
POLISI Mkoa wa Kusini Zanzibar imemkamata Mama Lishe na kuwapokonya sahani za wali vibarua na mafundi wa kampuni ya ujenzi kwa kosa la kula mchana katika kipindi cha mfungo.
Kivumbi hicho kilitokea juzi katika Kijiji cha Dunga, Mkoa wa Kusini Unguja, baada ya vibarua hao na mafundi kwenda kula chakula cha mchana kwa mama lishe huyo.
Kampuni hiyo ya S.S. Mehta inajenga barabara ya Dunga inayofadhiliwa na Benki ya Afrika (ADB) kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Vibarua na mafundi wa kampuni hiyo walikumbwa na mkasa huo wakati wakiwa wamekaa mkao wa kula ndani ya nyumba ya mama lishe huyo iliyojengewa uzio.
Polisi walivamia nyumba hiyo baada ya kupata taarifa kuwa kuna watu wanakula machana katika mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Imeelezwa polisi watatu waliokuwa wamevalia sare zao waliwaweka chini ya ulinzi watuhumiwa na kuwataka wasalimishe sahani zao za vyakula na baadaye kumpeleka Mama Lishe katika Kituo cha Polisi cha Dunga.
Wakizungumza na Tanzania Daima, wafanyakazi wa Kampuni ya S.S Mehta, wakiongozwa na Simon Joseph, walisema walitekeleza amri ya polisi iliyowataka wasalimishe sahani za wali.
Wafanyakazi hao walidai ni kawaida yao kwenda kupata chakula cha mchana ndani ya nyumba hiyo katika wa mwezi huu wa Ramadhani.
“Kwa kweli tumeshangazwa na kitendo cha polisi cha kutuvamia ndani ya nyumba wala si sehemu ya nje,’’ walilamika wafanyakazi hao.
Aidha, askari polisi walichukua pia sahani za chakula za wote waliowahi kumaliza chakula chao kabla ya uvamizi wa polisi.
Walisema sahani zilikusanywa kama kielelezo cha kula mchana wakati wa mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Kaimu Kamanda Polisi Mkoa Kusini Unguja, Rajab Khamis, alipoulizwa kuhusu kutokea kwa jambo hilo, alisema hana taarifa.
Kawaida migahawa yote ya nje hufungwa na wananchi wasiofunga hutakiwa kula kwa kujificha kuepuka kuwabughudhi waliofunga.
Kutoka gazeti la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment