Sunday, December 14, 2008

Makazi ya kale yagundulika

baharini, pwani ya Tanzania


CHUO Kikuu cha Dar es Salaam Kitengo cha Mambo ya Kale kimegundua makazi ya watu wa kale chini ya Bahari ya Hindi.

Makazi hayo yanasemekana yalikuwa ni ya watu waliokuwa wanaishi kwenye Kisiwa cha Zanzibar miaka 3000 kabla ya Kristo.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo hicho, Profesa Felix Chami alisema walipochunguza kwa makini makazi hayo waligundua makazi hayo yalikuwa na kumbi tatu.

Kwenye kumbi hizo walikuta mifupa ya binadamu, vyungu, shanga na vitu mbalimbali ambavyo walikuwa wakitumia enzi hizo.

Alisema, watu hao walikuwa wanatumia mawe kuhesabu nyakati, na waliofariki walitengewa maeneo maalumu ya kuzikwa.

“Tulifanya utafiti na kukuta mabaki ya watu wa kale vikiwamo vyungu, shanga, mawe makubwa ambayo yalikuwa yanatumika kuzikia mabaki hayo,”alisema Profesa Chami.

Aliongeza kuwa, katika eneo hilo walilolipa jina Kuhumbi, pia walikuta mabaki ya wanyama mbalimbali waliokuwa wakitumika katika shughuli zao, ikiwemo kitoweo.

Alisema, katika utafiti wao wamebaini kuwa, binadamu na wanyama hao waliweza kuishi miaka 5000 kabla ya Kristo.

Profesa Chami alisema kuwa, utafiti huo ulianza mwaka 2005 kwa kwa upande wa Chuo Kikuu cha Dar es Salam, lakini kwa upande wa makumbusho ya Zanzibar ulianza mwaka 1999 na bado unaendelea.

Ugunduzi mwingine wa namna hiyo umepatikana katika Kijiji cha Ikwiriri wilayani Rufiji, ambako waliweza kugundua mji wa kale ambao ulikuwa unatumiwa na warumi kwa ajili ya shughuli zao za biashara miaka 2000 kabla ya kristo.

Alisema, mji huo ambao unasaidikiwa ulikuwa kwenye latitudo 7.8 kutoka Ikweta uliitwa ‘Rhapta’ na ulikuwa maarufu kwenye eneo la Kusini na yalikuwa ni makazi ya Warumi.
“Katika eneo hilo tumekuta mabaki ya vyungu, shanga na vitu mbalimbali ambavyo vimetapakaa kila sehemu ambavyo inasadikiwa ni mali ya warumi kwa kuwa walikuwa wakifanya biashara,”alisema.

Aliongeza kuwa, katika eneo hilo kulikuwa na mto mkubwa ulikuwa unaingiza vyombo vingi vya usafiri wa majini.

Alisema,utafiti wa kugundua vitu hivyo ulianza mwaka 1995, ambapo mwaka 1996 waliweza kuona alama mbalimbali za watu hao katika eneo hilo.

Profesa Chami alisema, mikakati iliyopo ni kuhakikisha kuwa, wanachimba maeneo hayo ili waweze kugundua vitu vingine ambavyo vilikuwa vinatumika miaka hiyo.

Kutoka gazeti la Mwananchi.

No comments: