Sunday, November 30, 2008


Soo la EPA...



...........Gavana Balali aliruhusu na/au kuidhinisha na/au kunyamazia mkopo usio na riba wa Dola za Marekani 5,512,398.55 kwa kampuni ya Mwananchi Gold Co. Ltd. kati ya mwaka 2004 na tarehe 30 Juni 2006. Kati ya fedha hizo, deni la dola 2,807,920 limedhaminiwa kwa dhahabu ghafi ambayo ingenunuliwa kutokana na fedha za mkopo zilizotolewa na Benki Kuu yenyewe! Kwa maana rahisi ni kwamba kampuni ya Mwananchi Gold haijatoa dhamana yoyote inayoeleweka kwa mabilioni ya shilingi ilizokopeshwa na Benki Kuu chini ya Gavana Balali. Kwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, hadi kufikia mwezi Desemba 2006 Mwananchi Gold Co. Ltd. ilikuwa imeshindwa kulipa hata riba ya mkopo huo kwa kiasi cha dola za Marekani 62,847.91. "Katika mazingira haya", inasema barua ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, "hatukuweza kujiridhisha kwamba deni la dola la Marekani 5512398.55 inalodaiwa (Mwananchi Gold Co. Ltd.) hadi kufikia tarehe 30 Juni 2006 linaweza kulipika." 

Je, ni kampuni gani hii iliyopewa mamilioni ya fedha za umma katika fedha za kigeni bila kudaiwa riba au kupewa kipindi maalumu cha kulipa mkopo huo? Kufuatana na taarifa za BRELA, Mwananchi Gold Co. Ltd. ni kampuni binafsi ambayo wanahisa wake ni Benki Kuu ya Tanzania yenye hisa 500, Shirika la Maendeleo la Taifa (hisa 500), Mwananchi Trust Co. Ltd. (hisa 1,123) na Chimera Co. Ltd. (hisa 500). Kampuni hii ilisajiliwa kama kampuni binafsi tarehe 12 Desemba 2002. 

Mawakili wake ni kampuni ya mawakili ya Nyalali, Warioba & Mahalu Associates ikiwashirikisha aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania wakati huo marehemu Francis L. Nyalali, Waziri Mkuu wa zamani Joseph Sinde Warioba na aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia Profesa Costa R. Mahalu. Wakurugenzi wa Mwananchi Gold ni Joseph Sinde Warioba, Gavana Daudi Balali, Col. J. Simbakalia, Vulfrida Grace Mahalu, Yusuf H. Mushi na raia wawili wa Italia, Paolo Cesari na Patrizio Magrini. Vulfrida Mahalu ni Ofisa Mkuu Mtendaji wa kampuni binafsi ya VMB Holdings (1996) Ltd. na pia ni mke wa Profesa Mahalu ambaye kwa sasa anakabiliwa na tuhuma za kuhujumu uchumi kutokana na madai ya wizi wa zaidi ya shilingi bilioni tatu za Serikali wakati akiwa balozi wa Tanzania nchini Italia! Kanali Simbakalia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Taifa na Yusuf Mushi ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni binafsi ya Business Machines Consultants (T) Ltd

Source: Jamii Forums



No comments: