Saturday, March 28, 2009


 

Mbunge wa Bariadi Mashariki, Adrew John Chenge ametiwa mbaroni na jeshi la Polisi nchini bada ya kutuhumiwa kuua kwa kuwagonga na gari wasichana wawili waliokuwa kwenye usafiri wa Bajaj. kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, ajali hiyo ilitokea saa kumi juzi usiku (Alhamisi) kwenye makutano ya Barabara ya Haile Selaise na Morogoro Store, jijini Dar es Salaam. Vyanzo vyetu vikazidi kudai kuwa, wasichana hao wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 20 na 25, walikuwa wakitoka kujirusha kwenye Club ya Maisha iliyopo Masaki, jijini Dar.

Inadaiwa kuwa, Chenge aliivaa kwa nyuma Bajaj hiyo yenye rangi ya Bluu na namba za usajili T 736 AHE na kusababisha vifo vya abiria hao wawili huku dereva wao akinusurika na kuingia mitini. 

Ilielezwa kuwa, Mheshimiwa Chenge aliyawahi kuwa Waziri wa Miundombinu Awamu ya Nne na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin yenye namba ya usajili T 512 ACE ambayo kufuatia ajali hiyo, iliharibika kwa mbele.

Nao mashuhuda waliokuwa katika eneo la tukio maeneo ya Shule ya Msingi Oysterbay waliliambia gazeti hili kuwa, waliliona gari la Mheshimiwa Chenge likiwa katika mwendo wa kasi na lilikuwa likiyumba barabarani kabla ya ajali hiyo. 

“Mimi niliiona kabisa ajali hile wakati ikitokea, nilimwona dereva wa Bajaj akijitahidi kulikwepa gari la Mheshimiwa lakini bila mafanikio, maana ile spidi kama haikuwa 120 bahati,” alisema kijana mmoja ambaye alidai kuwepo eneo la tukio. 

Mashuhuda waliendelea kusema kuwa, baada ya ajali hiyo, mzee wa ‘vijisenti’ ambaye alikuwa na binti mmoja mweupe aliminya kwa muda ndani ya gari mpaka alipotokea askari polisi mmoja ambaye alisikia mlio wa ajali na kufuatilia kujua kulikoni.

Waliendelea kudai kuwa, baada ya Mheshimiwa Chenge kushuka alionekana dhahiri alikuwa ‘amepata kwa sana’ (amelewa) hali iliyotafsiriwa na mashuhuda wetu kuwa, ilichangia kutokea kwa ajali hiyo mbaya.

“Kusema ule ukweli Mheshimiwa alikuwa ‘nyingi’ hata kwa macho tu. Na tunahisi ndiyo maana ilitokea ajali, si unajua tena mambo ya ‘kilaji’ halafu naiti kali,” alisema shuhuda mmoja.

Hata hivyo habari zinadai kuwa ajali hiyo ilisababishwa na dereva wa Babaj baada ya kulichomekea gari la Mhe. Chenge na kwamba alikimbia baada ya kugundua kosa lake.

Nao baadhi ya wakazi wa jiji la Dar waliokuwa kwenye kituo cha Polisi cha Oysterbay ambako Mheshimiwa Chenge alikuwa ameshikiliwa, walisema Chenge amekuwa akikatiza katika mbuga ya mikosi kwa muda mrefu sasa bila kujulikana sababu. 

Walitolea mfano wa mkosi wa kwanza wa kashfa ya kuzichimbia nje ya nchi Shilingi za Kitanzania bilioni moja ambapo ili hali ya hewa Serikalini ikae sawa ilibidi aachie ngazi huku Kampuni ya Kimataifa ya Serious Frauds Organization (SFO) ikimchunguza kwa karibu.

Kama vile haitoshi, baadaye Mheshimiwa huyo alipigwa kibega na mkosi mwingine akidaiwa aliingia Bungeni na kunyunyuzia ‘madongoloji’ (uchawi) kwenye viti vya waheshimiwa wenzake, hata hivyo, uzushi huo ulitupwa mbali na Spika Sitta baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kitaalam.

Akiwa bado ana machungu ya mikosi, Alhamisi ametokewa na hili la kuua kwa kugonga na gari, wengi wanasema kweli ni mikosi juu ya mikosi.

Habari za ndani zinadai kuwa, Mheshimiwa huyo amebadilika tabia toka alipokumbwa na kashfa ya ‘vijisenti’ huku ikidaiwa kuwa, mara kadhaa amekuwa akitumia kinywaji kikali aina ya Captain Morgan akiamini anapoteza mawazo. 

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

 

No comments: