Tuesday, April 29, 2008



Tume yagundua

Wahamiaji Somalia

wanavyoingia nchini



Mwandishi Wetu
Daily News; Tuesday, April 29, 2008 @00:06


TUME iliyoundwa na serikali kufanya utafiti kuhusu tatizo la wahamiaji haramu nchini, imebaini kuwa wahamiaji wengi wanaotoka Somalia na Ethiopia huingia kwa msaada wa mtandao wa mawakala wanaofanya kazi hiyo kwa ujira.

Imebaini pia kuwa mpaka wa Tanzania na Kenya katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha una zaidi ya njia 470 za vichochoro zinazotumika kupitishia wahamiaji haramu kutoka eneo la Pembe ya Afrika.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imeikariri Tume hiyo ikisema wahamiaji hao ambao wengi hupita Tanzania wakienda kusini mwa Afrika, huwalipa mawakala hao kuanzia Dola za Marekani 95 hadi 2,000 (takribani Sh 96,000 hadi milioni mbili). Tume hiyo ya utafiti jana iliwasilisha ripoti yake kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha.

Idadi ya wahamiaji haramu wanaokamatwa nchini imekuwa imeongezeka hivyo kuilazimu serikali kufanya utafiti wa kina kukabiliana nayo. Hadi kufikia Machi mwaka huu, wahamiaji haramu 1,279 kutoka Ethiopia na Somalia, walikuwa katika magereza mbalimbali baada ya kukamatwa na kuhukumiwa.

Akizungumza katika kikao hicho cha makabidhiano, Waziri Masha alisema serikali itaipitia ripoti hiyo kwa kina kwa ajili ya kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa ili kukabiliana na tatizo hilo.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuimarisha vituo vya mipakani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuviwezesha kudhibiti wahamiaji haramu wanaopita katika maeneo ya vituo hivyo.

Pendekezo jingine ni kuweka mikakati ya kuwezesha kudhibiti mtandao wa mawakala wanaojihusisha na biashara hiyo ya kuwasafirisha na kuwahifadhi wahamiaji hao haramu.

Wajumbe wa kamati hiyo iliyofanya utafiti walitoka idara mbalimbali za Wizara ya Mambo ya Ndani. Wengine walitoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (ICRC) na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania.



No comments: