Saturday, February 07, 2009


Jifunze aina sita za

marafiki wa kuepukwa




Marafiki mara nyingi ni wale watu ambao wengi tunafurahia kuwa nao. Wao tunawaamini na kuwakumbatia na kuwafanya kuwa ni sehemu ya maisha yetu. Tunajisikia furaha kuwaambia mambo yetu, siri zetu, mbinu zetu tunavyohisi, tunavyojisikia tukitegemea mambo mazuri kutoka kwao.

Na tunawategemea katika kupita kipindi kigumu cha maisha yetu pia. Tunategemea msaada wao na tunashirikia nao katika day to day activities. Tuko tayari kwa lolote juu yao na tunawafanya kuwa ni wenzetu. Lakini si kila rafiki anastahili hii takrima. Ukweli ni kwamba wapo pia katika kundi la marafiki, 'marafiki maadui' waliojivika ngozi ya urafiki. Upo hapo!

Karibu sana mpenzi wa makala haya, naoma kwanza nistop kuwasabahi popote mlipo nikiwa na imani kuwa Jumaamosi kama hii imekuja kwenu kwa amani. Binafsi sichoki kumshukuru Mungu kwa hizi neema alizonijaalia nazo.

Niko hapa leo shoga yenu kwa kile kinachosemekana kuwa ni urafiki wakati kumbe ni MADE IN CHINA (yaani Feki)

Shoga hii ni mada nyeti sana. Sio vibaya ukasoma hapa na ukampa rafiki yako.

Kwanza ya yote inakubidi ufahamu kuwa kuna hekima katika usemi usemao "...kaa mbali na maadui zako lakini chukua tahadhari na marafiki zako vilevile."

Halikadhalika, unaweza kuwa na marafiki wengi tu, lakini ni vyema ukachagua moja wa kukushauri. Na ushauri wa kupewaaa shosti...! changanya na wakwakooo.

Nafahamu fika kuwa kuchagua marafiki ni kazi ngumu sana hasa kutokana na ukweli kwamba hawa watu wote kwa picha ya nje ni marafiki. Na wanakuja kwako wakiwa wanapeperusha hii bendera ya urafiki.

Na kwa hakika, kupata rafiki mwaminifu ni sawa na kupata kinga imara. Na ukipata rafiki kama huyo amepata hazina. Naomba nichukue furasa hii kuwasabahi marafiki zangu popote mlipo. Sasa leo hapa nataka niwatambulishe kwenu marafiki sita wa kwaepuka:

1. Rafiki Mnafiki

Rafiki huyu unapofanikiwa atataka kila mtu ajue wewe ni rafiki yake, na unapo pata aibu atajitahidi sana kuonyesha kuwa hiyo ni aibu yako, hahusiki. Ukisemwa atachangia, akikuona atakusifia. Rafiki huyu ni mwepesi kuchukua ya kwako na kukuletea ya watu.

Anatamani mgombane akuadhiri. Yuko tayari akununie kuwafurahisha maadui zako. Kajisemea Mzee Yusuf; 'Two in One' ndo huyu sasa! - Mara ananuna mara anacheka. Huyu ni kama yule niliyesema hapo juu; si rafiki bali adui aliyejivika ngozi ya urafiki.

2. Rafiki Mnyonyaji

Huyu shosti ni rafiki unapomfaa, lakini siku ya taabu kwako kamwe hatokuwepo kukusaidia. Anakuita rafiki anapokuhitaji. Anakuwa mwema zaidi anapokuwa na shida, katika kipindi chako cha mafanikio urafiki wenu utanoga, ukifilisika atakugeuka. Hakusikilizi, anataka umsikilize.

Anakuwa rafiki yako pale anapohisi unaweza kumsaidia. Kwa lugha nyingine huyu mtu ni tegemezi. Atataka umfanyie hiki umfanyie hiki lakini yeye hayuko tayari kwa lolote juu yako. Atakutumia kwa manufaa yake binafsi lakini hayuko tayari kutumiwa na wewe.

3. Rafiki Msaliti

Rafiki huyu huwa anakuja kwako kuchunguza udhaifu wako. Atageuza mambo mema kuwa maovu na kuonyesha kosa katika matendo yako mema na huenda anafurahia mabaya yaliyokukuta huku akijifanya kukuhurumia, utaona vile anavyokuzungumza kwa watu.

Yuko tayari kukugeuka wakati wowote, Mbaya zaidi ni kwamba rafiki dizaini hii anaweza hata kuthubutu kukuchukulia mumeo. Ni hodari wa kupaka matope Ni msaliti kama ambavyo inajieleza, Hajali maumivu yako, Kinyume nyume anacheka unapoharibikiwa.

4. Rafiki Mbeya

Huyu ndimi zake zimejaa hujuma na laana. Huyu yupo tayari

kujipatia sifa kwa kukuteta kwa watu. Anadiriki kutoa aibu zako nje na kuficha za kwake.

Hawezi kufunga mdomo wake kuzungumza mambo yako. Katika kipindi fulani cha urafiki wenu bila shaka umegundua kuwa anakuletea sana mambo ya watu na kuyashadadia, atapeleka na ya kwako. Anaweza pia kusema mambo ya uongo kwania ya kukuhatarisha na wengine.

Rafiki dizaini hii ni mwepesi kukutangazia ubaya. Hawezi kuweka kitu moyoni, tena yuko tayari kupoteza urafiki wenu kutumia mdomo wake. Ukimwambia 'usiseme' ndio kama umemwambia 'kaseme' Hana kifua huyu mtu, loh.

5. Rafiki Mlaghai

Rafiki huyu ni mjuzi na hodari wa kushawishi, lakini mara nyingi ni kwa nia ya kukupotosha. Rafiki dizaini hii hana jema hata kidogo. Rafiki huyu ni mjanja, anawapata sana wajinga.

Atakufundisha mambo mabaya na kukufanya uamini ni mwenzie kumbe nia yake ni kukuharibia. Atakuasha pekee yako utakapoharibikiwa. Atakulaghai ili ajinufaishe yeye mwenyewe. Anakutumia kama ngao na huenda akawa anakuonea wivu. Rafiki huyu anaweza kukushauri ujinga, na kwa kua unamuamini akatumia nafasi hiyo kukupoteza.

6. Rafiki Mshindani

Huyu anakuwa na ushindani na ushindani wake zaidi si wa maendeleo bali kujifurahisha yeye mwenyewe kwa kukuangusha.Anatamani kazi yako, anatamani gari lako, anatamani amisha yako, anatamani viwe vyake. Atafanya kila njia akukwaze.

Kama ni kazini rafiki huyu atakuchongea.Na huenda akakutaja katika waovu. Hapendi maendeleo yako hata kidogo, anaweza akufiche kuhusu michongo ambayo anahisi itakufaidisha. Kila unachofanya na unachotaka kukifanya atajaribu kukirudisha nyuma ili yeye afanikiwe.

Hakutakii mema hata kidogo. Wewe kuharibikiwa hiyo ndiyo furaha yake. Kila ulichonacho atataka awenacho. Ataichukua kazi yako na Lazima atakuja kukuzunguuka. Anakuwa na wivu juu yako, anataka kila chako kiwe chake.

Haya shostito kazi kwako, mpaka wiki ijayo usikose kupitisha tena macho hapa. Kwa lolote Ni hayo tu.

Niandikie asmahamakau@mwananchi.co.tz


No comments: