Salaam za mwaka mpya
kwa Watanzania kutoka
kwa Rais Jakaya Kikwete
Ndugu Wananchi;
Hatimaye imewadia ile siku ya kuuaga mwaka mmoja na kuukaribisha mwingine. Leo tunauaga mwaka 2008 na kuukaribisha mwaka 2009.
Kwanza kabisa, naomba sote tumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujaalia uhai na kutuwezesha kuiona siku hii adhimu salama. Ni wajibu wetu kumshukuru Muumba wetu kwani wapo wenzetu wengi hawakujaaliwa kuiona siku ya leo kwa vile wametangulia mbele ya haki. Wakati tukikumbushana wajibu wetu wa kumuomba Mwenyezi Mungu awape marehemu wetu hao mapumziko mema, tumuombe pia awape nafuu na kuwaponya wenzetu wote wanaougua maradhi mbalimbali ili wajumuike nasi katika shughuli za ujenzi wa taifa letu.
Ndugu Wananchi;
Mwaka wa 2008 tunaoumaliza leo ulikuwa mwaka wa aina yake kwa taifa letu na katika historia ya uongozi wangu. Ulikuwa ni mwaka ambao tumepata mafanikio mengi mazuri na mengine ya kihistoria katika nyanja mbalimbali za maisha ya wananchi wa Tanzania na taifa letu. Lakini, pia kulikuwepo na changamoto au matukio machache ambayo yalisababisha baadhi ya watu ndani na nje ya nchi yetu wapate shaka juu ya hatima ya umoja, amani na utulivu wa nchi yetu. Umoja, amani na utulivu ndiyo nguzo kuu na sifa kubwa inayoitofautisha na kutambulisha Tanzania miongoni mwa mataifa barani Afrika.
Ndugu Wananchi;
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba tumeumaliza mwaka huu kwa usalama, amani na utulivu. Tuzidi kumuomba baraka na rehema zake, katika mwaka 2009, ili nchi yetu iendelee kuwa na amani, utulivu na watu wake waishi kwa upendo, umoja, masikilizano, mshikamano na ushirikiano kama ndugu wa taifa moja.
Pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu, hatuna budi kutambua kuwa dhamana ya kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa tulivu na yenye amani na upendo miongoni mwa watu wake ni yetu wenyewe. Ni ukweli ulio wazi kuwa katika mwaka huu tunaoumaliza sasa baadhi yetu tumekuwa tunafanya vitendo au kutoa kauli ambazo zilikuwa zinalielekeza taifa kubaya. Tena tulikuwa tunafanya hivyo kwa ajili ya kuendeleza manufaa binafsi ya kisiasa. Ni matumaini yangu kuwa tutajiepusha na mambo hayo katika mwaka 2009. Nawasihi viongozi wenzangu wa kisiasa na wa kijamii tubadilike, tuweke mbele maslahi ya taifa ili tuiepushe nchi yetu na mabalaa ambayo baadhi ya wenzetu yaliwakuta.
Hali ya Uchumi wa Nchi na Dunia
Ndugu Wananchi;
Kwa jumla hali ya uchumi wa nchi yetu kwa mwaka 2008 ilikuwa ya kiwango cha kuridhisha. Lakini, hali ingekuwa bora zaidi kama uchumi wa dunia usingepata misukosuko iliyoupitia sasa. Kwa sababu ya matatizo makubwa yanayoukabili uchumi wa dunia, baadhi ya malengo tuliyojiwekea kuhusu ukuaji na mwenendo wa uchumi wetu yameathiriwa.
Mfumuko wa Bei
Ndugu Wananchi;
Bei kubwa za mafuta zilizokuwepo kwa karibu miaka miwili mfululizo na hasa katika miezi kumi ya mwanzo ya mwaka huu zilipokuwa juu sana, imekuwa kichocheo kikubwa cha kupanda sana kwa mfumuko wa bei na ukali wa maisha hapa nchini. Aidha, kupanda sana kwa bei za vyakula tunavyoagiza kutoka nje kama vile ngano, mchele na vinginevyo viliifanya hali ya mfumuko wa bei kuwa mbaya zaidi.
Tulikuwa tumejiwekea lengo, kwa mfano, katika bajeti iliyopita kuwa tutateremsha mfumuko wa bei hadi kuwa asilimia 4.5 mwezi Juni, 2008 kutoka asilimia 5.9 ya mwezi Juni, 2007. Badala yake mfumuko wa bei ukawa asilimia 9.3 mwezi Juni, 2008 na kupanda hadi asilimia 12.3 ilipofika mwezi Novemba, 2008. Hivi sasa bei za mafuta zimeshuka kuanzia Oktoba, 2008 na hivi leo zimefikia dola za Kimarekani 38.4. Hali kadhalika, bei za baadhi ya vyakula nazo zimeshuka. Lakini, itachukua muda mpaka manufaa ya hali hiyo kuonekana kwa uchumi wa nchi yetu na wananchi wake.
Ndugu Wananchi;
Wakati mwingine hali huwa hivyo kwa sababu ya ukaidi na tamaa ya wafanyabiashara. Nimekwishawaagiza Mawaziri wahusika kuzibana mamlaka husika kutimiza ipasavyo wajibu wao kwa mujibu wa mamlaka waliyopewa kisheria kuwalinda wananchi dhidi ya wafanyabiashara wa aina hiyo. Wakati huo huo narudia kuwataka wafanyabiashara watoe ushirikiano unaostahili kwa maslahi ya wateja wao na taifa kwa jumla. Aidha, nazitaka mamlaka husika kutokuchelewa wala kuchelea kuchukua hatua zipasazo kwa wafanyabiashara wakaidi.
Ndugu Wananchi;
Kutetereka kwa mfumo wa fedha wa kimataifa na kuanguka kwa masoko ya hisa katika mataifa yaliyoendelea kumesababisha uchumi wa nchi hizo kudhoofika. Hali hiyo imekuwa na athari za namna na viwango mbalimbali kwa uchumi wa nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Nilikwishalieleza siku za nyuma na napenda kurudia kusema kuwa sekta ya fedha hapa nchini bado ni tulivu. Haijaathiriwa na misukusuko inayoikumba sekta ya fedha ya kimataifa. Zipo sababu kuu mbili.
Kwanza, kwamba, sekta yetu ya fedha na soko la mitaji havijaunganishwa na mfumo wa fedha wa kimataifa na masoko ya hisa ya kimataifa. Hivyo basi, hakuna athari za moja kwa moja zinazotukuta hapa nchini kwa sasa.
Pili, kuna usimamizi mzuri wa soko na sekta ya fedha unaofanywa na Benki Kuu. Mpaka sasa, juhudi hizo za Benki Kuu zimesaidia. Hata hivyo, tunatambua haja na hoja ya kuendelea kuwa makini. Inaelekea matatizo ya mfumo wa fedha na uchumi katika nchi zilizoendelea yatachukua muda mrefu kutengemaa. Hatujui siku za usoni mambo ya yatakuwaje.
Serikali itaendelea kushirikiana na Benki Kuu kuzuia athari za soko la fedha duniani zisitufikie au kama zitatufikia, basi makali yake yawe nafuu. Kwa sasa mfumo wa ufuatiliaji (surveilance) na ule wa kutoa tahadhari ya mapema (early warning system) vinafanya kazi ipasavyo. Tuko tayari kuchukua hatua zaidi kama hapana budi.
Ndugu Wananchi;
Athari za hiyo Tsunami ya uchumi wa dunia, kama ilivyoitwa na baadhi ya watu, kwa uchumi wetu tumeanza kuziona kwa baadhi ya sekta. Tuchukue kwa mfano, sekta ya utalii. Katika mapumziko yangu ya mwisho wa mwaka huu nilitembelea mbuga zetu za hifadhi ya wanyama za Tarangire, Ziwa Manyara, Ngorongoro na Serengeti ya Kusini. Katika mazungumzo yangu na viongozi wa hoteli, hifadhi hizo na wale wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) nimeelezwa jinsi idadi ya watalii ilivyopungua na mapato yao kushuka kwa kati ya asilimia 7 na 18.
Aidha, nimezungumza na baadhi ya wamiliki wa viwanda vya kuchambua pamba na viongozi wa Bodi ya Pamba. Wote wamenieleza tabu wanayoipata ya kuuza pamba yao nje. Pia wanaelezea jinsi bei ya pamba ilivyoshuka katika soko la dunia. Katika kipindi cha mwezi Machi hadi Julai, 2008 bei ya pamba ilikuwa senti 82 za dola za Kimarekani kwa paundi na kushuka hadi senti 45 kwa paundi kwa sasa.
Hali kwa zao la kahawa nayo siyo nzuri. Nimeambiwa kuwa kati ya mwezi Agosti, msimu wa kahawa ulipoanza, na tarehe 18 Disemba 2008, bei ya kahawa ya Arabica kwenye soko la dunia, imeshuka kutoka dola za Kimarekani 158 hadi 104 kwa gunia la kilo 50. Hii ni sawa na anguko la asilimia 34. Katika kipindi hicho hicho, bei ya kahawa ya robusta imeshuka kutoka wastani wa dola za Kimarekani 93.6 hadi dola 65.46 kwa gunia la kilo 50. Hii ni sawa na anguko la asilimia 30.
Ndugu Wananchi;
Hata kwa mazao mengine nayo kwa jumla, hali ni hiyo hiyo ya kupungua kwa mauzo nje na kushuka kwa bei. Matatizo tunayoyapata sisi kwa mazao yetu ndiyo yaliyoikuta bidhaa ya mafuta. Kwa sababu ya uchumi kutetereka katika nchi za Marekani, Ulaya Magharibi, Japan, China na India mahitaji ya mafuta yamepungua na bei ya mafuta imeanguka kupita kiasi.
Ndugu Wananchi;
Kupungua kwa mauzo nje na bei ya bidhaa zetu pamoja na kupungua kwa watalii kuna athari kwa uchumi wa nchi yetu. Mapato yetu ya fedha za kigeni yatapungua jambo ambalo litapunguza akiba yetu ya fedha za kigeni, hivyo kuathiri uwezo wetu wa kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje. Aidha, mapato ya Serikali kwa kodi zitokanazo na mauzo hayo yatapungua, hivyo kuathiri uwezo wa Serikali wa kutimiza majukumu yake ya kiutawala na kiuchumi. Isitoshe ajira chache zilizopo katika sekta husika zitapungua na kusababisha watu hao kuwa na hali mbaya kiuchumi.
Ndugu Wananchi;
Hali mbaya ya uchumi wa dunia inasababisha uwekezaji wa kutoka nje nao kuathirika. Baadhi ya wawekezaji walioonyesha nia ya kuwekeza nchini wameahirisha nia yao. Ukiacha hofu inayotokana na hali mbaya ya uchumi wa dunia, wengine wamekuwa wanapata ugumu wa kupata mikopo kutoka katika mabenki. Mabenki yamekuwa yanasita kukopesha na pale yanapokopesha masharti yake huwa magumu kiasi cha kuwakatisha tamaa wakopaji.
Ndugu Wananchi;
Nimezitaja baadhi tu ya athari za kuyumba kwa uchumi wa dunia kwa uchumi wa nchi yetu ili tutambue kuwa tupo kwenye mazingira magumu na hali ya baadae ni ya mashaka. Tunaweza kunusurika kwenye eneo moja lakini tukaathirika kwenye maeneo mengine kwa sababu uchumi wetu ni uchumi wa dunia ya utandawazi. Kutokana na athari hizo inakadiriwa kuwa hatutafikia malengo yetu ya kukua kwa uchumi mwaka huu 2008 na hata mwaka ujao wa 2009. Inakadiriwa kuwa uchumi utakua kwa asilimia 7.7 badala ya 7.8 mwaka huu na mwakani utakua kwa asilimia 7.3 badala ya asilimia 8 iliyokadiriwa.
Ndugu zangu;
Watanzania wenzangu;
Napenda sote tutambue kuwa kuna kila dalili kuwa mwaka 2009 huenda tutatumia muda mwingi na nguvu nyingi kukabili athari za machafuko ya uchumi wa dunia. Kwa ajili hiyo, hatuna budi kutambua hivyo mapema na kuwa tayari kusimama kidete kukabiliana na athari zake. Sisi katika Serikali tunafuatilia kwa karibu hali inavyoendelea duniani na hapa nchini na kuamua hatua za kuchukua. Tutaendelea kupashana habari. Maombi yangu kwenu wananchi wenzangu ni uelewa wenu na ushirikiano wenu. Umoja, mshikamano na ushirikiano wetu wakati huu ndivyo vitakavyotukinga na kutuvusha katika tatizo hili kubwa.
Ndugu Wananchi;
Yapo mambo kadhaa ambayo hatuna budi kufanya katika kukabiliana na hali hii tete hapa nchini. Miongoni mwa hayo lipo suala la kujenga uwezo wa ndani wa kujitegemea kwa mambo fulani fulani kama vile chakula na bidhaa muhimu kwa matumizi ya watu. Pili, linalolingana na hilo, ni suala la kukuza utalii wa ndani na kutafuta vyanzo vipya vya watalii kama vile Mashariki ya Kati na Asia. Tatu, kukuza masoko ya ndani kwa bidhaa zetu na masoko ya kanda kama vile SADC na EAC. Wakati mwigine tunahangaikia masoko ya mbali wakati soko lipo hapa ndani au nchi jirani.
Ndugu Wananchi;
Kwangu mimi kauli mbiu muafaka kwa mwaka 2009 ni “Mwaka wa Kuhami na Kukuza Uchumi wa Taifa”. Bahati nzuri kauli mbiu hii inawiana na mpango wangu wa kazi nilipoingia madarakani. Nilikuwa nimepanga kuwa, katika nusu ya kwanza ya kipindi changu cha uongozi tuelekeze nguvu zetu katika upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii, na nusu ya pili tushughulikie kukuza uchumi. Nafurahi kwamba, tumefanikiwa kuweka misingi madhubuti ya kisera na mipango ya uhakika ya utekelezaji kuhusu elimu, afya, barabara, maji na umeme vijijini. Utekelezaji wake unaendelea na changamoto yetu kubwa ni upatikanaji wa fedha za kutosha kutekeleza malengo tuliyojiwekea.
Nashukuru kwamba ufanisi mkubwa tulioupata katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na misaada ya washirika wetu wa maendeleo tumeweza kupata mafanikio tuliyoyapata mpaka sasa. Hata hivyo mahitaji ya rasilimali bado ni makubwa. Ni wajibu wetu kuendelea kutafuta.
Ndugu Wananchi;
Kuanzia mwaka 2009 Serikali itaelekeza nguvu katika kukuza uchumi wa nchi kwa lengo la kuongeza mapato ya nchi na wananchi wake. Bahati mbaya au nzuri yanayotokea sasa duniani yanasisitiza haja na hoja ya kufanya hivyo. Pia, yameongeza jambo jipya la kufanya, nalo ni la kuhami uchumi usitetereke.
Kilimo Kipaumbele cha Kwanza
Ndugu Wananchi;
Katika agenda yetu ya kukuza uchumi, kilimo kimepewa kipaumbele cha kwanza. Tunafanya hivyo kwa sababu nzuri na za msingi kabisa. Kwanza, tunataka kuhakikisha kuwa tunajitosheleza kwa chakula na tunakuwa na ziada ya kutosha. Katika mazingira ya sasa ambapo bei za vyakula duniani ziko juu, kuwa na upungufu wa chakula na kulazimika kuagiza kutoka nje kutazua matatizo makubwa nchini. Mfumuko wa bei utatushinda kuudhibiti.
Pili, kilimo kitatupatia malighafi ya viwanda vya kusindika mazao ya kilimo na kuzalisha bidhaa kamili zinazotokana na mazao ya kilimo. Kuendeleza viwanda vya aina hii ni kipaumbele chetu cha pili katika agenda yetu ya kukuza uchumi wa taifa. Lazima tuanze safari ya kuuza nje mazao ya kilimo yakiwa yameongezewa thamani kuliko kuyauza yakiwa ghafi kama tufanyavyo sasa. Tutafanya kila liwezekanalo kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ili kufanikisha azma yetu hiyo.
Tatu, kilimo ni chanzo kikubwa cha mapato ya fedha za kigeni kwa nchi, mapato ya serikali kupitia kodi na ni tegemeo la watu wengi nchini kwa uhai wao. Asilimia 8.5 ya fedha za kigeni hutokana na mazao ya kilimo na asilimia 80 ya Watanzania wanaishi vijijini ambapo kilimo ndiyo shughuli yao kuu ya kuwapatia mapato na maisha yao.
Hali ya Chakula
Ndugu Wananchi;
Hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni nzuri kwa miaka miwili mfululizo sasa, yaani 2007 na 2008, na tumekuwa tunapata ziada ingawaje ni kidogo. Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna tishio la njaa nchini. Hata yale maeneo ambayo yamekuwa yanapata upungufu wa chakula tumeweza kuyahudumia kwa kutumia ziada hiyo na akiba kutoka katika Hifadhi ya Taifa ya Chakula (SGR).
Kwa mfano, tathmini iliyofanywa mwezi Septemba, 2008 inaonyesha kuwa watu 240,544 katika Wilaya 20 nchini watakabiliwa na upungufu wa chakula kati ya Desemba, 2008 na Januari, 2009. Watu hao watahitaji tani 7,182 za chakula ambacho tayari kimekwishatengwa kutoka Hifadhi ya Taifa ya Chakula. Hifadhi hiyo sasa ina akiba ya tani 127,420.
Ndugu Wananchi;
Mvua za vuli hazikuwa nzuri kwa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Lakini, zimekuwa nzuri kwa mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara. Hivyo basi mavuno ya vuli hayatakuwa mazuri katika mikoa iliyoathirika. Hali hiyo inaweza kuongeza iadi ya watu watakaohitaji msaada wa chakula. Hata hivyo, hakuna shaka yoyote tutaweza kuwahudumia. Matumaini yetu na sala zetu kwa mikoa hiyo ni kuwa mvua za masika zitakuwa nzuri. Ikiwa hivyo mzigo utapungua. Bahati nzuri mikoa mingine inayopata mvua moja hali ya mvua ni nzuri, hivyo inatutoa hofu ya upungufu mkubwa wa chakula nchini. Tuzidi kumuomba Mungu mvua zinyeshe kama kawaida katika mikoa hiyo nayo.
Ndugu Wananchi;
Dhamira yetu katika kuelekeza nguvu zetu katika kuendeleza kilimo ni kuongeza tija. Bahati mbaya kwa sasa tija iko chini sana jambo linaloelezea hofu za upungufu wa chakula, mazao ya biashara na hali duni ya maisha kwa wakulima wengi.
Kwa ajili hiyo Serikali imekusudia mwaka 2009 kutilia mkazo mambo matano:
a. Upatikanaji na matumizi ya mbegu bora;
b. Upatikanaji na matumizi ya mbolea;
c. Upatikanaji wa maafisa ugani;
d. Uendelezaji wa kilimo cha umwagiliaji pale inapowezekana; na
e. Upatikanaji na uimarishaji wa masoko ya mazao ya wakulima.
Ndugu Wananchi;
Mambo yote hayo na mengine ambayo sikuyataja si mapya. Tumekuwa tunayatekeleza katika miradi na programu mbalimbali za kuendeleza kilimo nchini kama vile DADP’s, PADEP na ASDP. Tunachokusudia kufanya mwaka ujao ni kutoa msukumo maalum wa kuendeleza kilimo kama tulivyofanya kwenye elimu na tunavyokusudia kufanya kwa upande wa afya.
Kuhusu upatikanaji wa mbegu, tumepanga kuimarisha vituo vyetu vya utafiti wa mbegu na kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha mbegu hapa nchini. Kwa ajili hiyo nimewaagiza Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Magereza watumie sehemu ya mashamba yao kuzalisha mbegu.
Nafuraji kwamba viongozi wa idara zetu hizo tayari wameshaelewana na wenzao wa Wakala wa Mbegu nchini kufanikisha mpango huo muhimu. Kwa upande wa mbolea nafurahi kusema kuwa kauli yangu niliyotoa Bungeni tarehe 21 Agosti, 2008 kuhusu pesa za EPA imeshaanza kutekelezwa. Shilingi bilioni 30 zimetengwa kwa ajili ya mbolea ya ruzuku na bilioni 10 kwa ajili ya madawa ya mimea. Madawa ya mifugo yametengewa shilingi bilioni 10 na mikopo ya kilimo TIB shilingi bilioni 10.
Ndugu Wananchi;
Nafurahi pia kuwa dhamira yetu ya kuzalisha mbolea hapa nchini inatekelezwa vizuri. Kiwanda cha kuzalisha mbolea ya phosphate pale Minjingu, mkoani Manyara kimekamilika na kimeshaanza kazi. Wakati huo huo mchakato wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea ya NPK hapo Minjingu umeshaanza. Aidha, uamuzi wetu wa kujenga kiwanda cha mbolea ya urea na ammonia kule Mtwara umefikia hatua nzuri. Kampuni ya kuwekeza imekwishapatikana na shughuli za mchakato wa ujenzi wa kiwanda hicho ziko mbioni.
Hatua hizi zote zitakapokamilika, ndani ya miaka miwili ijayo, zitaiwezesha nchi yetu kuwa moja ya wazalishaji wakubwa wa mbolea katika kanda yetu ya SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tutatosheleza mahitaji yetu na kuwa na ziada ya kuuza kwa wengine nchi za nje na kujipatia fedha za kigeni.
Mifugo
Ndugu Wananchi;
Juhudi za kuongeza tija katika kilimo zitaelekezwa pia kwenye mifugo. Nia yetu ni kuboresha ufugaji wetu ili tupate mifugo inayotoa nyama nyingi, maziwa mengi na ngozi zilizo bora. Juhudi hizo zitajumuisha kuboresha aina ya mifugo yetu kwa kutumia madume bora na uhamilishaji. Pia itahusisha upatikanaji wa huduma za kinga na tiba ya mifugo, majosho, malisho, maji, masoko ya mifugo na mazao ya mifugo. Suala la kuwa na viwanda vya kusindika mazao ya mifugo nalo tutalipa uzito unaostahili.
Uwekezaji
Ndugu Wananchi,
Katika mwaka 2009, tutaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi wa ndani na nje kuja kuwekeza nchini. Sifurahishwi na taarifa nizipatazo kuwa mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara nchini bado hayajaboreka vya kutosha. Na, linalonisumbua zaidi ni kule kuanza kujengeka dhana kuwa Tanzania inaanza kupoteza sifa ya mahali rafiki kwa wawekezaji. Hii si dalili nzuri, lazima tuibadili haraka iwezekanavyo.
Ndugu Zangu;
Dunia nzima hata mataifa tajiri yanavutia wawekezaji seuze siye maskini? Uwekezaji ndiyo chachu ya kukua kwa uchumi. Bila ya uwekezaji uchumi haukui. Wote tunaowasifia kufanikiwa kiuchumi ni kutokana na uwekezaji. Hata China imeendelezwa na uwekezaji tena kutoka mataifa ya kibepari.
Tutayaainisha mambo yanayotufikisha hapo na kuyatafutia majawabu. Natambua kuwepo malalamiko kuhusu usumbufu na urasimu mkubwa katika kuwahudumia wawekezaji. Mlolongo na muda wa uamuzi ni mrefu, kuna usumbufu upande wa kodi na tuhuma za vitendo vya rushwa zinasikika. Wakati mwingine kauli za wanasiasa wetu zimekuwa zinawaogopesha wawekezaji. Yote haya na mengineyo ni mambo ambayo yapo kwenye uwezo wetu kuyarekebisha.
Tumedhamiria kuyakabili kwa dhati matatizo hayo ili tuifanye Tanzania kuwa nchi nzuri kuwekeza. Pamoja na kusimamia kwa karibu mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Tanzania (BEST), nakusudia kuanzisha kitengo maalum cha kusikiliza malalamiko ya wawekezaji na kuyatafutia ufumbuzi (Investors Complaints Bureau). Kitengo hicho kitakuwa chini ya Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi na kazi yake itakuwa ni kutatua kwa haraka malalamiko ya wawekezaji.
Mikopo ya Wajasiriamali Wadogo na SACCOS
Ndugu Wananchi,
Miaka miwili iliyopita tulianzisha mpango wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo ambao hawana sifa za kukopesheka katika mabenki kwa utaratibu wa kawaida. Tumefanya hivyo ili wanyonge nao wapate fursa ya kujiendeleza na kujikwamua. Kama tujuavyo, tulitenga shilingi bilioni moja kwa kila mkoa wa Tanzania Bara na shilingi milioni 100 kwa kila mkoa kwa mikoa minne ya Zanzibar na milioni 200 kwa mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja. Tulikubaliana kuwa mikopo hiyo itatolewa na Benki za CRDB na NMB na asasi ndogo za fedha kama vile Benki ya Posta, PRIDE, SELF n.k.
Taarifa zinaonyesha kuwa hadi Novemba 30, 2008 jumla ya shilingi bilioni 39 zimekopeshwa na NMB (16.1bn/=) na CRDB (22.9bn/=) na watu 48,339 wamenufaika pamoja na SACCOS 192 na vikundi 137. Benki na asasi nyingine 12 zimeshakopesha SACCOS 236 na shilingi 4.6 bilioni zimetumika katika wilaya 46 za Tanzania Bara.
Katika ziara zangu katika mikoa ya Bara nimepokea malalamiko ya watu kuhusu upatikanaji wa mikopo hiyo. Moja ya jambo nililojifunza ni kuwa, mahitaji ya mikopo ni makubwa na fedha zilizotolewa ni kidogo. Jawabu lake ni kuongeza fedha, jambo ambalo tuko tayari kufanya.
Jambo la pili nililojifunza ni kuwa fedha zilizolipwa na wakopaji wa awali hazijazungushwa. Jawabu lake ni kuzizungusha ili wengine nao wakope. Tunazungumza na mabenki juu ya jambo hilo. Ni dhamira yangu mwaka ujao wa 2009 tufanye tathmini ya kina ya mpango huu ili tubaini mapungufu yake na mbinu za kuyarekebisha ili tuongeze fedha na kunufaisha watu wengi zaidi wa kipato cha chini wainue hali zao za maisha.
Kwa nia ile ile ya kuwasaidia watu wasiokuwa na sifa za kukopesheka moja kwa moja na mabenki wapate mitaji ya kufanyia shughuli zao za kujipatia kipato, tuliwahimiza wananchi waanzishe Vyama vya Kuweka na Kukopa. Tulipoingia madarakani kulikuwa na SACCOS 1,875 na sasa zipo 4,780 kutokana na msukumo maalum tulioutoa kwa uanzishwaji wake.
Fedha nyingi za akiba zimewekwa na wanachama wa SACCOS hizo na mikopo mingi imetolewa kwa wanachama hao. Aidha, SACCOS kadhaa zimeweza kupata mikopo ya kawaida ya mabenki na kupitia mikopo ya wajasiriamali wadogo wadogo.
Pamoja na kujenga utamaduni mzuri wa watu kuweka akiba, SACCOS zimekuwa nyenzo muhimu ya kukuza uchumi na vyombo vya kutumainiwa na wananchi wa kawaida katika harakati zao dhidi ya umaskini. Napenda kuahidi kuwa ni makusudio yetu kuendeleza juhudi za kuimarisha na kuanzisha SACCOS nchini.
Huduma za Kiuchumi na Kijamii
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka ujao tutaendeleza jitihada za kuongeza na kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kiuchumi na kijamii hususan elimu, afya, maji, umeme na barabara. Kazi kubwa imefanyika na watu wengi sasa wanapata huduma hizo, lakini bado hazijatosheleza mahitaji na viwango vya ubora.
Tunatambua wajibu wa Serikali wa kuongeza fedha katika bajeti za sekta hizo ili miradi mingi zaidi itekelezwe na kukidhi mahitaji ya wananchi. Hiyo ndiyo dhamira yetu kufanya katika mwaka 2009 na miaka ijayo. Sekta ya maji na umeme vijijini tutazipa kipaumbele stahiki.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa elimu ya sekondari napenda kwa mara nyingine tena kuwashukuru na kuwapongeza sana wananchi kwa moyo wao wa kujitolea na kujituma. Moyo wao huo na ushirikiano wao na Serikali ndiyo siri iliyotufanya tuendelee kupata mafanikio makubwa katika upanuzi wa elimu ya sekondari nchini.
Hivi sasa, nchini tunazo sekondari za Serikali 3,039 kutoka 1,202 mwaka 2005 na idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,222,403 mwaka huu. Haya si mafanikio madogo katika kipindi kifupi hivi.
Naomba moyo huo wa kujitolea na ushirikiano viendelee kwa manufaa ya watoto wetu na wajukuu wetu waliopo sasa na wajao. Sisi katika Serikali tunaahidi kuendelea kutimiza wajibu wetu katika ushirikiano wetu huo. Tutaendelea kukabili changamoto za upatikanaji wa walimu, vitabu, vifaa vya kufundishia, maabara na nyumba za walimu. Tunatambua kuwa ni mzigo mkubwa lakini hatuna budi kuubeba kwa maslahi ya taifa letu.
Matokeo ya Darasa la Saba
Ndugu Wananchi;
Kwa miaka miwili mfululizo matokeo ya mitihani ya darasa la saba yamekuwa si mazuri. Mwaka wa jana kiwango cha kufaulu kilikuwa asilimia 54.2 na mwaka huu ni asilimia 51.2. Hali hii si nzuri na hatuwezi kuacha iendelee. Hatuna budi kujiuliza kulikoni na kutafuta majawabu muafaka. Nimeiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kasoro zilizopo na kupendekeza hatua za kuchukua. Aidha, nimemuagiza Waziri Mkuu kulisimamia suala hili kwa ukamilifu.
Barabara
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka huu tunaoumaliza leo, tuliendelea kutoa kipaumbele cha juu kwa sekta ya miundombinu. Tumeongeza bajeti ya miundombinu na sasa ni ya pili kwa ukubwa baada ya elimu. Kiasi cha shilingi bilioni 973.3 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu nchini katika mwaka wa fedha 2008/09. Tumeendelea kujenga barabara mpya za lami, za changarawe na za udongo. Pia tumekarabati na kuimarisha barabara zilizopo.
Lengo letu la kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa yote kwa barabara za lami sasa lina muelekeo mzuri. Mipango kwa kuunganisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Rukwa na Ruvuma imefikia mahali pazuri. Hivi sasa nguvu zetu tunazielekeza kwa mikoa ya Kigoma na Tabora ambapo naamini mpaka katikati ya mwaka 2009 sura kamili inaweza kuwa imejitokeza. Nafurahi hata hivyo kwamba, taratibu za ujenzi wa daraja la Mto Malagarasi zimefikia hatua za mwisho.
Tunasikitika kwamba misukosuko ya mfumo wa fedha wa kimataifa umetulazimisha kuahirisha kutekeleza mpango wetu wa kupata fedha kwa kutumia hati fungani (soverign bounds) kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara zetu kuu nyingi hapa nchini. Ni matumaini yetu kuwa hali ikitengemaa tutautazama upya mpango huo.
Bandari, Reli na ATCL
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2009 tutaendelea kufuatilia na kusimamia kwa karibu hali katika mashirika ya reli, bandari na shirika la ndege. Hali ya huduma hizo muhimu hairidhishi hata kidogo. Yapo matatizo ya uendeshaji ambayo yamesababisha huduma zitolewazo kuwa za kiwango kisichoridhisha. Tutafanya kila tuwezavyo kurekebisha mambo ili huduma hizo ziboreke na kuwafanya watumiaji kufurahi.
Mapato ya Serikali
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada mwaka ujao tutaendeleza juhudi za kuhakikisha kuwa mapato ya Serikali yanaendelea kuongezeka. Tutaendelea kuimarisha Mamlaka ya Mapato na kuziba mianya inayopoteza mapato ya Serikali.
Napenda kutumia nafasi hii, kuwapongeza sana viongozi na watumishi wa TRA kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kukusanya mapato ya Serikali. Pamoja na matatizo ya hapa na pale hali ya mapato ya Serikali imeimarika.
Mara mbili katika mwaka huu wamevunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Mara ya kwanza ilikuwa mwezi wa Juni walipokusanya shilingi 346.7 bilioni na mara ya pili ilikuwa mwezi wa Septemba walipokusanya shilingi 420.8 bilioni. Tunatambua na kuthamini juhudi zao na nakusudia kuwatunza kwa mafanikio hayo mwishoni mwa mwaka huu wa fedha.
Nidhamu ya Matumizi
Ndugu Wananchi;
Sambamba na juhudi za kuongeza na kuimarisha mapato ya Serikali hatuna budi kuhakikisha kuwa kunakuwepo na nidhamu na uaminifu katika matumizi ya fedha na rasilimali za Serikali. Nimelisisitiza sana jambo hili na kuwataka viongozi wenzangu na watumishi wa Serikali kusoma na kuzingatia maoni na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yaliyomo katika taarifa zake za kila mwaka.
Nimeagiza Viongozi na Watendaji Wakuu wa Wizara, Idara, Mikoa, Wilaya na Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sheria ya Fedha na mali za Serikali na Kanuni zake. Kuna dalili za mabadiliko chanya, lakini hali bado si ya kiwango cha kutufanya tufurahi sana. Mwaka ujao tutaendelea kubanana katika jambo hili ili tufikie ufanisi unaotakiwa.
Ndugu Wananchi;
Kuanzia mwaka ujao nitawaomba wakaguzi wa mahesabu ya Serikali kumkabidhi kwenye vyombo vya sheria mtumishi wa Serikali aliyehusika na wizi au ubadhirifu mara watakapougundua. Najua utaratibu wa sasa hauko hivyo. Nataka tuutazame upya utaratibu wetu wa sasa ili isaidie kujenga nidhamu hata kama ni ya woga wa kufungwa. Itasaidia kunusuru fedha nyingi za umma zinazotumiwa isivyo.
Ni matumaini yangu pia kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ataendeleza kwa kasi na nguvu zaidi kazi waliyoianza ya ukaguzi wa thamani ya fedha zilizotumiwa na kulinganisha na kazi iliyofanyika (value for money audit). Ukaguzi wa asili umekuwa unahusu uandishi wa vitabu kwa mujibu wa kanuni za fedha. Lakini, inawezekana kabisa vitabu vya hesabu vikaandikwa vizuri lakini pesa zikatumika vibaya au hata kuibiwa. Tunataka ulinganifu sawia wa fedha zilizotumika na kazi iliyofanywa.
Ndugu Wananchi;
Nimewaelekeza wenzetu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufanya kazi kwa karibu na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kusaidia kupambana na wasiozingatia nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma hususan wezi na wabadhirifu wa fedha za umma.
Bahati nzuri Sheria ya Mwaka 2007 iliyounda PCCB mpya imetoa mamlaka ya kufanya hivyo. Nimewataka wawe wakali kwa wala rushwa kama wafanyavyo sasa, lakini pia wawe wakali kwa wale wote wanaokiuka kanuni za fedha za Serikali. Vitendo hivyo siyo tu vinaitia hasara Serikali bali pia vinapunguza uwezo wa Serikali kuwahudumia wananchi walioiweka madarakani.
Nimewataka waitumie vyema sheria mpya na fursa waliyonayo ya kuwaongezea uwezo wa rasilimali tuliyowapa kwa kutumiza ipasavyo wajibu wao. Nimewasihi pia kwamba katika kufanya hivyo wasionee wala kupendelea watu bali watende haki.
Ulinzi na Usalama
Ndugu Wananchi,
Tunaumaliza mwaka wa 2008 hali ya ulinzi na usalama wa nchi ikiwa ya kuridhisha. Mipaka ya nchi yetu ni salama na nchi ni tulivu. Hatuna budi kutoa pongeza maalum kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyoifanya na wanayoendelea kuifanya. Uhalifu wa makosa makubwa ya jinai kama vile mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha na unyang’anyi wa kutumia nguvu umepungua.
Taarifa za Januari hadi Novemba, 2008 zinaonyesha kuwa kulikuwa na matukio ya aina hiyo 8,330 ukilinganisha na matukio 10,381 katika kipindi kama hicho mwaka 2007. Huu ni ushahidi kuwa Polisi wanafanikiwa kudhibiti uhalifu, hata hivyo bado juhudi ziongezwe ili matukio ya uhalifu yapungue zaidi. Nafurahi pia kwamba hata ajali za barabarani zimepungua mwaka huu ukilinganisha na mwaka wa jana.
Mwaka wa jana kulitokea ajali 16,196 kati ya Januari na Novemba, wakati mwaka huu zimetokea ajali 5,500. Hata idadi ya watu waliopoteza maisha imepungua kutoka 2,757 mwaka 2007 hadi 1,270 mwaka huu.
Ndugu Wananchi;
Wakati tunawapongeza wadau na Jeshi la Polisi kwa maendeleo hayo bado naamini kuwa ajali za barabarani pamoja na idadi ya watu wanaopoteza maisha au kujeruhiwa na mali kuharibiwa vinaweza kupungua zaidi. Ajali nyingi za barabarani husababishwa na makosa ya madereva kutokuheshimu sheria ya usalama barabarani.
Lakini, pia kuna mchango wa Jeshi la Polisi hasa wale wa usalama barabarani kutodhibiti ipasavyo madereva wazembe. Tatizo hili lipo kwenye uwezo wa Polisi na wadau kulidhibiti.
Madereva wakubali kuzingatia na kuheshimu sheria ya usalama barabarani. Wenye magari wahakikishe wanaajiri madereva wenye sifa nzuri. Aidha, madereva wa mabasi ya abiria watambue kuwa wanabeba binadamu wenzao ambao kwa kipindi chote cha safari usalama wao uko mikononi mwao.
Makosa madogo ya dereva yanaweza kuwapotezea watu uhai au kuwapa vilema vya maisha. Lazima watambue umuhimu wa wao kuwa waangalifu. Polisi nao lazima watimize ipasavyo wajibu wao.
Polisi lazima wawe wakali kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa. Naamini Polisi wakiwa wakali tofauti itaonekana.
Mauaji ya Albino
Ndugu Wananchi;
Suala la mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, yaani albino nimekwishalisemea mara mbili tatu mwaka huu, na mara ya mwisho wakati wa Baraza la Idd tarehe 8 Desemba, 2008. Ni mauaji na mateso ambayo hayana sababu ya kutokea kwa sababu chanzo chake ni cha kipuuzi. Imani kwamba kiungo cha albino kinampa mtu utajiri ni jambo la kijinga. Nirudie kuwasihi wenzetu hawa wanaotafuta utajiri wa haraka haraka kuwa juhudi na maarifa yao ndiyo siri ya kufanikiwa kwao na si vinginevyo. Lakini, kwa vile wapo watu wanaoamini kuwa wakipata viungo vya albino watatajirika na wapo waganga na wauwaji, Serikali haina budi kuchukua hatua za kuwabana watu wote hao na kulitokomeza kabisa tatizo hili.
Tumeunda kikosi-kazi kinachojumuisha Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa cha kuendesha mapambano haya. Hivi sasa wanaendelea na uchunguzi wa kina nchi nzima kuwatambua wahalifu na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria. Mpaka sasa watu 91 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani na mapambano yanaendelea.
Kwa nia ya kuongeza kasi na nguvu ya mapambano haya, mapema mwaka ujao tutaendesha zoezi la kura ya maoni nchi nzima. Tutawataka wananchi wawataje watu wanaowajua kuwa wanajihusisha na mauaji au kukata viungo vya albino. Wawataje waganga wanaohusika, wauawaji wa albino, wauzaji wa viungo vya albino na wafanyabiashara wanaotumia viungo hivyo.
Taarifa hizo zitasaidia kuwafuatilia na kuwakamata watu hawa waovu. Utaratibu kama huu ulitusaidia katika mapambano dhidi ya ujambazi nchini. Naamini utasaidia kwa hili. Tunafanya matayarisho ya zoezi hilo. Wakati utakapowadia watu wataarifiwa namna ya kushiriki. Naomba ushirikiano wa hali ya juu wa wananchi wakati huo. Jitokezeni kuwataja ili isaidie kukomesha aibu hii kwa taifa letu.
Hitimisho
Ndugu Wananchi,
Tunaumaliza mwaka nchi ikiwa na sifa kubwa katika medani ya kimataifa. Uhusiano wetu na mataifa yote duniani ni mzuri. Hatuna adui. Hali kadhalika uhusiano wetu na mashirika ya kimataifa ya kisiasa na kiuchumi ni mzuri.
Nchi yetu inaheshimika na kutumainiwa katika diplomasia ya kimataifa. Tumepokea wageni wengi mashuhuri na wengine ni wa kihistoria kama ziara ya siku nne ya Rais wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush. Tumekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa mwaka huu.
Pamoja na ugumu wake lakini tumeifanya kazi hiyo vizuri na yapo mambo kadhaa mazuri ambayo nchi yetu itakumbukwa nayo. Miongoni mwa hayo ni amani ya Kenya, kurejesha umoja wa taifa la Comoro, kuongoza vyema mijadala kuhusu masuala magumu kama yale ya uundaji wa Serikali ya Umoja wa Afrika na kuyafikisha mahali pazuri.
Mwaka 2009 nchi yetu itakabidhi uongozi wa Umoja wa Afrika kwa heshima na upendo mkubwa kutoka kwa wanachama wenzetu na mataifa mengine duniani.
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza mwaka nchi ikiwa tulivu. Hii inathibitisha kuwa nchi inaweza kuwa tulivu isipokuwa pale ambapo baadhi yetu tutakapokuwa tumeamua kuwa isiwe hivyo. Naomba mwaka 2009 uwe tofauti.
Tuache vitendo vya kuchochea ghasia kwa kisingizio chochote kile. Vitendo hivyo havitavumiliwa hata kidogo. Ni vizuri tukaambiana mapema tusije tukalaumiana. Naomba Watanzania wenzangu wote na hasa wanasiasa wenzangu tuyatambue hayo na tujiepushe nayo.
Naomba makundi ya kijamii yatambue ukweli huo na waache kuwaendekeza wanasiasa hasidi.
Ndugu Wananchi;
Naomba nimalize kwa kuwakushukuru kwa mara nyingine tena Watanzania wenzangu wote kwa ushirikiano wenu na uelewa wenu na msaada wenu kwangu na kwa wenzangu wote serikalini katika kipindi chote cha mwaka huu tunaouaga leo. Tumepita vipindi vya raha na vigumu kwa pamoja na tunaumaliza mwaka tukiwa wamoja na watu wenye mshikamano.
Naomba tuingie mwaka mpya na moyo huo na tuendelee hivyo.
Nitakuwa mtovu wa fadhila kama sitamshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na upendo wake na kutuvusha salama mwaka 2008. Tuzidi kumuomba atuongoze na kutuvusha salama mwaka ujao na miaka ijayo.
Mimi si Sheikh na wala si mwanazuoni, mimi na mfuasi tu. Lipo wazo nimekuwa napewa mara kadhaa kuwa pengine si vibaya kila mwishoni au mwanzoni mwa mwaka tungekuwa na siku ya maombi ya pamoja watu wote wote wa dini tukiongozwa na viongozi wa dini zetu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mwaka tulioumaliza na kuliombea taifa mema kwa mwaka unaofuata.
Ni wazo linalovutia wengi lakini sidhani kuwa ni ni jambo la kufanywa kwa amri ya Serikali. Nawaachia viongozi wa dini zetu watuongoze.
Naomba tutakiane heri na fanaka tele katika mwaka mpya, 2009.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Ahsanteni kwa kunisiliza.
No comments:
Post a Comment