Sunday, April 05, 2009

Kiswahili na jukumu lake la  

kimaendeleo,  kimataifa



Na Sammy Makilla


TANZANIA inaonekana kuwa nyuma katika kuendeleza lugha ya Kiswahili ukilinganisha na nchi zingine kama vile Uingereza, Rwanda, Burundi na Kenya.

Hali si nzuri katika Baraza la Kiswahili Tanzania kama ilivyo kwa Taasisi ya Uchunguzi na Uendelezaji Kiswahili nchini. Je, hii ni kwa sababu ya umasikini wa Tanzania? La hasha. Katika nchi zilizo mstari wa mbele kuendeleza Kiswahili ni Uingereza kupitia shirika lake la utangazi (BBC), ambayo unaweza kusema ni nchi tajiri.

Jibu muafaka ni kwamba; sidhani kwa hali hiyo inahusiana na umasikini wetu hata kidogo. Jibu muafaka pengine linaendana na Watanzania hadi wa leo kutokuwa na nia, sababu na ari ya kuitumia na kuiendeleza kikamilifu lugha yao ili iwe ni aina mojawapo ya uwekezaji ndani na nje ya nchi.

Toka awamu ya kwanza imekuwa ni kawaida kwa viongozi wetu kuhadaika na kujipa matumaini yasiyostahili kwamba, nchi hii inaweza ikaendelezwa haraka zaidi kwa kutumia lugha ya kigeni badala ya lugha yetu.



Ushahidi (kwa mfano ukienda iwe India, Korea Kusini, Malaysia, Singapore, Indonesia, Vietnam, Cambodia, China na Uarabuni) unaonyesha dhahiri kuwa nchi zinazotumia lugha zao wenyewe zina nafasi nzuri zaidi ya kuendelea kuliko zinazotumia lugha za kuazima.

Hapa Afrika ukitoa Afrika Kusini, Botswana na Namibia nchi zote zinatumia lugha za kuazima (Kiingereza, Kireno au Kifaransa) na takriban zote ni masikini.

Swali la kujiuliza hapa ni je Kiswahili kingelikubalika kama lugha ya Afrika yote kusini mwa Sahara,hivi kweli tungelikuwa hapa tulipo?




Nini ruiya na azma yetu? Ili kutambua umuhimu wa Kiswahili katika leo na kesho yetu ni muhimu kujua ni nini ruiya (visheni) na azma (misheni) yetu minghairi ya lugha ya taifa hili-Kiswahili.

Baada ya kupata ruiya na azma hiyo inakuwa sasa ni rahisi kupanga na kuweka mikakati ya malengo na matarajio mbalimbali kwa watu, taasisi na maeneo mbalimbali. Je, ruiya yetu ni kwa Kiswahili kuwa tu lugha ya Tanzania au ya Afrika. Na hali kadhalika, iwe ni lugha inayotumika tu shule za msingi au mpaka chuo kikuu? Ruiya yetu ni kwa sisi wenyewe, yaani, Watanzania kuwa mstari wa mbele kuiendeleza lugha yetu au kuwaachia BBC na wengineo ndio watuoneshe njia?

Kwa kutafakari maswali hayo hapo juu bila shaka tunaweza kufikia uamuzi wa hekima na busara kuwa ruiya yetu inapaswa iwe nini. Kwa sasa hivi inavyoelekea serikali, vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla wanakifanya kiswahili kuwa ‘boi’ au mtumishi wa nyumbani na hawatarajii au hawana habari kuwa lugha hiyo inaweza kujifaragua penda tusipende ili iwe bosi mahala fulani. Azma ni yale mambo ambayo tunapaswa kuyafanya ili ruiya iwe kweli.

Ni baada ya kuipata ruiya tuitakayo ndipo itakapofaa sasa kuanza kutafakari mambo yanayostahili kufanyika ili tufike kule tunakotaka kwenda. Hili husaidiwa kwa kuwepo kwa sera, malengo na mikakati mbalimbali ambayo kwa umoja na wingi wao husaidia kufanikisha kufikiwa kwa ruiya tarajiwa.

Tahadhari kuwa tunaposema kuwa lugha ya Kiswahili itumike hapa nyumbani au Afrika hatuna maana kwamba lugha nyingine hazitatumika tena. La hasha. Afrika tofauti na nchi nyingi duniani tuna fursa peke ya watu wetu kuwa wazungumzaji lugha tatu au nne kwa ufasaha.

Dhamira yetu iwe ndiyo hiyo. Kwamba, pamoja na Kiswahili, Mwafrika wa kesho atakuwa anazungumza pia Kiarabu na au Kiingereza au Kifaransa, Kiafrikansi au Kizulu au Kihausa au Kireno au Kigujarati au Kihindi au Kichina au Kijapani au Kijerumani na kadhalika. Lakini ili hili litokee lazima nchi zetu zikae mkao wa kutukuza na kushabikia watu kuzungumza lugha zaidi ya mbili au tatu toka shule za msingi. Wenzetu Uholanzi na Swideni wanaweza, kwa nini sisi tushindwe.



Hata hivyo, kwa kuzingatia kuwa Kiswahili ni lugha mama, lugha ya mzizi kwa Waafrika wengi na lugha yenye mashiko katika makabila na historia yetu na kwamba, wenetu wanaelewa haraka zadi wanachofundishwa kwa lugha yao mama kuliko za kigeni, tutoe kipaumbele kwa lugha hii kufunzwa na kutumika na wote. Tanzania ndio inayostahili kuonesha njia katika hili.

Lakini kama ilivyo kwa vitu vingi, hatuoneshi msukumo, hatuweki mtaji, hatuvutiwi na tulicho nacho, hatutumii vyema watu wetu, hatuwasaidii watu wetu na hatuoni fursa zilizopo mbele yetu kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Kuna wanaoamini kwamba, Kiswahili kina weza kuifanya Tanzania 'superpower' Afrika, kama itaacha kuwa mdebwedo na kuanza kushughulikia kwa tasihili ya kipekee masuala yafuatayo:

Tanzania pengine kuliko nchi nyhingine Afrika inastahili kuwa mstari wa mbele katika kujenga miundomsingi wa kuiendeleza na kukuza Kiswahili katika matumizi yake kijamii, kibiashara, kiuchumi, kiutamaduni na kiteknolojia ndani na nje ya nchi. 



Miundomsingi katika lugha ni yale yote yanyorahisisha kutumika, kukubalika, kutafitiwa na kuendelezwa. Ukianzia nyumbani, ni upatikanaji wa vitabu, magazeti na machapicho mengine kwa bei nafuu; kusilikiza redio kwa Kiswahili na kutazama televisheni, filamu na michezo mbalimbali kwa Kiswahili.

Katika shule na vyuo ni upatikanaji wa maarifa, elimu na ujuzi wa mambo mbalimbali katika lugha ya Kiswahili. Na kitaifa ni mfumo jumla wa jamii, uchumi, utamaduni, siasa na teknolojia kuendeshwa kwa lugha hiyo bila tatizo lolote ili raia wa kawaida waelewa kinachomzunguka na kuendelea popote nchini na duniani.

Kwa kutambua kuwa asilimia kubwa ya watu wetu hawatakuwa na mahusiano makubwa na wageni kufundisha masomo mengi kadri iwezekanavyo kwa Kiswahili, ili kurahisisha kueleweka na kutumika kwa maarifa mbalimbali yatakayochangia kuongeza kasi ya maendeleo ya watu wetu.



Kubwa ambalo watu toka Tripoli hadi Moroni, Kinshasa hadi Abuja, Khartoum hadi Harare wanalikitegemea kutoka kwetu kwa hivi sasa, ni kuanzishwa na kuendeshwa kitaalamu na kifaida vituo vya ufudnishaji Kiswahili katika nchi mbalimbali Afrika.Mathalani, katika ziara yake Comoro, Rais Jakaya Kikwete pamoja na mambo mengine, aliombwa kusaidia kupata walimu wa kuwafundisha Wakomoro Kiswahili.

Kingazija ni mojawapo ya lahaja za Kiswahili lakini chenyewe sio Kiswahili sanifu.Aidha Tanzania inapaswa kuwa mstari wa mbele katika Kutoa changamoto kwa uanzishwaji magazeti, redio na televisheni za Kiswahili; kuchangia rasilimali katika uendelezaji wa wavuti za Kiswahili; kuchangia katika maendeleo ya uendelezaji video na sinema za Kiswahili vyote vikiwa na shabaha ya kuharakisha muungano na maendeleo ya uchumi ya Afrika.



Vilevile lazima Tanzania kuhamasisha wengine katika kuchangia na kusaidia kupunguza gharama za utafiti na machapisho mbalimbali katika Kiswahili; uendelezaji uchoraji katuni kwa magazeti na televisheni kwa malengo kama ya hapo juu. Wasiwasi wa Watanzania

Unapozungumzia maendeleo ya Kiswahili kama lugha toshelevu katika harakati zetu za kijamii, kiuchumi, kisayansi, kiteknolojia, kielimu na kadhalika; wasiwasi wa watu wengi ni kwamba, utasababisha Kiingereza chetu kuwa rojo zaidi. Hili silikubali.

Enzi za Mwalimu, wakati sisi tukifundishwa Kiingereza na walimu toka Uingereza, Marekani na India mbona Kiingereza kilipanda. Dawa ya kuhakikisha watoto wetu wana kitawala vyema Kiingereza sio kwa kudhoofisha Kiswahili bali ni kwa kuimarisha Kiingereza kwa kuwa na walimu wazuri ambao aghalabu Kiingereza ni lugha yao ya kwanza. Kwa namna hii, tutaua ndege wawili kwa jiwe moja.

Vijana wetu wataelewa dhana na maarifa mbalimbali kwa urahisi na vilevile watakuwa wazuri katika lugha za nje ikiwemo Kiingereza, Kiaabu, Kireno, Kifaransa, Kihindi, Kichina na kadhalika, jambo ambalo pia litaongeza thamani yao kama wasomi na wafanyakazi popote duniani.

Kwa kumalizia napenda ieleweke kuwa Kiswahili ni rasilimali sawa na rasilimali nyngine hapa nchini. Kama zilivyo rasilimali nyingine kama haitafnyiwa kazi ya kuchakatwa na kutumika kwa manufaa ya maendeleo yetu, lugha hii ikawa sababu ya sisi kubaki nyuma kwa miaka mingi ijayo. Hata hivyo, endapo tunazinduka toka usingizini na tukagundua kwamba, kumbe kwa kukidharau Kiswahili tunapoteza mengi kisha tuanze kufanyia kazi mipango na mikakati ya kukiendeleza ili kituendeleze, Tanzania bila wasiwasi wowote ina nafasi ya kuwa 'superpower' hapa Afrika.



Barua-pepe: sammy.makilla@columnist.com

Toka gazeti la Mwananchi

No comments: