Saturday, May 10, 2008

AYA ZA AYAH

Virusi ya harusi



Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.


Mpenzi Frank,

Lo, asante sana mpenzi kwa pepe lililoniwasha kama upupu. Yaani wewe … acha tu. Unaponipa maneno kama yale, najisikia kupagawa. Hivi kweli wataka tupange harusi na waniuliza ninaonaje? Mpenziiiii! Unategemea niseme nini? Kwangu mimi hata kesho ingawa najua wahitaji muda kidogo.

Lakini sioni kama tunahitaji muda sana mpenzi. Ya nini kuwa na harusi kubwa? Waache wakubwa wamwage pesa kama radhi. Utadhani mashindano ya fahari. Leo huyu anabuni njia mpya ya kumwaga pesa, kesho mwingine haridhiki hivyo inabidi abuni nyingine zaidi tena. Hivi harusi ndiyo njia pekee ya kumaliza pesa? Au tuseme ni njia bora? Sikatai harusi ni muhimu sana lakini kwa nini harusi ipimwe kwa kiasi cha pesa unazomwaga? Hapo sielewi kabisa.

Tena naona pesa zimeharibu sana mambo ya ndoa. Ninavyojua mimi huko zamani kama ungetaka kunioa mimi lazima uonyeshe kwangu na kwa wazazi wangu kwamba wewe ni mtu! Ndiyo, ujenge nyumba, ufanye kazi, uonyeshe kwamba ni mchapakazi ambaye utanijali na kunipa maisha mema. Tena ilibidi uhamie kwangu tuishi kama mume na mke lakini uko kwenye mtihani. Wazazi wanakupima kama kweli ni mchapakazi au umeficha makucha ya uvivu. Ukishindwa mtihani, hakuna kurudia darasa, ni baiii baiii tu. Unaonaje mpenzi, tukupe mtihani huo? Ingawa najua wewe utafaulu bila wasiwasi wowote.

Najua pia mahari ilikuwepo ndiyo lakini tofauti ya siku hizi. Ilikuwa njia ya kuleta mahusiano baina ya pande zote mbili na wala haikutakiwa kulipwa mara moja. Hata sasa kuna kijana mmoja huko kwetu anayemaliza mahari ya babu yake. Hivyo, mahari haikuwa kitu cha msingi. Cha msingi tabia. Lakini siku hizi … sisemi. Pesa, pesa, pesa. Labda ndiyo maana watu wamegeuka mafisi, maana kipimo cha utu ni pesa tu. Ndiyo maana lazima isakwe kwa kila njia. Hata ukiangalia matangazo ya luninga. Jamaa hakubaliwi na baba wa mpenzi wake hadi alete gari kwa ajili yake. Anapokuja na vizawadi vidogovidogo, nuksi lakini, mbele ya gari, hata angekuwa yule mwuaji wa huko Ulaya aliyemfunga binti yake huko chini, angepokelewa bila hata kuchunguza. Yaani baba hajali kabisa kama yule anamfaa binti yake (ingawa naona kweli binti alimpenda lakini baba anajali mambo mengine kabisa!). Upo hapo mpenzi?

Halafu nacheka sana mambo ya siku hizi na naomba kweli tusiingie kwenye mtego huo. Wazazi pande zote mbili wanashindana nani anaweza kumwaga pesa zaidi. Si unamkumbuka yule mtoto wa dada yake bosi aliyeolewa mwaka jana. Basi keshaachika. Lakini wakati wa harusi, fujo kabisa. Vikao kibao vilifanyika hapa nyumbani kwa bosi na nusu ya mazungumzo ilikuwa jinsi ya kuwapiku wale upande wa Bwana harusi eti ‘tusiaibishwe’. Sijui bosi alilazimika kufisadi pesa kiasi gani ili ‘tusiaibishwe hivyo’! Nguo lazima zitoke Ulaya moja kwa moja. Nadhani hata chakula kiliagizwa spesho na muhuri wa Ulaya ili watu wajue wanakula kigeni. Halafu kwenye sendofu yenyewe binti kakabidhiwa gari lenye matako ya kumshinda Miss Bantu kabisa! Jinsi alivyo mfupi sijui kama aliweza kuona mbele bila kuweka mito mitatu kwenye kiti. Ili mradi ijulikane pesa zipo.

Lakini bado Bwana Harusi alitaka kumpiku. Kaja na funguo za nyumba ya ghorofa. Kampeleka bibi harusi saluni kwa matarompeta! Hata kwenye saluni jamani! Au alitaka sisi sote mabwege tuone anavyoweza kumwaga pesa.

Na wacha sendofu. Siku hizi pati za jikoni, sijui ni jiko gani ambamo wanapika wao. Utapika kweli na nguo za bei mbaya hivyo? Lakini lazima ifanyike, na michango kibao. Ingekuwa hii ni nchi tajiri ningeelewa lakini sivyo. Nilimsikia binti bosi akisema kwamba hata Ulaya ndoa si za fahari kiasi hicho. Walio nacho wanatulia na walicho nacho. Sisi tunalimbukia tu kutambia tulichokifisadia!

Najua wengine watasema kwamba ni wivu tu unanisumbua. Wivu wa maskini kwa tajiri lakini siamini hivyo. Mbona wameshaachana, tena nasikia chanzo ni ugomvi wa mali. Harusi mali, mapenzi mali, ndoa si hali. Hivyo binti anakaa na gari lake na Bwana anakaa na nyumba yake, wapi na wapi.

Kwa hiyo mpenzi sitaki mambo makubwa. Nataka tushindane katika kuonyeshana mapenzi tu si mali. Upo hapo?

Lakini lazima niseme jambo moja zaidi. Hivi kweli tuna akili timamu? Yule mtoto anayesemekana amemwua mtoto mwenzie mbona anaanika hadharani hivi? Hii ilizua tafrani nyingine kati ya bosi na binti yake. Walikuwa wanaangalia kesi ya yule mtoto kwenye taarifa ya habari.

‘Baba we si Waziri wa Mikiki na Makeke? Mbona huzuii mikiki kwa yule mtoto?’

‘Yaani we mwanangu mdomo wako unawasha vipi? Pilipili ziko shamba …’

‘Hapana baba, nyinyi si mnadai kwamba mnaheshimu haki za binadamu. Sasa iweje mtoto mdogo aonyeshwe mbele ya kadamnasi, na kuhojiwa laivu. Nilidhani mtoto ana haki ya kutoonyeshwa hadharani hivyo.’

‘Kwanza ana miaka kumi na nane …’

‘Tafadhali baba, usinichekeshe. Hebu umwangalie! Ana miaka kumi na nane kweli? Naamini wametangaza hivi ili waweze kumfanyia mikiki hivi maana akiwa chini ya miaka kumi na nane marufuku.’

‘Lakini huoni amefanya ukatili wa ajabu. Mwache akatiliwe na yeye!’

‘He he he! Sasa haki za binadamu ziko wapi? Halafu bado ni mtuhumiwa! Unao uhakika kweli alifanya yeye? Au katumwa? Au ana akili timamu?’

‘Ama kweli mdomo wako unawasha hadi unataka kutetea hata yasiyoteteka.’

‘Sitetei kitendo kile hata kidogo unajua. Lakini nasema kwanza ni mtoto mwenye haki zake na yeye. Na pili, nilidhani mbele ya sheria wewe bado ni mtuhumiwa hadi ushahidi unasikilizwa na hakimu anatoa hukumu. Lakini wote wameshamhukumu yule mtoto bila kuelewa kitu chochote.’

‘Haya, haya, haya. Kwa hiyo?’

‘Baba wewe si Waziri? Si waweza kuagiza watu wafuate sheria? Au hakuna sheria katika nchi hii? Kama watu wanataka kuonyesha mabibi wa mkubwa ni hatari kabisa lakini …’

‘Usianze! Mimi sikai hapa ili utapike upumbavu wako wote.’

‘Lakini baba kwa nini hutaki kusikiliza? Unajua shuleni watu wanasema nini? Wanauliza kwa nini hizi kesi zote za uchawi zinaibuka ghafla namna hii. Na wanasema si bure! Wacha watu wafikirie uchawi wasahau ufisadi.’

Bosi akacheka.

‘Ujinga mwingine. Siku hizi watu wanatafuta fimbo yoyote kupiga serikali kana kwamba hakuna kazi tunayoifanya. Kila kitu kibaya … serikali, kila kitu kibaya … serikali! Mwisho utasema kwamba bahari ikichafuka ni kosa la serikali.’

‘Hapana baba. Lakini nani kweli ni wachawi katika nchi hii? Fisadi hanyonyi damu ya watu? Tena damu ya watu wengi sana. Watu wanadhoofika na kufa kwa sababu pesa za hospitali, na za barabara na za nini sijui zimelambwa kama damu ya watu.’

Lo, mpenzi, nilifikiri baba atapasuka.

‘Sikiliza wewe mwanasiasa chipukizi usiyejua jambo lolote. Kila siku unanishambulia kana kwamba mimi pia ni fisadi hivyo. Nani kakuambia kwamba sisi sote tunafanya hivyo?’

‘Basi wale waliofanya wapelekwe mahakamani kama wachawi. Washtakiwe kwa kunyonya damu, hapo watu watajua kwamba nyinyi hampo. Na mjitoe kwenye klabu hiyo ya mafisi.’

‘Si wewe unasema unataka sheria ifanye kazi yake? Basi wacha uchunguzi ufanyike kisha tutawapeleka wanaostahi kupelekwa.’

BB alionekana anataka kuendelea lakini aliamua kujizuia.

‘Haya baba, si tupo! Tutaona kama kweli watachukuliwa hatua au ni danganyatoto lingine.

Basi mambo ndiyo hayo mpenzi. Lakini naamini kabisa kwa vituko katika jamii ni zao la vituko wanaofanyiwa hadi maisha hayawezekani kabisa.

Akupendaye kwa hali zote bila mali
Hidaya


mabala@gmail.com


Kutoka gazeti la Raia Mwema wiki hii.

No comments: