Rais Kikwete
asikitishwa na
waliompopoa mawe
Salim Said na John Stephen
Rais Jakaya Kikwete amesikitishwa na kitendo cha wananchi wa Kijiji cha Kanga wilayani Chunya kuurushia mawe msafara wake na kuwajeruhi baadhi ya watu waliokuwa kwenye msafara huo.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu wakati akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) baada ya msafara wa Rais Kikwete kushambuliwa kwa mawe na wananchi wa kijiji hicho.
Rweyemamu alisema kuwa Rais Kikwete amesikitishwa na tukio hilo na kwamba, alishindwa kusimama na kuwasalimia wananchi wa kijiji hicho kwa kuwa muda haukuruhusu kufanya hivyo.
"Rais amesikitishwa kwa kuwa alishindwa kusimama na kuwasalimia wananchi, lakini pamoja na hayo mazingira ya jana asingeweza kusimama," alisema Rwehemamu.
Alisema tukio hilo, lilitokea baada ya saa 1:00 jioni na kwamba, baadhi ya vijana waliurushia mawe msafara huo baada ya kuona Rais anawapita bila kusimama na kuwasalimia.
Kufuatia kupigwa huko kwa mawe kwa msafara wa Kikwete juzi Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad amemtaka Rais huyo kuitisha kongamano la kitaifa la wadau wote kujadili na kutafuta suluhu ya hali mbaya ya nchi.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalum ofisini kwake Buguruni jijini Dar es Salaam jana Hamad alisema nchi inayumba kwa kukosa mwelekeo wa kiongozi imara na kwamba inavimba huku wakionya kuwa wakati wowote inaweza kupasuka.
No comments:
Post a Comment