Wednesday, February 11, 2009

William Macha na Julius Kihampa


KITAELEWEKA? Wachezaji wa kikosi cha timu ya soka ya taifa, Taifa Stars jana alfajiri walijikuta wakivamiwa na kukurupushwa kutoka vyumbani ili wapimwe damu zao kubaini iwapo wanatumia dawa za kulevya au la. Zoezi hilo la upimaji liliendeshwa katika kambi ya timu hiyo iliyopo Hoteli ya Atriums maeneo ya Sinza Afrikasana jijini Dar es Salaam na kusimamiwa na daktari wa Taifa Stars, Sufiani Juma. Shuhuda wetu alitupasha kuwa, wachezaji wote wa Taifa Stars waliamshwa mapema alfajiri na kuanza kuchukuliwa damu ili kupima kama wana magonjwa na pia iwapo wanatumia dawa za kulevya.

“Ilikuwa ni zoezi la ghafla, kwani hata wachezaji wenyewe hawakuambiwa kama kutakuwepo na zoezi hilo leo (jana), ila lilienda vizuri na lilisimamiwa kwa umakini na Dk. Sufiani,” kilisema chanzo chetu. 

Ildaiwa kuwa wakati zoezi hilo lilifanyika kwa umakini mkubwa, huku lengo likiwa ni kutaka kwenda na wachezaji safi katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), huku kukiwa na madai baadhi ya wachezaji wa Stars wanatumia bangi. 

Akizungumza na Championi Jumatano mara baada ya zoezi hilo kukamilika, Dk. Sufiani alisema wachezaji wamepimwa vipimo vyote na zoezi halikuwa na dosari yeyote. 

Alisema waliamua kuwafanyia asubuhi kwani katika kipindi hicho unaukuta mwili ukiwa katika hali ya kawaida, hivyo vipimo vinavyotoka vinakuwa sahihi. “Zoezi limekamilika mapema asubuhi hii (jana) na limekwenda vizuri, tumeamua kuwavamia asubuhi kutokana na taratibu za kidaktari ambapo wakati huo, unaweza kupata vipimo sahihi zaidi na kwa kuwa mwili unakuwa umetulia,” alisema.

Daktari huyo aliongeza kuwa katika vipimo hivyo, wamechukua sampuli za damu za wachezaji wote kwa ajili ya kuangalia mambo mbalimbali ambapo uchunguzi wa magonjwa ya kawaida utafanywa Hospitali ya Taifa Muhimbili, wakati vile vya kutambua kama wanatumia dawa za kulevya vitaangaliwa Afrika Kusini au Tunisia. 

“Vipimo vya magonjwa kama maralia na mengineyo nitavipeleka Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi, lakini hivi vingine kwa ajili ya dawa za kulevya ni vigumu kutolea mchanganuo kwa sasa kwani vipimo vyake vinafanyika Afrika Kusini au Tunisia, hapa nchini hakuna maabara inayoweza kupima.” 

Alisema ingawa kulikuwa na hofu ya kawaida kwa wachezaji wakati wa kuchukua vipimo hivyo, lakini wote wameunga mkono kupimwa ili kuondoa fikra potofu miongoni mwa watu kama wanajihusisha na matumizi ya dawa za kulevya. 

Wakizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, baadhi ya wachezaji wa Stars walisema wamefurahishwa na zoezi hilo na pia wako tayari kupokea majibu ya matokeo ya vipimo vyote walivyofanyiwa.

“Bora wametupima bwana, watu wamezungumza sana baada ya kutolewa taarifa kwamba tutapimwa kama tunatumia dawa za kulevya hasa bangi na hayo matokeo ndiyo yatakayowanyamazisha, kwani sisi tunajiamini,” alisema kiungo wa Stars, Mwinyi Kazimoto. 

Wachezaji waliopo katika kikosi hicho na waliopimwa kama wanatumia dawa za kulevya ni, Deo Mushi, Shaaban Dihile, Farouk Ramadhani, Shadrack Nsajigwa, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Juma Jabu, Nurdin Bakari, Nadir Haroub, Salum Swedi, Zahor Pazi, Kelvin Yondani, Godfrey Bonny, Shaaban Nditi, Nizar Khalfan, Athuman Idd, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa, Haruna Moshi, Jerry Tegete, Jabir Azizi, Mussa Mgosi, Kigi Makassy, Salvatory Ntebe, Uhuru Seleman, Wakati huohuo, Taifa Stars leo inaingia katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, kukwaana na Zimbabwe katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki wa kujipima nguvu. 

Chausiku Omary anaripoti kuwa, Kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo amesema anasikitishwa na kauli za mashabiki wanaodai ana mapenzi makubwa na Yanga kuliko timu nyingine zozote hapa nchini. “Mimi sina upendeleo na timu yeyote kwa sababu kwanza mimi nilikuja Tanzania kwa ajili ya kufundisha timu ya Taifa na sio timu nyingine.

Mimi ninapotaja kikosi cha timu yangu siangalii timu fulani ila ninachoangalia ni uwezo wa mchezaji tu na sio kitu kingine. “ ashindwa kuwaelewa hao wanaosema mimi ni kocha wa Yanga, kama ningekuwa kocha wa Yanga basi ningechagua wachezaji wa timu hiyo tu bila kuchanganya na kuwapa mazoezi ya kutosha ili waweze kuiwakilisha Tanzania,” alisema Maximo.


Kutoka Global Publishers Limited


No comments: