Saturday, November 15, 2008

TAARIFA YA SERIKALI KWA

VYOMBO VYA HABARI KUHUSU

KUSUDIO LA WALIMU LA

KUTAKA KUGOMA



1. Tarehe 13 Oktoba, 2008 Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi ilitoa amri ya kusitisha mgomo usiokuwa na ukomo wa walimu uliokuwa umekusudiwa kuanza tarehe 15 Oktoba, 2008 na kuendelea, ili kutoa fursa kwa majadiliano yaliyokuwa yanaendelea kati ya Serikali na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kufikia ufumbuzi. CWT hawakuridhika na uamuzi huo hivyo walipeleka maombi yao ya marejeo ya uamuzi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi kwenye Mahakama ya Rufani. Katika maombi yao hayo, walidai kuwa Mahakama Kuu ilisikiliza shauri ambalo lilikuwa limepelekwa mbele ya Mahakama ile chini ya Kifungu kisichokuwa sahihi kulingana na maombi husika.

2. Mahakama ya Rufani, katika uamuzi wake kuhusu suala hilo ulioandaliwa tarehe 11 Novemba, 2008 na kusomwa tarehe 13 Novemba, 2008, ilikataa maombi ya CWT ya kutaka kurejewa kwa uamuzi wa Mahakama Kuu na kuelekeza kuwa walipaswa kukata rufaa badala ya kuomba marejeo.

3. Hata hivyo, Mahakama ya Rufani, kwa kutumia mamlaka yake yenyewe iliamua pia kuwa maombi ya Serikali yaliyowasilishwa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, yalikuwa yamewasilishwa kupitia Kifungu cha Sheria kisicho sahihi. Kwa sababu hiyo, Mahakama ya Rufani ilifuta mwenendo wote pamoja na maamuzi juu ya shauri lile.

4. Ni vema isisitizwe hapa kwamba Mahakama ya Rufani haikutamka kwamba mgomo usio na kikomo uliokusudiwa kuanzishwa na CWT ulikuwa halali na wala haikuruhusu kufanyika kwa mgomo huo. 

Baada ya uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani, Serikali imepata taarifa ya Tamko la CWT la tarehe 14 Novemba, 2008 lililotolewa na Mwal. Gratian Mukoba, Rais wa CWT kupitia vyombo vya habari kwamba, pamoja na mengineyo, wanachama wa CWT wataanza mgomo wao usio na kikomo siku ya Jumatatu tarehe 17 Novemba, 2008. 

Pia katika tamko lao, CWT wametoa mapendekezo ya namna ya kuboresha zoezi la uhakiki wa madai ya madeni yao linaloendelea ambayo wanaitaka Serikali kuyafanyia kazi.

Serikali kwa upande wake imeendelea kulipa madai mbalimbali ya walimu na watumishi wengine kwa mujibu wa taratibu zilizopo. Aidha, Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi kwa Taifa ya tarehe 31 Oktoba 2008, alielekeza na kuahidi kuwa Serikali italipa madeni yote ya walimu yaliyohakikiwa. 

Maelekezo ya Mhe. Rais yalirejewa tena na Mhe. Waziri Mkuu tarehe 7 Novemba, 2008 alipokuwa akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 13 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuahidi kwamba Serikali itakamilisha uhakiki huo mapema iwezekanavyo. Serikali hivi sasa inakamilisha zoezi la uhakiki wa madeni ya walimu na italipa madeni yote yaliyohakikiwa ifikapo tarehe 30 Novemba 2008. Kuanzia tarehe 17 Novemba, 2008, Wizara ya Fedha na Uchumi itaanza kupeleka fedha kwenye Halmashauri zote 133 tayari kwa malipo. Kwa hiyo, Serikali inawataka walimu kuwa na subira kwani kwa hatua hizi zinazochukuliwa na Serikali hatuoni busara ya walimu kugoma. 

Walimu ni watumishi wa umma, na kama ilivyo kwa watumishi wote wa umma, masuala yahusuyo mgomo lazima kwanza yawe yameshughulikiwa na kukamilika chini ya Sheria ya Majadiliano ya Pamoja Katika Utumishi wa Umma Na. 19 ya mwaka 2003 ambayo imeweka masharti yanayohitaji kutimizwa kabla ya watumishi kugoma. Katika kusudio la walimu la kutaka kugoma, baadhi ya masharti hayakutimizwa na ndio maana Serikali inapinga mgomo batili usio na kikomo unaokusudiwa. 

Tayari Serikali imekwishawasilisha katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi Maombi Anuai Na. 21 ya 2008 kuiomba Mahakama Kuu izuie mgomo usio na kikomo unaokusudiwa. Aidha, CWT wamepelekewa samansi ya kuitwa Mahakamani kwa ajili ya shauri hilo la maombi anuai ambalo limepangwa kusikilizwa tarehe 17 Novemba, 2008.

Kutokana na hatua hizi zinazoendelea kuchukuliwa, Serikali inakitaka Chama cha Walimu kufanya yafuatayo:- 

Kusitisha mgomo wao usio na ukomo unaokusudiwa kuanza tarehe 17 Novemba 2008, kwa kuwa tayari Serikali inashughulikia kwa ukamilifu madai ya madeni yao. 

Serikali inawashauri CWT wawasilishe rasmi Serikalini mapendekezo yaliyo kwenye tamko lao, kuhusu namna ya kuboresha zoezi la uhakiki wa madai ya madeni ya walimu, na Serikali iko tayari kuyafanyia kazi. Serikali inaamini kwamba iwapo mgomo utaendelea, utainyima fursa ya kushughulikia mapendekezo ya CWT yaliyo katika tamko lao. 

Kwa kuwa mgomo unaokusudiwa haukutimiza masharti yote yaliyotajwa katika Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma, mgomo huo machoni mwa Serikali kama mwajiri ni batili na walimu watakaoshiriki kwenye mgomo huo wanaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria hiyo. Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 mtumishi atakayeshiriki kwenye mgomo batili, hatalipwa mshahara na Serikali, kama mwajiri kwa kipindi chote cha mgomo. Itabidi mshahara wake ulipwe na aliyeitisha mgomo huo.

10. Ikumbukwe kuwa tayari suala hili liko Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, hivyo walimu hawapaswi kugoma kwa sababu kufanya hivyo ni kuishinikiza mahakama kutoa maamuzi ambayo walimu wanayataka, kitendo kinachoingilia uhuru wa mahakama. Mgomo huo hauna maslahi kwa umma na hata kwa walimu wenyewe kwa sababu unakusudiwa kufanyika katika kipindi ambacho wanafunzi wanapaswa kufanya mitihani yao ya kuvuka madarasa au vidato.
Hivyo, kwa kuwa Serikali inayafanyia kazi madai ya madeni ya walimu, na kwa kuwa mgomo unaokusudiwa kufanyika ni batili na usio na maslahi yoyote kwa Taifa, Serikali inawataka CWT kusitisha kusudio lao la kufanya mgomo usio na kikomo uliopangwa kuanza tarehe 17 Novemba, 2008 na kuwataka walimu wote kuendelea na kazi zao kama kawaida.

(Phillemon L. Luhanjo)
KATIBU MKUU KIONGOZI NA
MKUU WA UTUMISHI WA UMMA
15 Novemba, 2008

No comments: