Monday, January 05, 2009

HUKU wakitoa tahadhari kubwa ya majina yao kuwekwa kapuni kwa kuhofia kuchukuliwa hatu za kinidhamu, kwa nyakati tofauti wachezaji wa Klabu ya Yanga ambao wapo hapa jijini na nchini Uganda kwenye michuano ya Chalenji walisema: “Kondic ajiuzulu.”

Wakizungumza kwa jazba na waandishi wetu, walisema kitendo cha Mwenyekiti wa klabu hiyo, Imani Madega kunukuliwa akisema kwamba wachezaji wakiwa kikosini hawajitumi kama kwenye timu ya taifa na kudai kwamba kama siyo Yanga basi wachezaji hao wasingecheza kwenye kikosi cha Mbrazil Marcio Maximo kimewahuzunisha.

“Uongozi hauna budi kuelewa kwamba tukiwa Stars ndiyo tunajifunza mbinu nyingi kuliko klabuni, kwanza kocha wetu hana jipya kwani siku zote mambo anayofundisha ni yale-yale.

“Nadhani mwenyekiti wa klabu angefahamu hilo asingeweza kutoa kauli kama hiyo kwani tunapata mbinu nyingi tukiwa na Maximo kuliko Kondic ni bora Mserbia huyo ajiuzulu tuletewe kocha atakayeweza kutusaidia kuinua viwango vyetu zaidi,” kauli hiyo ilitolewa kwa nyakati tofauti na wachezaji wa Yanga.

Waliendelea kufafanua kwamba: “Hebu jiulize, timu imesajili wachezaji 30 na waliopo timu ya taifa wapo kama 12, inakuwaje ikatae kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi ambalo lingeendelea kuwapa uwezo na mazoezi wale 18 waliobaki kikosini?

“Mbona Simba imetoa wachezaji wanane timu ya taifa na bado imekubali kushiriki Kombe la Mapinduzi? Kondic woga mtupu, ameshaelewa kwamba bila wale wa Stars ambao wanapata mbinu kutoka kwa Maximo hana ujanja.

“Kama kweli waliopo Stars hawajitumi kwanini wasitupe nafasi sisi hasa kwa kukubali kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi? Kaka hizo ni janja zao, wakae na sisi tuwaeleze, kwani Mserbia huyo hana jipya na Maximo ndiye anayembeba.

“Hebu angalia Jerry Tegete anapotokea Stars kiwango chake kinavyokuwa juu, lakini akikaa klabuni kwa muda anapoteza muelekeo,” walieleza wanasoka hao.

Hali ni tete ndani ya timu hiyo tangu ilipotolewa kwenye michuano ya Kombe la Kagame mapema mwaka jana, hata hivyo ilikuwa haijionyeshi wazi, lakini baada ya timu hiyo kutolewa katika michuano ya Tusker siri zote zilianza kuwekwa hadharani.

Taarifa zilizonaswa ndani ya klabu hiyo ambayo inafadhiliwa na Yusuf Manji zinadai kuwa hali sio shwari hata kidogo kwa Kondic, kwani licha ya madai hayo ya wachezaji, amekuwa haelewani na viongozi, hivyo kuna tetesi za chini kwa chini kwamba mchakato wa kusaka kocha mwingine u-mbioni kuanza.

“Kutoelewana huko kwa Kondic na viongozi ndiko kulikochangia hata John Njoroge na Joseph Shikokoti kununuliwa wakati dirisha dogo limeshafungwa, kwani Kondic alikuwa anawasiliana zaidi na Manji badala ya uongozi,” kilieleza chanzo chetu.

Mhariri wa Championi na Jopo Lake, unawaomba viongozi wa Yanga, wachezaji, wanachama na kocha kumaliza malumbano hayo kwani ni hatari hasa kipindi hiki ambacho timu inakabiliwa na michuano ya kimataifa.

No comments: