Kitabu Nilichokiandika
Kuhusiana na Maisha
ya Barack Obama
kimesababisha CNN
Kuongea Nami-
Maggid Mjengwa
Jana asubuhi nilipata ugeni wa CNN kwenye kiofisi changu'kijijini'Kinondoni Biafra. Ugeni huo uliokuja kunitembelea na kunihoji kuhusiana na uchaguzi wa Marekani na hususan kitabu nilichokiandika kuhusiana na maisha ya Barack Obama; alikotoka, aliko na anakokwenda. Hakika nafurahi kuandika,kuwa kitabu hiki ni moja ya kazi zangu za kiuandishi zilizopatwa kusomwa na Watanzania wengi zaidi wa kada mbalimbali kuliko kazi zangu nyingine zote.
Kwa mujibu wa taarifa za wauza vitabu, hiki ni kitabu chenye kuuzwa kwa kasi zaidi kuliko vitabu vyote kwa sasa hapa nchini. Na ndio sababu hata CNN wametaka kuongea nami. Kwa ufupi nimewaambia watu wa CNN kuwa kwa matokeo yeyote yatakayokuwa ifikapo Novemba nne, Barack Obama atakuwa ameweka historia kwa kuwa Mwamerica wa kwanza mwenye asili ya Afrika kuwania nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa kisiasa katika America.
Kwamba Watanzania wengi mijini na vijijini wamekuwa wakifuatilia habari zake tangu walipojua adhma yake ya kutaka kuwania kiti hicho. Kwa vile mimi ni mmoja wa waelimishaji jamii ama (Adult educator) niliye na fursa ya kupata taarifa nyingi kumhusu Obama kupitia vyanzo mbalimbali ikiwamo vitabu alivyoviandika Obama mwenyewe, niliona mapungufu ya taarifa katika uelewa wa Watanzania wengi juu ya Obama hususan juu ya alikotokea, aliko na anakokwenda.
Niliona ni wajibu wangu wa kuandika japo kitabu kidogo kusimulia kwa namna yangu juu ya mtu huyo Obama.Nilijiuliza swali kabla ya kukiandika;nataka nini kupitia kitabu hicho? Nikapata majibu; Mosi, nataka kuinua kiwango cha hamasa ya usomaji vitabu ambapo kwa sasa iko chini mno. Na kupitia simulizi za Obama yaweza kuwa njia muafaka. Pili, nataka kiwe ni cha kuelimisha hususan kuhusu siasa na mwisho kiwe ni chenye kutufanya Watanzania tutafakari juu ya hali yetu ya kisiasa kwa sasa hasa inapohusu masuala ya Katiba na hata wajibu wa Wanahabari katika chaguzi.
Kwa kiwango kikubwa nimefanikiwa kufikia malengo hayo matatu. Na katika hilo la kwanza la kuhamasisha usomaji ndio sababu niliamua kitabu kiuzwe kwa bei ya chini sana ili kiwafikie Watanzania wengi hata kama wachapishaji waliniambia ningeweza kuuza kwa shilingi 2000 hadi 3000 kwa kitabu. Sikuwa na dhamira ya kutengeneza faida ya kibiashara bali nimepata faida kubwa ya kijamii; kwamba maelfu kwa maelfu ya Watanzania wamesoma na wanaendelea kusoma kitabu hiki.
Kuna mamia ya Watanzania wanaonipigia simu na kunitumia SMS. Kuna mifano ya waliobainisha kuwa kitabu hicho kwao ndio cha kwanza kukisoma na kukimaliza.
Mwingine amenunua vitatu, cha kwake na vingine kwa wanawe walio shuleni ili wahamasike kusoma vitabu na kujijengea ujasiri kama wa Obama!Ifikapo katikati ya Oktoba tuna hakika hakutakuwa na nakala iliyobaki ya kitabu hicho.
Sina mpango wa kuchapa nakala nyingine isipokuwa nafikiri hii ni njia nzuri ya kuinua hamasa ya kusoma, nafikiri kutafuta maudhui mengine yenye kuvutia na kuwaandakia Watanzania wenzangu hawa walionyesha kukubali aina ya uandishi wangu na kuwavuta katika kutaka kufuatilia kazi zangu. Na naelewa, kuwa katika hili siku zote kuna wachache watakaonikebehi na hata kunidhihaki, na laiti ningewafikiria sana hao,leo ningewanyima maelfu ya Watanzania wenzangu fursa ya kupata maarifa mapya.
Ni Watanzania wenzangu hawa ambao kupitia kodi zao wameniwezesha nisomeshwe na Serikali na kupata elimu na maarifa haya niliyonayo.Deni lao kwao ni kubwa sana.Kamwe siwezi kulilipa nikalimaliza. Mwisho kabisa,watu wa CCN waliniuliza kwanini Watanzania wengi wanamshabikia Obama?
Niliwachekesha nilipowajibu; kuwa kama Tanzania ingekuwa ni jimbo katika Marekani, basi, Obama asingekuwa na haja ya kufanya kampeni, angepata 99.9% ya kura zote! Lakini nililisitiza kuwa Watanzania na Waafrika wengi hawamshabikii Obama kutokana na rangi yake au asili yake bali sera zake.
Wengi wanazikubali sera za Obama, wanaamini endapo ataingia Ikulu ya Marekani, basi, mabadiliko na matumaini anayoyaelezea Obama katika sera zake huenda nao yakawafikia. Naam. Kama Obama atashindwa ni bahati mbaya kwake,lakiki hata mimi, kupitia CNN,nimejitahidi kujenga hoja na kumpigia'debe' Obama kwa wapiga kura wa America ambao wataona coverage hiyo ya watu wa Afrika wanavyomzungumzia Obama siku ya Jumamosi usiku kwa mujibu wa maelezo ya jamaa wale wa CNN.
Mdau
Maggid Mjengwa.
No comments:
Post a Comment