Monday, February 09, 2009


ni lugha ya Afrika



na Padri Privatus Karugendo

KISWAHILI ni moja kati ya lugha nne za taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila, anaongea Kiswahili sanifu. Kwa vile rais wa nchi anaongea Kiswahili sanifu, hii itakuwa chachu ya kukiboresha Kiswahili cha DRC, na kukieneza kwenye nchi zinazoizunguka DRC, kwa upande wa kaskazini.

Kiswahili ni lugha ya taifa Tanzania, Uganda na Kenya. Ingawa Kiswahili si lugha ya taifa la Rwanda na Burundi, lakini vita ya Maziwa Makuu vimekifanya kiswahili kuzungumzwa karibu na watu wote wa Rwanda na Burundi. Mipango iko mbioni kukifundisha Kiswahili kwenye shule za msingi za Rwanda na Burundi. Msukumo huu unatokana na nchi hizi mbili kukubaliwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Kwenye miaka ya 1980, Kenya ilifanya jitihada nyingi kukiendeleza Kiswahili. Kiswahili lilifanywa somo la lazima kweye shule za sekondari. Matokeo yake yameanza kujitokeza miongoni mwa kizazi kipya cha Kenya, kwa kuongea Kiswahili sanifu kuliko kile Kiswahili cha kizazi cha miaka ya nyuma. Pia ongezeko la vyuo vikuu nchini Kenya vimeongeza ufanisi wa Kiswahili, kila mwaka zaidi ya vijana 2,000 wanaokifahamu vizuri kiswahili wanahitimu vyuo vikuu.

Hii itachangia kuwapata walimu wazuri wa kufundisha lugha ya kiswahili na wataalamu wazuri wa lugha ya Kiswahili. Ingawa magazeti ya Kiswahili hayajaongezeka kwa kasi kubwa, lakini uchapishaji wa vitabu vya Kiswahili uko juu zaidi nchini Kenya kuliko Tanzania. Kenya inatoa vitabu vingi vya Kiswahili na usambazaji wake ni mzuri kuliko wa Tanzania.

Pia Wakenya wanasoma vitabu kuzidi Watanzania. Bidii ya Kenya, katika kukikuza Kiswahili itachangia kwa kiasi kikubwa kueneza lugha hii katika nchi zinazopakana nayo upande wa kaskazini kama vile Somalia, Sudan na Ethiopia. Tukizingatia kwamba wakimbizi wengi kutoka katika nchi hizi wamekuwa wakiishi Kenya. Hizi ni dalili za kukipanua Kiswahili kuwa lugha ya Afrika nzima!

Tofauti na Tanzania, ambapo Kiswahili, karibu kinatumika kila sehemu katika jamii, Kenya Kiswahili kinatumika kama lugha ya siasa, dini na wasomi.Ingawa hii inaonyesha picha hali ya kukiendeleza Kiswahili katika jamii nzima ya Wakenya, lakini pia kwa njia hii Kiswahili kinaweza uongeza kasi ya kuongea lugha ya kisayansi na kiteknolojia na kujikita katika utandawazi kwa haraka zaidi ya Tanzania.

Kwenye miaka ya 1970, Idi Amin wa Uganda, alikitangaza Kiswahili kuwa lugha ya taifa ya Uganda. Lakini waganda na hasa ‘Baganda’ hawakukipokea Kiswahili kwa vile wanaipenda sana lugha yao ya ‘Luganda’. Sababu nyingine ni kwamba wanajeshi wa Amin walitumia Kiswahili kama lugha ya jeshi. Matendo maovu ya jeshi la Amin na mauaji yaliyofanywa na jeshi hilo yalikipaka matope Kiswahili na kuwafanya watu wa Uganda, kukichukie.

Pia Waganda walimchukulia mtu anayeongea Kiswahili kuwa ni ‘mswahili’ mjanjamjanja na mtu asiyeaminika. Lakini pia waganda wengine walikihusisha Kiswahili na Uislamu, maana Waislamu walikitumia kama lugha ya dini kwa kukichanganya Kiswahili na Kiarabu au kutafsiri Kiarabu katika Kiswahili.

Kwa nchi kama Uganda, ambayo imepitia migongano na michafuko mikubwa ya kidini, kujifunza Kiswahili ilikuwa ni sawa na kuamsha vita kati ya Wakristu na Waislamu.

Jeshi la Rais Yoweri Museveni na hata yeye mwenyewe walitumia Kiswahili. Hadi leo hii Kiswahili ni lugha ya jeshi la Uganda. Hii haikuwavutia Waganda waliokuwa wamechoka na utawala wa kijeshi. Hivyo Kiswahili ilibaki ni lugha ya jeshi na biashara ya magendo kati ya Uganda, Tanzania na Kenya.

Kwa sababu ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, ambayo Waganda wanaiona ina faida kubwa kuliko hasara, wameanza kuwa na hamu ya kujifunza Kiswahili. Serikali ya Uganda imepitisha kuanzia mwaka juzi Kiswahili ni somo la lazima katika shule za msingi na sekondari. Huu utakuwa ni msaada mkubwa wa kukikuza kiswahili na kukipatia picha ya kuwa lugha ya Afrika ya Mashariki na hatimaye Afrika nzima.

Vita vya ukombozi kusini mwa Afrika, vimekifanya Kiswahili isiwe lugha ngeni katika nchi za Zimbabwe, Namibia, Angola, Msumbiji na Afrika Kusini. Lakini pia wakimbizi wa Sudan, Somalia na Ethiopia walioishi Kenya na Uganda wamesaidia kukisambaza Kiswahili hadi kwenye nchi zao.

Wafanyabiasha wa Kisomali ambao hufanya kazi ya kusafirisha mizigo kwenye magari ya mizigo kwenye maeneo yote ya Afrika ya Mashariki, Kati na kusini wamekuwa mabalozi wa kuisambaza lugha ya Kiswahili.

Ingawa kuna lugha nyingine za Afrika zinazozungumzwa na watu wengi kama Kihausa, Kiswahili kinachomoza zaidi kwa sababu si lugha inayofungamana na kabila au taifa fulani. Mfano ni tofauti na Kihausa. Ingawa Kihausa kinazungumzwa na watu wengi wa Afrika ya Magharibi, kinafungamana na kabila kubwa la Wahausa ambalo limekuwa kwenye migogoro na mapigano na makabila mengine kwa muda wa miaka mingi. Lengo lolote la kutaka kukifanya Kihausa kuwa lugha ya Afrika nzima, ni lazima litaamsha chuki miongoni mwa makabila makubwa ya Afrika magharibi ambayo nayo yangependa lugha zao zichukue nafasi ya kwanza.

Profesa Mulokozi, kwenye mada yake: ‘Kiswahili as a National and International Language’ anaeleze kisa alichosimuliwa na Kanyama Chiume, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 2002; kwamba mwaka 1959, wapigania uhuru wa Afrika walikuwa na mkutano ulioitishwa na Sekou Toure, katika mji wa Conakry, Guinea, ili kupanga harakati za kudai uhuru. Mkutano huu ulihudhuriwa na watu kutoka nchi zilizokuwa zikiongea Kiingereza na Kifaransa. Tatizo kubwa lilojitokeza katika mkutano huo ni lugha ya kutumia. Wajumbe walikaa wakitafakari zaidi ya masaa mawili juu ya lugha ya kutumia katika mkutano huo ili wote waweze kusikilizana na kuchangia hoja.

Waliotoka kwenye nchi zilizokuwa zikiongea Kiingereza hawakufahamu Kifaransa na wale waliotoka kwenye nchi zilizokuwa zikiongea Kifaransa hakukifahamu Kiingereza. Huu ulikuwa mtindo wa wakoloni, wakutaka kufundisha lugha zaidi ya lugha yao. Baada ya muda mrefu wa kutafakari namna ya kuendesha kikao hicho kigumu, Kanyama Chiume, ndiye aliyeokoa jahazi.

Alipendekeza: Kwa vile yeye alifahamu Kiswahili na Kiingereza na Patrice Lumumba alifahamu Kiswahili na Kifaransa, mkutano ungeweza kuendelea kwa wajumbe waliokuwa wakitumia Kiingereza, kuongea kwa Kiingereza na Kanyama Chiume, kutafsiri yote kwa Kiswahili ili Patrice Lumumba aweze kutafsiri Kiswahili kwa Kifaransa.

Vilevile na wale wa upande wa kifaransa waliongea kwa Kifaransa na Patrice Lumumba alitafsiri kila kitu kwa kiswahili ili Kanyama Chiume, aweze kutafsiri kwa Kiingereza.

Kufuatana na maelezo ya Kanyama Chiume, mkutano huo uliendelea kwa ufanisi mkubwa ingawa ulikuwa wa kuchosha. Lakini wajumbe walielewana vizuri kwa msaada wa Lumumba na Kanyama Chiume waliokuwa wakikifahamu Kiswahili.

Ndiyo kusema Kiswahili kiliwaunganisha Waafrika katika mkutano huo. Na kama nilivyosema hapo juu, ni kwamba kiswahili ni tofauti na Kihausa au lugha nyingine maana si lugha ya Kabila fulani au taifa fulani.

Mfano katika mkutano huu wa Conakry wa mwaka 1959, Patrice Lumumba alitokea Congo na Kanyama Chiume alitokea Malawi! Kiswahili haikuwa lugha ya kabila la Lumumba na wala haikuwa lugha ya kabila la Kanyama Chiume. Tunaweza kusema kiswahili ilijitokeza kama lugha ya waafrika katika mkutano huo.

Huu ulikuwa ni mwanzo mzuri, kama si uvivu na kutojali kwa watu wanaojiita chimbuko la Kiswahili, kama vile watanzania, leo hii Kiswahili, kingekuwa kimepiga hatua kubwa katika Bara zima la Afrika na duniani kote.

Mfano mwingine anaotoa Profesa Mulokozi ni ule wa mwanapinduzi Che Guevara, wakati akiongoza harakati za mapambano ya vita vya msituni kuikomboa Congo, akiwa bega kwa bega na Laurent Kabila, alilazimika yeye na wapiganaji kutoka Cuba kujifunza Kiswahili hadi yeye Che Guevara, akabatizwa jina la kiswahili la Tatu!

Waligundua kwamba hii ndo lugha pekee iliyoweza kuwaunganisha Waafrika waliokuwa wakipigana msituni na kwamba adui aliyeongea Kiingereza na Kifaransa asingeweza kufuatilia nyendo zao katika mawasiliano. Che Guevara, ni mwanamapinduzi anaheshimika duniani kote na historia yake imejaa mvuto wa pekee na kati ya mvuto huu ni lugha ya Kiswahili!

Mkutano wa viongozi na wataalam wa Maziwa Makuu uliofanyika Aprili 2002 kwa kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere, ulitoa wito wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya mataifa ya maziwa makuu.

Katika miaka ya 1960 mwandishi maarufu wa Nigeria, Wole Soyinka, alitoa wito wa kukitangaza Kiswahili kuwa ni lugha ya Afrika nzima. Nigeria, kuna lugha kubwa za Kiafrika, lakini Wole Soyinka aliguswa na Kiswahili! Baadhi ya vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili.

Wito huu ulirudiwa tena na mwandishi mwingine wa Ghana, Ayi Kwei Armah, mnamo mwaka wa 1985, yeye alikiona kiswahili kama lugha ambayo inaweza kuingiza maneno mengi kutoka kwenye lugha nyingine za Kiafrika na kukifanya Kiswahili kuwa tajiri kwa msamiati.

Ayi Kwei Armah aliishi na kufanya kazi Tanzania. Alifundisha kwenye Chuo cha Walimu Chang’ombe. Kitabu chake ‘Te Beautiful Ones Are Not Yet Born’ kimetafsiriwa katika Kiswahili: ‘Wema Hawajazaliwa’.

Kwa vile utandawazi unatishia kuzimeza nchi za ulimwengu wa watu na hasa Afrika, kwa karibu kila kitu, ni vyema na Afrika itafute kitu cha kuuza kwenye utandawazi. Tukishindwa kuuza vitu vingine kama utamaduni, kazi za mikono na bongo zetu, basi tuuze lugha zetu na hasa zile zinazoelekea kukubalika Ulimwengu mzima kama vile Kiswahili.

Kutoka Tanzania Daima


No comments: