Friday, May 09, 2008


Tukimhitaji

Dk.Ballali

tutampata-Ikulu



Shadrack Sagati
Daily News; Friday, May 09, 2008 @00:03


IKULU imesema serikali haimtafuti aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dk. Daud Ballali.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu ya Dar es Salaam, Salva Rweyemamu, alisema jana kuwa kama serikali itamhitaji Ballali kurudi nyumbani kujibu tuhuma za wizi wa mabilioni hayo ya fedha, kamwe haiwezi kumkosa.

Dk. Ballali aliondoka nchini akidaiwa kwenda kutibiwa Marekani; lakini baadaye Rais Jakaya Kikwete alibatilisha uteuzi wake kutokana na upotevu wa Sh bilioni 133 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) wakati wa uongozi wake. Profesa Benno Ndulu ndiye aliyepewa nafasi aliyokuwa nayo daktari huyo.

“Ballali hatafutwi na serikali, ikimhitaji atapatikana kwani ina mkono mrefu,” alisema Rweyemamu wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari jana Ikulu; siku moja baada ya gazeti moja la kila siku jana kumkariri Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, akisema kwamba hivi karibuni katika ziara yake nchini Marekani, alimsaka Ballali bila mafanikio.

Mkurugenzi huyo wa mawasiliano alisema kwa sasa Ballali ni raia wa kawaida na siyo tena mtumishi wa serikali, hivyo ana haki ya kwenda kuishi katika nchi yoyote.

Tangu Rais Kikwete alipotengua uteuzi wa Ballali Januari mwaka huu na nafasi yake kujazwa na Profesa Ndulu, kuna utata juu ya wapi yupo gavana huyo wa zamani.

Rais alichukua uamuzi huo baada ya kuipitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na mkaguzi wa nje, kampuni ya Ernst & Young.

Wakati Rais anachukua uamuzi huo ilielezwa na Ikulu kuwa alisikitishwa na kukasirishwa na taarifa za kuwapo vitendo vya ukiukwaji wa makusudi wa sheria, kanuni na taratibu za uuzaji wa madeni ya nje vilivyofanywa katika taasisi muhimu na nyeti kama vile BoT.

Ukaguzi huo ulibaini Sh 133,015,186,220.74 zililipwa katika kampuni 22 zisizokuwa na nyaraka, ama zenye nyaraka batili na nyingine usajili wake haupo kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Baadaye Rais aliunda tume inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Johnson Mwanyika na inahusisha pia Mkuu wa Polisi na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Lakini hata hivyo, tume hiyo haijawahi kusema mahali alipo Ballali.

Kampuni hizo ni Bencon International Ltd, VB & Associates Company Ltd, Bina Resorts Ltd, Venus Hotel Ltd, Njake Hotel &Tours Ltd, Maltan Mining Company Ltd, Money Planners & Consultants na Bora Hotels & Apartment Ltd.

Nyingine ni B.V. Holdings Ltd, Ndovu Soaps Ltd, Navy Cut Tobacco (T) Ltd, Changanyikeni Residential Complex Ltd, Kagoda Agriculture Ltd, G&T International Ltd, Excellent Services Ltd, Mibane Farm, Liquidity Services Ltd, Clyaton Marketing Ltd, M/S Rashtas (T) Ltd, Malegesi Law Chambers (Advocates, Kiloloma and Brothers na Karnel Ltd.

Katika orodha hiyo zimo G&T International Ltd, Excellent Services Ltd, Mibane Farm, Liquidity Service Ltd, Clayton Marketing Ltd, M/S Rashtas (T) Ltd, Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloloma and Brothers na Karnel Ltd, Rashtas (T) Ltd.

No comments: