
Uingereza sasa yafutilia
vigogo wengine 11 katika
kashafa ya rada
* SFO yachunguza akaunti zao za benki
Na Ramadhan Semtawa
BAADA ya akaunti ya Andrew Chenge, kuchunguzwa kwa tuhuma za kujipatia mabilioni ya shilingi kutokana na ununuzi wa rada ya kijeshi kutoka kampuni ya BAE System ya Uingereza, imebainika kuwa mchakato wa ununuzi wa rada hiyo unagusa vigogo wengine kumi wa serikali iliyopita na iliyopo madarakani
Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili, uchunguzi wa vigogo hao kuhusika kwenye kashfa hiyo unafanywa na Taasisi ya Kuchunguza Makosa makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza, ili kubaini kama nao walipata chochote.
Vyanzo huru vya habari vya Mwananchi kutoka serikalini, katika orodha hiyo ya vigogo ambao akaunti zao zinachunguzwa wamo mawaziri waandamizi katika serikali iliyopita na ya sasa.
Mawaziri hao wanatajwa kuhusika na kashfa hiyo kutokana na nyadhifa zao na uwajibikaji wao wa moja kwa moja au kutokana na nafasi zao kuhusika moja kwa moja na uidhinishaji mkataba na malipo.
Katika orodha hiyo pia wamo naibu waziri mmoja, makatibu wakuu wa wizara, wataalamu na maafisa waandamizi katika wizara iliyokuwa ya Mawasiliano na Uchukuzi na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) kutokana na mamlaka kuhusika moja kwa moja katika suala zima la usimamizi wa usafiri wa anga.
Taarifa hizo zimedokeza kwamba, kabla ya Chenge kuhojiwa, makachero wa SFO walifika nchini na kupata ruhusa ya kumchunguza.
Ununuzi wa rada hiyo kwa kiasi cha Sh70bilioni uliwahi kupigiwa kelele, kwamba utaitia hasara nchi kwa kuwa hizo ni fedha nyingi na kwamba mahitaji halisi ya nchi ingeweza kununua rada ya Sh5bilioni.
Hata hivyo, serikali ya awamu ya tatu ilipuuza malalamiko ya wananchi na kununua rada hiyo kwa madai kuwa ni kwa ajili ya usalama wa anga la nchi.
Sakata la ununuzi wa rada hiyo kwa Tanzania, ni sawa na linalotikisa nchini Saud Arabia ambayo imeuziwa vifaa vya kijeshi, huku Pauni1 bilioni zikidaiwa kuingizwa katika akaunti ya Mwana wa Mfalme Bandari, ambaye hata hivyo amekana kuwa na kiasi hicho cha fedha.
Kwa Tanzania, hadi sasa Chenge anachunguzwa ndiye anayechunguzwa na Taasisi ya Uingereza ya Makosa Makubwa ya Jinai, (Serious Fraud Office) kwa madai ya kujilimbikizia sh 1.2 bilioni katika akaunti yake moja katika kisiwa cha Jersey.
Wakati Chenge mwenyewe akiwa ameweka bayana msimamo wake wa kushirikiana na SFO na kutaka watu wasubiri matokeo ya taarifa ya uchunguzi huo.
Hata hivyo, uchunguzi wa SFO haumanishi kwamba wanaochunguzwa wamekula rushwa ya rada, bali kuangalia fedha zao zilipatikana kwa njia ipi na kama zina uhusiano na ununuzi wa rada hiyo.
SFO inachunguza ili kubaini kama dalali wa ununuzi wa rada hiyo kati ya serikali ya Tanzania na BAE System, Shailesh Vithlani aligawa fedha za kamisheni Sh12 bilioni kwa baadhi ya wanasiasa na maafisa wa Serikali ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment