Ajali ya treni yaua 13
Watu 13 wanahofiwa kufa katika ajali mbaya ya treni iliyotokea katika eneo la Gulwe na Igandu na wengine saba wakijeruhiwa huku serikali ikidai kuwa ajali hiyo imesababishwa na hujuma iliyofanywa na wafanyakazi wa Kampuni ya Reli (TRL) kwa kushirikiana na wananchi ambao si waaminifu. Hadi kufikia jana jioni, miili saba ilikuwa imeopolewa katika baadhi ya mabehewa ambapo miili hiyo haijatambuliwa na imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 10:29 alfajri katika eneo la Msagali Kata ya Chunya Wilaya ya Mpwapwa katikati ya Stesheni ya Gulwe na Igandu kilomita chake kutoka eneo la ajali ya treni ya abiria ya mwaka 2006, hivyo kuwakumbushia Watanzania ajali hiyo mbaya ya treni katika historia ya Tanzania. Ajali ya jana ilihusisha treni ya abiria namba A11 na kichwa namba 73-R -17 na ya mizigo namba A-11, zote zikiwa zimetoka Dar es Salaam kwenda Mwanza.
‘HabariLeo’ ilishuhudia mwili wa kijana mmoja ukiwa umebanwa na behewa ambapo kifua na kichwa vikiwa juu na kiwiliwili kimebanwa chini, hivyo kuhitajika kazi ya ziada ya kutenganisha behewa hilo namba 3712 na injini ya treni hiyo; huku ikielezwa kwamba alipatwa na mauti akiwa ameenda chooni.
Marehemu wengine walioopolewa baada ya behewa namba 3705 kukatwa kwa kutumia gesi na nyundo walitambuliwa kwa majina ya Joston Lucas fundi bomba; mwingine alitambuliwa kwa jina moja la Yohana huku maiti wengine watatu wakiwa wanaonekana ndani ya behewa hilo 3705 wakiwa wamebanwa na kuna uwezekano wa kupatikana kwa miili zaidi ndani ya behewa hilo.
Hata hivyo gadi anayesaidiana na dereva kwa upande wa nyuma, Absalom Mwaisukule alisema hajui lolote kuhusu ajali hiyo na alishtukia mshindo mkubwa na kugundua kuwa tayari wamepata ajali, hivyo kumwomba mwandishi wa habari hizi kuwauliza viongozi wa TRL na si yeye.
Akizungumza na gazeti hili, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dk. Seif Mhina, alikiri kupokea majeruhi saba ambao ni Abbas Kafyome (62) mkazi wa Nyamanoro Mwanza; Jafet Kikando (30) wa Kiteto; Alphonce Kayanza (32) Tabora; Shija Mtenza (50); Butika Simwenda (20); John Makenza (22) mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Uchama Nzega na Sajini wa Magereza Asha Majala. Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Rajabu Kabogota alisema ni mapema kutoa taarifa kamili kuhusu ajali hiyo, lakini taarifa za awali zinaonyesha ilitokana na uzembe wa Kituo cha Gulwe kuruhusu treni ya abiria kabla ya kuhakikisha ya mizigo imefika katika kituo kilichofuata cha Igandu.
Alisema pamoja na uchunguzi kamili kutokamilika kwa muda huo, lakini kwa kawaida Stesheni Masta hawezi kuruhusu treni kuondoka kabla hajaridhika kwa taarifa sahihi kutoka kituo kinachofuata kuwa iliyotangulia imefika salama na njia ni salama. Mabehewa yaliyohusika katika ajali hiyo ni namba 3712, 3720 na 3705 ambayo ndiyo yaliyokandamizwa na namba 3720, 3710,3701,3702, 3714,3704,3715 na injini yake ya nyuma namba B.V.B8600. Treni ya mizigo ilikuwa na mabehewa 19.
Waziri wa Maendeleo ya Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa aliyefika katika eneo la ajali jana, alisema imesababishwa kwa kiasi kikubwa na wafanyakazi wa TRL, ambao wamekuwa wakiiba mafuta na mizigo inayosafirishwa katika mabehewa kwa kushirikiana na wananchi wasio waaminifu. Dk. Kawambwa aliagiza kukamatwa mara moja kwa wakuu wa vituo vya Stesheni ya Igandu na Gulwe ili wahojiwe juu ya chanzo cha ajali hiyo. Pia Waziri huyo ametoa siku tatu kwa Kikosi cha Polisi cha Reli ya Kati kutoa taarifa kamili ambayo itaelezea chanzo halisi cha ajali hiyo.
Kutokana na hali hiyo, alisema serikali inapitia upya utaratibu wa uendeshaji wa shirika hilo na kuongeza kuwa serikali inatambua kuwapo kwa upungufu mwingi katika uendeshaji wa TRL. Aidha, Dk. Kawambwa amekasirishwa na kitendo cha uongozi wa kampuni hiyo kuchelewa kufika katika eneo la ajali ambapo viongozi hao walifika majira ya saa 10 jioni.
No comments:
Post a Comment