Ole wetu sisi wazazi
hapa Norway.
Unaweza kufungwa
kwa kumfinya,
kumdhihaki au
kumkaripia mtoto...
Ole wetu sisi wazazi hapa Norway. Wizara ya watoto na usawa wa jamii (Barne-og likestillingsdepartmentet) wanafikiria kupeleka mswada Bungeni (Stortinget) wa kubadilisha sheria ya watoto (Barneloven) na ya makosa ya jinai (straffeloven) ili ziwabane wazazi kwenye malezi ya watoto wao. Wizara inasema lengo la kubana vipengele ni kuhakikisha kuwa watoto hawateswi kwa nguvu au kisaikolojia na wazazi au walezi wao. Limeandika gazeti la Jumapili leo la Aftenposten.
Kama mswada huo ukipita, itakuwa ni kosa la jinai kwa mzazi kutoa adhabu ya aina yoyote kama kumchapa mtoto, kumfinya, kumtolea vitisho, kumkaripia, kumgombeza, kumsengenya, kumfanyia dhihaka na kumdhalilisha.
Hilo la kuchapa liko kwenye sheria ya watoto (barneloven), lakini halikuwa kosa la jinai.
Chanzo cha mabadiliko haya ni uamuzi wa kesi moja mwaka 2005 uliofanywa na mahakama kuu ya Norway (Høyesterett) kuwa si kosa kumfunza mtoto adabu hata kama ikiwa ni kumshika kwa nguvu na kumtingisha au kumsukuma sukuma. Hilo lilizuia soo kubwa kati ya wahafidhina, wanaounga mkono malezi makali juu ya watoto na wapenda mabadiliko ya kila mara, wanaopinga mtoto kushikishwa adabu kwa njia za kiasili, kama ilivyotajwa hapo juu.
Jaji Mkuu wa Norway, Tor-Aksel Busch anaunga mkono mswada huo kwa shingo upande, kwa kusema ni sawa kuhakikisha watoto hawatendewi mabaya na wazazi wao, lakini itawanyima wazazi haki ya malezi wanayoona yanafaa kwa watoto wao!
Chanzo: Aftenposten, Jumapili 15.Machi, 2009
No comments:
Post a Comment