Thursday, March 19, 2009



Watanzania tuache

kuwa wanafiki



Mhariri
Daily News; Wednesday,  March 18, 2009 @18:13


Wakati mauaji ya albino yalipoanza kubainika nchini na wimbi kuongezeka, zilikuwapo lawama za hapa na pale kutoka ndani na nje ya nchi, hususan kwa vikundi vya wanaharakati wakiwamo watetezi wa haki za binadamu.

Kelele nyingi zilielekezwa kwa serikali, kwamba imeshindwa kulinda watu wake na ndiyo sababu mauaji haya yanaendelea, hata kusababisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kufanya ziara mikoani na kushuhudia unyama huo ambao kwa kweli ulimuumiza sana.

Si yeye tu, lakini watu wengi wapenda amani na wanaojali thamani ya ubinadamu, ni vitendo vilivyowahuzunisha kiasi cha kuihimiza serikali kuchukua hatua ya kuwakamata wauaji hawa na kuwachukulia hatua stahiki ikiwezekana wauawe.

Waziri Mkuu Pinda alifikia hatua akazidiwa uchungu mpaka akajikuta anatamka kuwa wauaji hawa na wauawe. Baadhi ya watu na viongozi wa siasa wakiwamo wabunge wanaoheshimika, wakaja juu na kumlaumu Waziri Mkuu kuwa anaruhusu mauaji ya kujichukulia sheria mkononi.

Hata alipojieleza bungeni, Pinda alikosa uvumilivu akatokwa na machozi hasa alipokumbuka matukio ya mauaji hayo alipokuwa ziarani Tabora, lakini alijieleza vizuri na akaeleweka na kuchomoka katika wingu hilo zito lililoanza kuonekana kutegwa kisiasa.

Baada ya kauli ya dhati ya Waziri Mkuu ya serikali kuchukua hatua madhubuti dhidi ya mauaji haya, Rais Jakaya Kikwete alilitangazia Taifa kusudio la kufanyika kura za kuwabaini wauaji hawa pamoja na wa vikongwe; na majambazi.

Hatimaye kura zimeanza kupigwa, waliopigiwa hawajatambuliwa wala hatua hazijachukuliwa, tayari lawama zimeanza kutolewa tena kupitia vyombo vya kigeni, kuwa hatua hii ni mbaya na inakiuka haki za binadamu!

Wanaozungumza hivi ni Watanzania hawa hawa, ambao leo waliilalamikia serikali kuwa haichukui hatua, lakini sasa hatua zinachukuliwa, umekuwa sasa ni ukiukwaji wa haki za binadamu, hawa ni wanaharakati na baadhi ya wanasheria wetu wenyewe! Sisi tunajiuliza, wanataka serikali ifanye nini?

Wanasema imeshindwa kuwalinda watu wake, iwalinde vipi? Kila mtu apewe askari wake aishi naye nyumbani na silaha? Au ijenge mtambo ambao kila Mtanzania ataonekana kila anachokifanya popote alipo? Tunadhani hatua hii ni ya awali na si kwamba kila atakayebainika kapigiwa kura atauawa bila kuchunguzwa na kujiridhisha kuwa kweli ameshiriki, kama ambavyo alivyojiita mwanasheria aliyehoji kupitia chombo cha kigeni, kuwa nani atatoa ushahidi mahakamani.

Ieleweke wazi, kuwa sheria inatamka wazi, kwamba muuaji ana haki ya kusikilizwa mahakamani na auaye albino ameua binadamu na hakuna sheria popote inayobagua kuwa huyu kaua albino, basi ahukumiwe bila kusikilizwa! Kupinga juhudi zinazofanyika ni kuitega serikali, ife moyo na baadaye watu hawa hawa waibuke na kuizodoa kuwa imeshindwa kulinda wananchi wake. Huu ni unafiki na tunadhani serikali haitayumbishwa na wanaharakati uchwara kama hawa wenye uchungu feki na mauaji ya albino.


No comments: