasema kwamba, wanawake wajawazito nchini walitakiwa kupewa huduma yote inayostahili kama malikia kwa sababu ya mzigo mkubwa walioubeba.
"Hospitali nyingi hapa nchini hususani za vijijini hazina vifaa wala dawa za wajawazito, miundombinu yenyewe ni mibovu, lakini bado Serikali inaendelea kutenga bajeti ndogo katika sekta hiyo," alisema Bi. Akilimali.
Aliongeza kuwa tatizo la miundombinu katika hospitali mbalimbali nchini ni kubwa, ambapo alitaka bajeti ya wizara iongezwe kwa asilimia 15 ili iweze kusaidia kutatua matatizo mbalimbali katika sekta ya afya.
Naye Mjumbe wa Kikundi hicho Bi. Festa Andrew alisema fungu ambalo limekuwa likitengwa kwa ajili ya watumishi wa afya limekuwa alipatikani na ndio maana watumishi wengi wanakimbia vituo vyao vya kazi hasa wale wanaopangiwa vijijini.
Kiungo na http://watanzaniaoslo.blogspot.com

No comments:
Post a Comment