Wednesday, January 28, 2009

Lazima Wabunge wajue
Kiingereza?


SERIKALI imetoa wito kwa wabunge ambao wana tatizo la kuelewa lugha ya Kiingereza kuweka juhudi za makusudi katika kujifunza lugha hiyo ili waweze kufahamu masuala mbalimbali yanayoendelea duniani.

Wito huo ulitolewa jana na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), Aggrey Mwanri, wakati akijibu swali la Mbunge waViti Maalumu, (CCM) Martha Mlata, aliyehoji sababu inayowafanya viongozi wa Afrika Mashariki kuzungumza na wabunge wa Tanzania kwa lugha ya Kiingereza wakati vikao vya Bunge vinaendeshwa kwa lugha ya Kiswahili.

Katika swali lake hilo, Mlata alihoji iwapo viongozi hao hawaelewi kuwa wabunge wengi wa Tanzania hawaelewi Kiingereza na kwamba si lugha yao na kwamba ni kwa nini Bunge linapopata wageni wasiofahamu lugha ya Kiswahili asitafutwe mkalimani ili waweza kusikia kwa urahisi kinachozungumzwa na mgeni huyo.

Katika majibu yake, Mwanri, alisema Ibara ya 144 (1) ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la 2007 inatamka kuwa shughuli za Bunge zitaendeshwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza bila tafsiri ya lugha hizo kutolewa.

Alisema kutokana na mwongozo wa kanuni hiyo ndiyo maana hakuna mkalimani wa kutafsiri hotuba za viongozi zinatolewa bungeni hadi sasa.

Aliongeza kuwa Ofisi ya Bunge ina mkakati wa kuweka vifaa maalumu vya kutafsiri wakati Bunge linapopata mgeni asiyefahamu Kiswahili, hata hivyo alisema hakubaliani na kauli kuwa wabunge wengi hawajui lugha ya Kiingereza kwa sababu sifa moja ya mtu anayestahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge ni kujua kusoma na kuandika katika lugha ya Kiingereza.

Kutoka Tanzania Daima soma maoni ya wasomaji


No comments: