Saturday, February 28, 2009



Rais mstaafu wa Malawi

Bakili Muluzi ambaye ni

swahiba wa Rais

mstaafu wa Tanzania,

Benjamin Mkapa,

amepandishwa kizimbani.  


Rais Mstahafu wa Malawi, Alhaj Bakili Muluzi.


Na Usu-Emma Sindila, Malawi


Rais mstaafu wa Malawi Bakili Muluzi ambaye ni swahiba wa Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, amepandishwa kizimbani akikabiliwa na mashtaka kadhaa ya ubadhirifu wa fedha za umma na rushwa. 

Kabla ya tukio hilo, juzi Muluzi ambaye anagombea tena urais kupitia chama cha United Democratic Front (UDF), juzi 
alihojiwa na Taasisi ya Kuzuia Rushwa nchini hapa (ACB), kwa muda wa saa moja majira ya asubuhi kabla ya kukamatwa jana. 

Muluzi anakabiliwa na mashtaka 80, yakiwemo ya kujipatia fedha zilizotolewa na wafadhili, kiasi cha Kwacha bilioni 1.4 sawa na dola za Marekani milioni 11. 

Katika mfululizo huo, aliyekuwa msaidizi wake, Lyness Whiskey, naye amejumuishwa katika kesi hiyo, akidaiwa kumsaidia rais huyo mstaafu kufanikisha mipango yake hiyo ya ubadhirifu. 

Muluzi alihojiwa na ACB baada ya kupewa hati ya kuitwa iliyotolewa Jumatano iliyopita ambapo alitahadharishwa kwamba endapo angekaidi kufika kwenye mahojiano hayo angelikamatwa na kufunguliwa mashitaka. 

Hata hivyo, Muluzi aliachiwa kwa dhamana iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Blantyre, baada ya mawakili wake kupigana kufa na kupona. 

Muluzi anadaiwa kuchukua fedha hizo toka kwa wafadhili na kuzihamishia katika akaunti yake binafsi, ununuzi wa majengo ya ofisi ya Keza na ununuzi wa magari 106 kwa ajili ya chama chake. 

Anadaiwa kujipatia vitu hivyo kati ya mwaka 1994 na mwaka 2004 wakati akiwa madarakani. 

Hata hivyo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Mike Tembo, baada ya kusikiliza mashtaka toka kwa Mkurugenzi wa ACB, Alex Nampota, na wakili wa upande wa mshtakiwa, Fahad Assan, aliamuru kesi hiyo kuhamishiwa Mahakama Kuu. 

Aidha, Mahakama ilimtaka Muluzi na Lyness kuwasilisha hati zao zote za kusafiria. 

Mapema Januari 28 mwaka huu, ACD ilituma maswali kwa Muluzi wakimtaka kuelezea namna kiasi cha Kwacha milioni 21.9 sawa na dola za Marekani 156,565 za mfuko wa pamoja zilivyoweza kuhamishiwa katika balozi tatu za Malawi zilizopo Japan, Tanzania na Uingereza katika kipindi cha kati ya mwaka 2003 na 2004. 

Muluzi alipaswa kujibu maswali hayo kwa muda wa siku 21, lakini mawakili wake walitafuta kibali cha muda kuzuia mteja wao kuhojiwa na ACB. 

Muluzi ni mgombea wa kiti cha Urais kupitia chama cha UDF katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Mei 19, mwaka huu. 

Katika uchaguzi ndani ya chama chake, Muluzi alipata kura 1,950 dhidi ya mpinzani wake ambaye ni makamu wa chama chake, Cassim Chilumpha, aliyepata kura 30. 

Muluzi aliyekuwa rais kati ya mwaka 1994-2004, alijaribu kubadili katiba ili kuongoza muhula wa tatu bila mafanikio. 

Rais wa sasa, Bingu wa Mutharika, alichaguliwa na Muluzi ili kumrithi kiti hicho, lakini mara baada ya kuingia Ikulu wawili hao walianza kusigana, hatua iliyosababisha Mutharika aunde chama chake. 

Muluzi alipokuwa madarakani alikuwa mshirika wa karibu wa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa. 

Alipokuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alimsaidia Muluzi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa muhula wake wa pili, kwa kutuma kikundi cha sanaa na burudani cha CCM cha Tanzania One Thietre (TOT) kwenda nchini Malawi na kukaa kwa miezi kadhaa kwa ajili ya kumpigia debe. 

Baada ya kufanikisha ushindi huo, TOT chini ya kiongozi wake, Kapteni John Komba, ilirejea nchini ikiwa na zawadi kadhaa, likiwemo gari kubwa maalum kwa ajili ya kubeba wasanii na vifaa vyao wakati wa kutoa burudani hasa wakati wa kampeni za CCM. 

Kapteni Komba baada ya kurejea kutoka Malawi katika kampeni za Muluzi, alifungua Shule ya Sekondari katika eneo la Mbweni, Dar es Salaam na kuiita jina la Bakili Muluzi. 

Moja ya mambo ambayo serikali ya Mkapa iliyaiga kutoka Malawi wakati wa utawala wa Muluzi ni Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Malawi (MASAF). 

Pia Rais Mkapa aliwahi kwenda kufungua miradi ya binafsi ya Muluzi na kumpongeza kwa jitihada zake za kujiimarisha kiuchumi. 

Kumpongeza kwa Hivi sasa Mkapa anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka hususan kuanzisha kampuni ya Tan Power Resources Limited na kufanya biashara Ikulu. 

Baadhi ya wabunge, wanasiasa na wanaharakati wanashinikiza Mkapa aondolewe kinga ili ashitakiwe kwa makosa hayo aliyoyatenda, ambayo hayahusiani na majukumu ya urais. 

Kosa wanalomtuhumu ni kuitumia kampuni hiyo kujimilikisha mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ulioko katika Mkoa wa Mbeya. 

Inadaiwa kuwa Mkapa na aliyekuwa Waziri wake wa Nishati na Madini, Daniel Yona, walijimilikisha mgodi huo kinyemela na kwa gharama ndogo kulinganisha na thamani yake halisi. 

Gharama halisi ya mgodi huo ni Sh. bilioni nne lakini wao walijimilikisha kwa Sh. milioni 700. Hata hivyo, badala ya kulipa kiasi hicho, walilipa Sh. milioni 70 tu. 

Mjadala kuhusu suala hilo umewagawa Watanzania katika makundi mawili. 

Kundi moja linalowahusisha baadhi ya viongozi wa dini na wanasiasa linataka Mkapa aachwe apumzike wakati lingine likipendekeza bunge limuondolee kinga ili akabiliwe na mkono wa sheria. 

Hata hivyo, licha ya kutupiwa tuhuma hizo, Mkapa ameamua kuendelea kukaa kimya badala ya kuzikanusha.

  • SOURCE: NIPASHE


No comments: