Tuesday, May 13, 2008

Pemba

Kumekucha



na Waandishi Wetu, Zanzibar na Dar es Salaam

MWANZO wa ngoma ni lele. Hayo ndiyo maneno yanayoweza kueleza kwa ufasaha ni kitu gani kimeanza kutokea huko Pemba.

Siku chache tu baada ya wazee 12 wa Kipemba kuandamana hadi katika Ofisi ya Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na kuwasilisha barua yao ‘nzito’, joto la kisiasa linaonekana kuanza kupanda visiwani Zanzibar na hususan katika Kisiwa cha Pemba.

Tukio la kwanza kubwa la kupanda huko kwa joto la kisiasa limetokea katika kisiwa hicho, usiku wa kuamkia jana, baada ya watu wanaoaminika kuwa ni maofisa wa usalama kuvamia katika nyumba kadhaa usiku wa manane na kuwanyakua baadhi ya Wapemba ambao waliandamana hadi katika ofisi za UNDP, mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Katika tukio hilo la aina yake, maofisa usalama hao waliokuwa wakishirikiana na polisi, walianza operesheni yao hiyo ya siri majira ya saa 5:00 usiku wa kuamkia jana na kuanza kuwakusanya watu na baadaye kupekua nyumba wanazoishi wananchi hao.

Miongoni mwa watu waliokamatwa ni kiongozi wa wazee hao wa Pemba aliyewasilisha barua hiyo UNDP, ikielezwa kuwa ni maoni ya Wapemba wapatao 10,000, Ahmed Marshed Khamis.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, mke wa Marshed, aitwaye Sharifa Mussa, alisema mumewe alichukuliwa nyumbani kwake Mkanjuni, Mkoa wa Kusini Pemba majira ya saa 5:00 usiku.

Akielezea tukio hilo, Sharifa alisema mume wake alichukuliwa na watu watano ambao hawakuwa na sare za polisi, ambao waligonga mlango wao wa nje na wao kulazimika kuamka haraka na kutoka nje kuangalia kinachoendelea.

“Tulishtuka tuliposikia mlango unagongwa kwa nguvu, tukatoka nje, haraka haraka mara tukawaona watu wameingia ndani bila ya kukaribishwa… tukauliza kuna nini, mara wakamwita mume wangu njoo hapa. Wakatoka naye...nilipochungulia nje nikaona gari mbili za polisi,” alisimulia.

Sharifa alisema mume wake ana wake wawili, hivyo mwanzo watu hao walikwenda kumtafuta nyumba kubwa iliyopo Machomanne na baada ya kumkosa huko, ndipo walipokwenda kwake.

“Sijui vipi huko, maana angalau ametoka na nguo… walivyokuja na vishindo nadhani wangembeba hivyo hivyo, tulidhani kuna mtu ameua amekimbilia kwetu, ndiye amefuatwa, maana mwanangu vishindo vilikuwa vikubwa mno,” alisema mama huyo.

Alisema hata hivyo ilipofika asubuhi, polisi hao walifika tena nyumbani kwake wakiwa na mumewe na wakafanya upekuzi kabla ya kuondoka naye tena moja kwa moja.

“Naona asubuhi mapema mume ameletwa na polisi wakaingia ndani wakaanza kusachi kila pembe, wakaondoka, lakini hawakumuacha, wamekwenda na mume wangu, ahhh! Sijui kama amepata angalau chai, mume wangu ni mgonjwa yule,” alilalamika bibi huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Pemba, Ameir Khatib, hakutaka kuzungumzia chochote kuhusiana na kukamatwa kwa watu hao, ingawa alikiri kulifahamu tukio hilo na badala yake akawataka waandishi wawasiliane na Makao Makuu ya Polisi Unguja.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Khamis Mohammed Simba, hakutaka kukubali wala kukataa juu ya suala hilo na akaahidi kutoa habari leo, kwa maelezo kuwa hakuwa na taarifa zaidi alizozipata.

“Mimi nasema njooni kesho, sina taarifa za kukamatwa watu, kwani suala hilo nimepigiwa simu na ninyi, kwa hivyo kama mlivyoniarifu, basi ninafuatilia… sasa hivi ni mapema mno kutoa taarifa,” alisema Kamishna Simba.

Naye Zainab Omar Hamad, ambaye ni mtoto wa Fatma Abdallah Hamad, ambaye ni miongoni mwa watu 12 waliowasilisha barua katika ofisi za UNDP jijini Dar es Salaam, alisema alifuatwa na askari majira ya saa 6:00 usiku akitakiwa kueleza alipo mama yake huyo.

Alisema zaidi ya watu 10 walikwenda nyumbani kwao Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba na kuwaamsha, na kumpakia katika gari la polisi hadi Makao Makuu ya Polisi, walikotakiwa kutoa maelezo kuhusu mahali alipo mama yake.

Binti huyo alisema katika mahojiano hayo, alitakiwa kueleza kile alichokuwa akikifahamu kuhusu waraka huo ambao ulikuwa ukienda kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

“Niliwaeleza kuwa sifahamu chochote. Wakaniuliza mama yangu alipo, nikawaambia kuwa yupo Dar es Salaam tangu alipokwenda kupeleka barua hajarudi… wakanihoji na kuniweka pale kituoni usiku wote ule,” alisema Zainab.

Akizungumza kwa simu na gazeti hili kutoka Pemba, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed, alikiri kushuhudia ‘kunyakuliwa’ kwa baadhi ya wakazi hao wa Pemba usiku wa manane.

“Kwa macho yangu nimeiona ndege ya jeshi ikiwachukua watu hao waliokamatwa na kuondoka nao kwenda sehemu ambayo hatuijui,” alisema Hamad Rashid.

Waandishi wa habari waliokuwa Makamo Makuu wa Jeshi la Polisi Ziwani Zanzibar jana asubuhi, waliwakuta watu kadhaa walioonekana kuwa ni maofisa usalama wakiwa na mabegi yao mfano wa watu waliotoka au wanaojiandaa kwa safari.

Baadhi ya watu hao walikuwa katika Ofisi ya Kamishna wa Polisi wakizungumza naye wakati waandishi walipokuwa wakisubiri kupata taarifa za tukio hilo.

“Ndiyo, ujumbe huu unatoka Dar es Salaam, si unaona mwenyewe wameingia na mabegi yao sasa hivi tena. Unauliza nini, wewe mwenyewe huoni au kwani huoni kama hizo sura si za hapa?” alisema ofisa mmoja wa polisi Makao Makuu Ziwani.

Hata hivyo muda mfupi baadaye, kundi la watu linaloaminika kuwa ni la watu waliokamatwa Pemba lilionekana likiteremeshwa kutoka katika gari moja kabla ya watu hao kuingizwa katika chumba maalumu cha polisi.

Baadhi ya watu wanaoaminika kuwa ni miongoni mwa watu waliokamatwa Pemba usiku huo wa kuamkia jana na wilaya wanazotoka zikiwa katika mabano ni, Ahmed Marshed (Chakechake), Maryam Hamad Bakari (Wete), Jirani Alli Hamad (Micheweni), Gharib Omar Gharib (Wete), Mohammed Mussa (Mkoani), Salim Abeid (Mkoani) na Hidaya Khamisi Haji (Mkoani).

Wanafamilia wengine waliozungumza na Tanzania Daima jana walisema, jana asubuhi walijaribu kuwatafuta ndugu zao hao katika vituo vya polisi vya Pemba bila ya mafanikio.

Hata hivyo wanafamilia hao walisema taarifa walizokuwa nazo ni kwamba jamaa zao hao walikuwa wamesafirishwa kwa ndege kwenda nje ya kisiwa hicho.

Akilizungumzia tukio hilo, Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani, alisema kwamba wamepata malalamiko kutoka kwa wanachama wa CUF Pemba kuwa usiku wa kuamkia jana, polisi walifanya operesheni majumbani na kukamata baadhi ya watu.

“Tumepokea orodha ya watu waliokamatwa katika nyumba zao usiku. Baadaye walipakiwa katika magari na kupekuliwa majumbani mwao, hatujui hadi sasa walichofanya, lakini ni miongoni mwa waliokwenda ofisi za Umoja wa Mataifa,” alisema.

Miongoni mwa madai ambayo wazee hao wa Pemba waliyawakilisha UN ni kutaka kuona Pemba ikipewa haki ya kuunda serikali yake, hatua ambayo mamlaka za dola zimekuwa zikiitafsiri kuwa ni uhaini.

Wiki iliyopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Muungano, Mohammed Seif Khatib, alikaririwa akisema kitendo cha wananchi hao kutaka Pemba ijitenge ni uhaini.

Alisema kwamba kitendo hicho hakina tofauti na kile kilichofanywa na muasi wa Anjouan, Kanali Mohammed Bacar.

Hali ya kisiasa kisiwani Pemba imeanza kutetereka tangu kukwama kwa mazumngumzo ya muafaka hivi karibuni.

Kukwama huko kwa mambo kwa kiwango kikubwa kumetokana na uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi kuamua kuurejesha uamuzi wa kuundwa kwa serikali ya mseto visiwani kwa wananchi, ili wapige kura ya maoni, kabla ya utekelezaji wake haujaanza, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Uamuzi huo wa CCM umesababisha CUF kuandaa maandamano ya nchi nzima kupinga ajenda hiyo ya kura ya maoni ambayo inatafsiriwa na chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar kuwa yenye lengo la kukwamisha muafaka.


Bofya na usome maoni ya wasomaji




No comments: