
Jeshi la Kujenga Taifa
kwa mujibu wa sheria
kurejeshwa mwaka 2010
NAIBU Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Emanuel Nchimbi, amesema kuwa kuanzia mwaka 2010 serikali itarejesha utaratibu wa wahitimu wa elimu ya kidato cha sita na vyuoni kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa.
Naibu Waziri huyo alisema hayo jana alipojibu swali bungeni, akiongeza kuwa, wizara yake inatambua bayana umuhimu wa ulinzi kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania na kwamba kutokana na hali hiyo, ni lazima mfumo huo utarejeshwa.
Akijibu swali la msingi, Nchimbi alisema kuwa wanajeshi kwa ujumla wanapoingia jeshini lazima wawe na sifa ya kuanzia elimu ya msingi, sekondari hadi elimu ya juu.
Alisema kuwa, wanajeshi pia hupatiwa mafunzo ya ujuzi mbalimbali wawapo kazini ambayo huwasaidia wanapohitajika kwenda kufanya kazi za ulinzi wa amani nje ya nchi.
“Kama nilivyoeleza katika sehemu ya hapo juu, wastani wa elimu ya askari wetu ni kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu,” alisema Nchimbi na kuongeza kuwa:
''JWTZ huajiri askari toka JKT, kigezo cha urefu na maumbile ni baadhi tu ya sifa wanazotakiwa kuwa nazo vijana wanaojiunga na JWTZ.''
Alisema pia kuwa, kupeleka majeshi katika nchi za nje kulinda amani kunasaidia kujenga mahusiano, ingawa pia alisema kuwa katika jeshi urefu na ufupi huhitajika kutegemea na kazi atakazofanya askari mhusika.
Katika swali la Msingi, Mbunge wa Chakechake, Fatma Maghimbi (CUF), pamoja na mambo mengine, alitaka kujua iwapo elimu kwa askari kwenda kufanya kazi nje siyo kikwazo, na pia alitaka kujua serikali inaweza kueleza wastani wa elimu ya askari wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment