Thursday, April 02, 2009

Mahojiano:

Mohamed Raza

”kuendekeza urafiki

kutatuponza..”



Mshauri wa aliyepata kuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, Mohamed Raza, anasema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinahitaji kurekebishwa katika uongozi wa juu, hususan, wakati huu ambao jua linakuchwa. Akizungumza katika mahojiano maalumu na Godfrey Dilunga wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, Raza pia alizungumzia ufisadi. Endelea.

Raia Mwema: Umekuwa mshauri wa Rais wa Zanzibar…naamini una ufahamu na uzoefu wa kutosha kuhusu masuala ya uongozi, unazungumziaje kwa muhtasari mwenendo wa uongozi nchini?

Mohamed Raza

Mohamed Raza

Raza: Ninachosema ni kwamba tokea uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar naona kwa kweli Watanzania wana mwamko mkubwa sana na Bunge hili lililopo limeweza kuleta mabadiliko mengi.

Wabunge bila kujali itikadi zao za kisiasa wameweza kuleta mabadiliko mengi na wameleta mwamko  kwa Watanzania na hasa katika hali hii tunayokwenda nayo ya kashfa kama za EPA, Dowans na Richmond.

Kwa hiyo Watanzania sasa hivi tuna mwelekeo mmoja, kwamba ukombozi wetu ni Bunge lililopo na kuna haja kwa Watanzania kuwaombea dua wabunge ambao wanajitoa mhanga kwa kuweza kuyatoa mambo ambayo yalifichwa kwa muda mrefu yakinufaisha wachache.

Raia Mwema: Umetaja baadhi ya mambo kama EPA, Dowans na Richmond, ambayo yameleta mjadala mkali nje na ndani ya Bunge huku baadhi ya wabunge wakilumbana. Je, unaridhika na mjadala wa masuala haya na uamuzi uliofikiwa?

Raza:  Kwanza nasema mijadala hii ingekufa kama tusingekuwa na Bunge imara na wabunge waliojitoa mhanga. Mjadala ungelikufa na mimi natoa wito kwa wananchi huu mjadala tusiufunge. Kuna haja ya waandishi wa habari na Watanzania wote kuuendeleza uwe na faida kwa Watanzania wengi. Lakini kitu cha kuonyesha hapa sisi Watanzania nafikiri tumtake mchinja ng’ombe.

Raia Mwema: Kumtaka mchinja ng’ombe ndiyo kusema nini?

Raza: Kwa sababu pesa hizi zilizochotwa, mtu anachota bilioni 100, 200 lazima kuna mchinja ng’ombe. Mtu hawezi tu kwenda benki akachota pesa. Hawezi.

Kwa hivyo kuna haja ya Watanzania kuliangalia suala hili kwa urefu sana na tusipofanya hivyo matajiri wachache wanaweza kuliumiza Taifa na hata kuharibu uhuru tulioupata.

Kwa mfano, chanzo cha Mapinduzi ya Zanzibar ni mmoja alijiona bora, kundi fulani lilijiona bora kuliko kundi jingine katika kila kitu. Kwa hiyo, mimi naona kwamba haya yametokana na ubabe wa viongozi waandamizi.

Lakini ubabe haujengi nchi. Kwa mfano, watu walipiga sana kelele kupinga suala la rada na ndege ya Rais, hawakusikilizwa, sasa kuna haja ya wananchi wakasikilizwa.

Nasema katika hali hii tuliyofika watendaji wote hasa wa kitaifa ni lazima wawe wakweli kwanza ndipo wawaambie wengine kuwa wakweli. Unapotaka kuwaeleza wenzako ukweli lazima nawe uwe mkweli kwanza.

Raia Mwema: Unaweza kufafanua? Unalenga makundi ndani ya CCM?

Raza: Hapo tuwaachie Watanzania wenyewe wapambanue. Lakini lazima unapotaka kumwambia mwenzako ukweli basi lazima nawe uwe mkweli.

Raia Mwema: Mwanzo ulizungumzia kidogo matajiri wachache wanavyoweza kuumiza Taifa. Ulimaanisha nini?

Raza: Ndiyo. Wanaweza kuumiza Taifa. Kwanza nataka kusema hivi kwa Watanzania na nikiambie hivi Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama changu kwamba kundi haliongozi nchi. Na halitoongoza nchi, kama kuna watu wanafikiria kuna kundi litaweza kuongoza nchi hao wanafikra…wana ndoto za Abunuwas.

Huwezi kufika pahala ukasema kundi liongoze nchi. Sasa katika mazingira kama haya Chama Cha Mapinduzi ndicho kinaongoza Serikali, kina ridhaa ya wananchi na wananchi ndiyo sisi wapiga kura.

Kwa hiyo huko kwenye ngazi ya chini kabisa kwenye chama wananchi bado wana imani na chama, nikiwamo mimi, na tunaona ni kama chama ambacho hakina tabaka za kikabila, rangi wala jinsia.

Sasa asije mtu akafikiria na akajiona ni bora kwa sababu tu kawa kiongozi mwandamizi. Akajiona bora zaidi ya wenzake. Fikra hizi sasa lazima  ziondoke.

Haya mambo yanayofanyika yanakera sana. Sisi leo tunasema na, si mimi pekee bali Watanzania karibu wote, kwamba kama angelikuwapo Mwalimu Julius Nyerere haya yote yasingetokea.

Raia Mwema: Mambo gani hasa unadhani yasingetokea kama Mwalimu Nyerere angekuwapo?

Raza: Haya yote…suala la EPA, Dowans, Richmond na mambo mengine. Hivi leo mtu anachota pesa mabilioni, anakwenda kuchota tu halafu yule anayeshuhudia (mtendaji wa kawaida) hana fedha ya kumlipia mwanawe shuleni. Halafu wanalalamika siri za Serikali zinavuja. Sasa wewe unachota bilioni nane, 10 halafu mimi sina pesa za kulipia pango eti unalalamika siri za Serikali zinavuja, hapana bwana hii haiwezekani. Unajua urafiki katika nchi usiwepo. Tusiweke urafiki katika nchi.

Leo mimi nashangaa viongozi na watendaji wengine wanalalamika siri zinavuja, hivi unachota bilioni 100, bilioni saba mimi pango na ada ya mtoto sina, sehemu nyingine za nchi hakuna huduma ya maji, shule nyingine hazina madawati. Watoto wanakaa chini, mbavu zinawauma, wewe unachota mabilioni halafu unalalama siri zinavuja.

Sasa mimi nafikiri katika hili tumefika wakati, kwanza sasa hivi CCM kinateremka kilima, hakipandi, tunataka kwenda kwa wananchi kupata tena ridhaa, Mwenyekti wangu Rais Jakaya Kikwete inabidi sisi wanachama twende naye kuomba kwa wananchi tuongoze tena nchi.

Raia Mwema: Kwa mujibu wa maelezo yako, unaonekana huridhishwi na mambo ndani ya CCM?

Raza:  Mimi nazungumza ki-ujumla. Nasema hivi, kuna viongozi wa upinzani huko nyuma walijaribu kutafuta kundi ili waongoze nchi na mpaka leo wanautafuta urais lakini hawajaupata.

Mimi Zanzibar nikisema kundi langu hili la Kusini au Kaskazini je, hawa wa Magharibi au Mashariki nitawafanyaje? Kwa hiyo, tujue kuwa tupo madarakani kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wote.

Kwa sababu, sheria ni sheria hakuna anayeweza kupanda juu ya sheria. Nasema kweli wafanyabiashara tupo sote na wengi…lakini si kila anayepepesuka ni mlevi.

Raia Mwema: Unazungumza kwa mafumbo mno. Umesema si kila anayepepesuka ni mlevu…hiyo maana yake nini?

Raza: Kwa sababu tukiacha haya ya EPA na mengine, kuna pesa nyingi hazijadaiwa kutoka kwa wafanyabiashara. Kuna pesa za OGL, Import Support, pesa za chakula zinazokopwa na miradi mingine mingi.

Lakini sasa utakuta mtu kazikusanya kwa ubinafsi wake mabilioni kwa mabilioni huku wananchi wakiwa na umasikini, wanahitaji huduma za msingi za maji, umeme na barabara. Halafu tunasema Tanzania ni nchi masikini ndiyo…sawa nchi masikini lakini sisi wenyewe tunajisimamia vipi?

Leo kila unakokwenda katika uchaguzi mtu anakwenda na makatoni ya pesa. Mfano, mtu anatumia milioni 400 hadi 500 katika uchaguzi ili ashinde, sasa mimi mfano ikiwa mtu anatumia hizo pesa huyo ana lake kwa sababu mwisho wa siku anataka kujilipa.

Kwa hivyo, katika hali hii lazima tuwe wakweli na sheria ifanye kazi yake. Lakini mtiririko mzima huu wa kulazimisha mambo tunaouona leo si mzuri na ni aibu sana kwa nchi na mimi nasema bahati nzuri Watanzania ni watu wavumilivu sana.

Raia Mwema: Kulazimisha mambo kama yapi hasa?

Raza: Kulazimisha mambo kama Dowans kwa mfano, mpaka Spika anatoa ushauri wa kuheshimu sheria sasa bado maofisa watendaji wanakuja juu kumpinga. Ni lazima hapo kuna mchinja ng’ombe.

Kwa hivyo mimi nafikiri bado hata hawa wabunge wanaojitoa mhanga tukawaombea dua maalumu. Unajua mambo yetu, hata katika safari zao wawe waangalifu sana, mimi nawaombea sana kwa sababu naona ule uzalendo wao, hata katika kula chakula anapoalikwa mbunge mhusika awe mwangalifu.

Ni watu wachache waliojitolea mhanga kuipenda nchi yao kwa hiyo ni lazima tuwe na uchungu na nchi, mambo haya ni lazima yafanyiwe kazi na huu mtikisiko ambao umetokea huu… mtikisiko najua mtikisiko wa vyombo vya habari hasa waandishi nimeuona, lakini kama hatukupiga kelele na hasa Bunge, mambo haya hayatafutwa, hayataondoka.

Raia Mwema: Kwa hiyo unasema kama si Bunge nchi ingekuwa pabaya kabisa?

Raza: Kabisa. Nchi ingekuwa pabaya sana. Nafikiri watendaji kama wanataka kuvaa kanzu nzuri, basi hiyo fulana yao ya ndani waioshe isitoe harufu. Lakini usivae kanzu una fulana inatoa harufu ndani au unavaa koti shati yako inatoa harufu ndani. Kwa hiyo kama unataka kuvaa kanzu basi fulana yako isafishe na kama ni suti pia shati yako isafishwe.

Ninachotaka kusema mimi ni kuwa suala la uongozi ni la mpito. Hapa alikuwapo Mwalimu Nyerere kaondoka nchi ipo, kaja mzee Mwinyi (Ali Hassan) kaondoka nchi ipo, kaja Mkapa (Benjamin) kaondoka nchi ipo, kaja Kikwete atamaliza lakini nchi itabaki. Naomba Watanzania tumuunge mkono Rais Jakaya Kikwete kwa kusimamia maadili na kuongoza Taifa. Tumsaidie kama mwenyekiti wa CCM ili atekeleze majukumu aliyopewa na wananchi.

Raia Mwema: Wana-CCM wengi mmekuwa mkitoa wito Rais Kikwete asaidiwe, kuna dalili gani mlizobaini. Je, hana msaada wa kutosha?

Raza: Nasema, Kikwete hajapewa majukumu ya urais na kikundi, kapewa na wanachama na wananchi wote, tunataka amalize muda wake ili heshima yake ibakie na ndivyo tunavyoamini hivyo.

Kwa sababu amefanya mambo ya ujasiri tayari, kama si Kikwete haya mambo mengine yasingekuja, lakini yeye kwa sababu ameunda tume mbalimbali ameonyesha kufungua zaidi milango ya demokrasia, uhuru wa vyombo…kwa hivyo inafaa nasi Watanzania tumuunge mkono katika hili.

Raia Mwema: Katika CCM mambo hayajakaa vizuri na Kikwete mwenyewe hotuba zake zinaonyesha kuwa hakuna umoja. Unasemaje na hasa ukitazama Uchaguzi Mkuu mbele yenu.

Raza: Unajua matatizo tunayo sisi wakereketwa au wapambe. Panapokuja uchaguzi, kwa mfano, kila mgombea anakuwa na wapambe wake au kila mgombea anakuwa na kundi lake, kwa mujibu wa Katiba hiyo inaruhusiwa. Lakini uchaguzi  unapomalizika mambo hayo yanakwisha.

Mfano huku Bara walikuwapo akina Profesa Mark Mwandosya, Frederick Sumaye, Dk. Salim Ahmed Salim na Kikwete. Mungu ndiye anayepanga Rais, kwa hivyo Mungu akajalia Kikwete akawa mgombea.

Sasa kuna kasumba za hawa wapambe wanaamini kwamba wao ndiyo wameshinda, lakini hayo ni maono potofu… ni kasumba tu, kilichoshinda ni chama, kwa sababu wanachama hawaongezeki kwa hivyo hao wapambe ilibidi wawe pamoja sasa. Lakini unakuta kuna watu si wabunifu, wanapeleka majungu kwa Rais kuwa kuna watu wanakupiga vita.

Lakini mimi nasema ukitaka kumsaidia Rais usimpelekee sifa zake kutoka mitaani mpelekee yale magumu wanayolalamikia wananchi huko mitaani.

Mimi nimefanya kazi na Rais wa SMZ nikiwa mshauri na nimemsaidia mambo mengi tu si michezo, lakini hata siku moja sijaenda Ikulu kumwambia mambo yote yanaenda sawasawa tu. Mazuri yake nilikuwa namwachia mwenyewe yale ambayo wananchi walikuwa wanaguna mitaani nilikuwa namwambia mzee huko mitaani wananchi wanaguna….maji hakuna.

Rais ana wasaidizi, hawezi kufanya kazi peke yake. Inabidi awe na watu wabunifu na waaminifu. Lakini  sasa unakwenda unamtisha Rais, unamweleza unajua bwana hawa kina Raza wanakupiga vita, hawakutaki, hawakusaidii wanakuchochea, unatia majungu.

Matokeo yake, kwa kuwa anawaamini kwa yale ambayo wanamueleza inaweza kuwa siku moja akawa Rais asiye na busara wala hekima, anaweza akakumaliza tu.

Kwa hiyo nafikiri kuna busara lazima zitumike kwa sababu kiongozi yeyote katika nchi bila kupangiwa na wenzake hawezi kuongoza nchi.

Rais ana mamlaka yake ya kuamua mambo, lakini Rais huyo huyo ndiye bosi, hawezi kukaa akaandika speech, akakaa akapanga mambo yeye tu, anatakiwa awe na watu waadilifu wakakaa wakamsaidia.

Mimi nataka nikuhakikishie Rais Kikwete ninavyomjua mimi kama mwanamichezo kwa kipindi kirefu ni mtu mwenye hekima, busara na mvumilivu na anapenda kusikia. Kwa hivyo, mimi nafikiri kuna haja katika hili kumsaidia vya kutosha kwa sababu tunateremka kilima na tayari jua limetua na jua likitua maana yake kiza kinaingia.

Kwa hivyo mimi nasema nawaomba wafanyabiashara kulipa hizi fedha walizofaidika nazo za OGL, Import Support na za chakula walizokopeshwa, zikasaidie wananchi. Leo hii asilimia kubwa ya Watanzania hawakidhi milo mitatu kwa siku. Ndiyo! Napenda nikuhakikishie kuwa kuna watu wanashindia uji tu.

Sasa tunakwenda sehemu leo madawati hakuna, maisha bora hayajatimia sawasawa, kasha unasikia mtu anachota mabilioni mengi peke yake, nafikiri kwenye haya yote watu wanapotoa vilio vyao walimu au watu wa afya, wenye madai wanadai vijipesa kidogo tu, wanagoma au kuandamana, wameona uchungu kwamba mtu amechota mabilioni lakini mwalimu anaona kuwa yeye miaka mitatu anadai elfu zake 70 tu, hajalipwa. 

Unajua lazima ujiulize kwa nini katika historia ya Tanzania kunaibuka matukio mfululizo kama migomo mara ya walimu au madaktari. Si kugoma tu, wameona kwamba hazina kumbe ina pesa ya kutosha…mimi nadai shilingi 75,000 au 80,000/-… mishahara yangu haikufika lakini kuna huyu mtu amechota bilioni. Sasa Serikali na vyombo vyake wakae wajiulize.

Lakini badala yake wakati mwingine kunakuwa na majibu ya mkato katika hili kwamba wapinzani hao ndiyo wamewaambia walimu wagome, ina maana gani hii? Kwanza nasema Tanzania hakuna upinzani.

Kama Tanzania kungelikuwa na upinzani bora, imara na wa kweli CCM isingelibakia…believe me, kama tungelikuwa na upinzani uliokuwa wa ujasiri loo! Pale hata lile Bunge lisingeweza kumalizika.

Kwa hivyo tushukuru kwamba CCM chama changu hatuna upinzani, lakini CCM tulichokuwa tunakipata walio wengi kwenye grass root wanatukubali na wanaendelea kutukubali.

Raia Mwema: Lakini mkiendelea hivyo watawakataa hata hao walalahoi mitaani.

Raza: Sikatai. Ndiyo maana nilisema unapotaka kusema ukweli kwanza wewe mwenyewe uwe mkweli. Hakuna binadamu mkamilifu lakini ni vizuri tukajenga utamaduni wa kurejea katika historia.

Nchi yetu sasa ina pengo kubwa na hii ni hatari wakati wowote inaweza kufikwa na machafuko. Ni mbaya sana yaani pale pengo la matajiri na masikini linapozidi.

Raia Mwema: Kwa kuzingatia maelezo yako, ni dhahiri kuwa kuna hali ya kutowajibika. Unashauri nini kifanyike?

Raza: Mimi ninachosema ni tuwe wakweli kwa sababu hiki chama ni cha wananchi si cha watu fulani. Urafiki katika nchi…mimi sina msalie, Zanzibar kwa mfano, huko sina urafiki na mtu hata akiwa ndugu yangu…no way! Hakuna msalie, ile ni alama yangu bwana. Urafiki katika nchi hapana.

Sasa katika hali kama hii chama kikae, Serikali ikae kitako kutazama mambo haya kwa kina. Kwa sababu umeona hivi sasa wabunge wa CCM kwanza sipendi kuingia upande wowote nataka kuzungumzia masuala yanayohusu nchi na si kikundi fulani…hiyo haitusaidii.

Wabunge wa CCM wanalumbana na haya malumbano wakati mwingine yanahusu pesa za walipa kodi, kwa hiyo mimi hofu yangu ni uongozi wa juu wa chama, huku chini chama changu hakijaharibika lakini huku juu ndiko panapotaka kutengenezwa.

Katika chama hakuna ‘bwana’ wala hakuna CCM A wala B, kama mtu anafikiria hivyo basi aondoke.

Huko CCM juu watu wakae kitako, umaarufu wa mtu unatokana na chama na si mtu. Huko ndiko kumeharibika. Nafasi ipo watu wazoefu pia wapo, sasa warekebishe huko juu.

Raia Mwema: Kwa mfano ukiambiwa utaje mambo mawili ambayo unadhani yanatakiwa kurekebishwa sasa, utajibu nini?

Raza: Mimi nafikiri mfano huu wa Dowans, Bunge limetoa ushauri wake suala hili liachwe ofisa waandamizi wametoka wanataka kununua Dowans, lakini tayari Richmond imetoka kuwa Dowans.

Hadi Spika wa Bunge, ambaye ni mwana-CCM anatoka kusisitiza ushauri anasema hapana sasa wote hawa wanaovutana ni CCM hakuna Chadema wala CUF. Kwa hiyo tatizo lipo uongozi wa juu wa CCM.

Kuna mbunge anamwambia mbunge mwenzake wa CCM…bwana hapo ulipofika tulizana kuna mambo nikizungumza patakuwa hatari nchi inaweza kuingia katika zahma. Sasa hii ni one system, hakuna Chadema, CUF wala TLP. Kwa hiyo katika hali hiyo tatizo lipo na kama tatizo lipo tusilifungie macho tu.

Binadamu anaweza kukosea lakini watu wakae ndani wakosoane…aah..Raza hee mwendo wako huu bwana hapana unaumiza nchi bwana…sasa haya mambo bwana acha.

Kama nilivyosema ukishafika pahala mmoja anasema huyu mmalize ndiyo yale ya Zanzibar yalipotokezea ufa.  Tulipoingia wana-CCM sasa wakaanza kubaguana..aah huyu Raza kundi la Salmin (Dk. Salmin Amour), huyu kundi la Amani (Aman Abeid Karume) kumbuka wote ni wana-CCM.

Kwa hivyo unatazama pale Raza aah…huyu ni wa Salmin unatazama kwa namna hiyo. Sasa mazingira kama haya unaposema kwamba unayaacha, na yanapozidi kuimarika yatakapolipuka huwezi kuyazuia.

Nataka kuwasihi waandishi wa habari bora wale mhogo na viazi lakini waweke mbele nchi yao. Bora wale mhogo lakini wajiamulie mambo yao. Nasi Watanzania bora tule mhogo na viazi lakini tujiamulie mambo yetu wenyewe.

Mtu anakuja anakwambia mimi natoa milioni 600 au 700 katika uchaguzi…huyu ana lake…atakuumiza. Nilisema mimi katika uchaguzi mwaka 2005, nendeni mkasome magazeti nilisema bwana hizi pesa zinazotoka hawa wanatakiwa kuja kuzilipa na watakapoanza kuzilipa watakuwa wanaamuru, sasa leo ndiyo haya.

Wakati leo kuna sehemu za skuli zinahitajika 200,000/- au 300,000/- lakini upande mwingine watu wanaiba mabilioni. Hizi pesa zilizoibwa zikipatikana sisi leo tunamaliza Ilani yetu ya uchaguzi tunamaliza matatizo yetu yote ya mikoa yote, suala la afya, zahanati na maji…matatizo yote.

Raia Mwema: Turudi nyuma kidogo wakati ule ukiwa mshauri wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Salmin Amour  nakumbuka ulikuwa wakati mwingine ulikuwa ukiisaidia kifedha SMZ lakini sasa hivi inaonekana kama haihitaji msaada wowote wa fedha kutoka kwa wananchi. Je, unaiona kwamba Serikali sasa imeimarika kiuchumi?

Raza: Nafikiri mjadala kuhusu uchumi wa Zanzibar tufanye katika mahojiano ya wakati mwingine, lakini nitakujibu kwa ufupi tu kwamba mimi nikiwa mshauri wa Rais,  Zanzibar iliwekewa vikwazo mpaka sisimizi. Dunia nzima ilituwekea vikwazo hadi Tanzania Bara na kama utakumbuka kuna waziri mmoja wa Muungano….mimi kumbukumbu ninazo aliwahi kusema wakati akipokea msaada alisema huu msaada ni wa Bara tu si wa Zanzibar.

Sasa turejee katika masuala tuliyokuwa tukizungumza. Kwa hivyo sasa hivi vyombo vya habari, Watanzania wote kuna haja ya kuendeleza mijadala hii ya ufisadi mpaka tujue mwisho wake…sheria…sheria hakuna mtu anayeweza kwenda juu ya sheria.

Kwa hiyo hata kwetu sisi CCM ni vema tukapata ufumbuzi kabla ya Uchaguzi Mkuu mwakani. Ee kwa sababu tunataka kurudi kwa wananchi najua kuna katika mambo ya Mahakama huwezi kuingilia lakini katika yale mambo ambayo unaweza kuyafanya tuyakamilishe kabla ya kuingia katika uchaguzi.

CCM inataka kurejea nataka kuwaambia wananchi ilikuja 2005 na mgombea Rais Kikwete obvious ndiye atakayekuwa mgombea…

Raia Mwema: Zipo habari kuna njama za kutaka kumng’oa, una uhakika gani?

Raza: Hiyo ni demokrasia lakini nasema mimi naona watu bado wana imani naye. Kikwete ameonyesha demokrasia na ni msikivu…ndiyo Kikwete ni msikivu ameonyesha ushupavu na ustahimilivu wake.

Raia Mwema: Lakini wapo wanaoamini kuwa amekuwa mzito wa kuchukua hatua hata kwa mambo yaliyo wazi?

Raza:  Nasema unajua kwa sababu katika hali kama hiyo unatakiwa  uwe na wasaidizi wenye busara zaidi wakusaidie ili kufikia uamuzi wenye tija kwa Taifa.

Raia Mwema: Kama unakuwa mzito wakati muda unazidi kwenda na uchaguzi umekaribia?

Raza: Unajua haya mambo si mambo madogo. Haya ya ufisadi yalitakiwa kukamilishwa mapema ili twende kwenye Ilani yetu ya uchaguzi. Sasa leo sisi badala ya kuzungumzia ilani ya uchaguzi tunajadili ufisadi ambao umetokana na ubabe wa viongozi waliopita.

Hata sehemu nyingine Afrika kuna viongozi wengine wamebadili hadi mwendo, wanatembea wakijiona wao ndiyo wao hii yote inatokana na ubabe tu na mimi namwomba Rais Kikwete, Mungu amsaidie asibadilike kuwa mbabe.

Kama hatukuwa wakweli na hatutakuwa wa kweli hatuwezi kufika mahala tukapata tija inayostahili kwa hivyo unapomwambia mwenzako kwa kumnyoshea kidole je nawe ni mkweli? Sote tuwe wa kweli katika kila suala.

Ali Hassan Mwinyi alikuwa waziri, Benjamin Mkapa alikuwa waziri na Kikwete alikuwa waziri pia. Unapokuwa waziri unakuwa mtu huru kidogo lakini unapokuja kuwa  Rais wewe ni Rais tena hata kama Raza ni swahiba wako Rais maana yake unawajibika kwa wananchi wote. Kikwete si Rais wa CCM tu ni Rais wa Watanzania wote na Tanzania yote bila kujali itikadi za kisiasa na anaweza kuingilia suala lolote.

Maana kuna watu wengine ni tatizo, hili hawataki kuliona…mimi nilipokuwa Zanzibar nimekuwa nikisema lakini wapo wengine wanasema yule si wetu…CUF yule, lakini kitu kilichonisaidia mimi ni kwa sababu ya msimamo wangu.

Haya ndiyo matatizo yetu unapokosoa wanakuona kama mpinzani. Tufike mahala tuzungumze masuala yetu hasa matatizo. Kwa hiyo  nafikiri hapa wenye jukumu zito la kurekebisha mambo ni Kamati Kuu ya CCM na Halmashauri Kuu.

Kamati Kuu na Halmashauri Kuu inaweza kuweka mambo haya sawa.

Raia Mwema: Lakini Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ni vyombo visivyo nadhifu, kuna watuhumiwa wa ufisadi na maovu mengine na wengine wanazozana?

Raza: Sasa ndiyo nasema lazima tufike mahala tuwe wa kweli. Unajua binadamu mtu ukifika mahala umekwishatuhumiwa kwa ufisadi ni vizuri mimi kwa ufahamu wangu ujiuzulu kwa muda ndiyo uongozi mzuri huo na ndiyo ustaarabu unaotakiwa. Kama bado wapo viongozi wanachunguzwa na vyombo mbalimbali wajiuzulu.

Nafikiri kujiuzulu ni jambo muhimu …ni kukipa chama nguvu kama kuna wajumbe wapo Kamati Kuu wanazongwa na tuhuma wajiuzulu ili kukipa nguvu chama…sawa kwa sababu hujahukumiwa huwezi kuitwa fisadi moja kwa moja lakini jiuzulu, ukipe chama nguvu na heshima mbele ya wananchi. Kipe chama heshina, tatizo liko wapi? Mambo yakirekebishwa utarudi!

Lakini sasa watu wazima nchi hii…. mimi nasema sisi wananchi tunastahili kupongezwa sana kwa uvumilivu, amani haiendi bila uvumilivu wananchi ndiyo wanailetea nchi amani kutokana na uvumilivu wao. 

Kwa hivyo inafaa tukajiuliza hapa tulipofikia tumefikaje. Niseme kwamba watu wanaokwenda kumwona au kuzungumza na Rais Kikwete waende na mapendekezo ya ufumbuzi wa matatizo yaliyopo.

Tumsaidie Mwenyekiti wa chama, tusiende na matatizo tu twende na ufumbuzi. Kwa hiyo Watanzania tunakata viongozi wawe na ufumbuzi lakini si unakwenda kumwambia mwenzako tatizo… yeye atatatua vipi? Na mimi naona Waziri Mkuu Mizengo Pinda mpaka sasa katika takwimu yeye amekuwa na uwazi sana katika utendaji.

Kwa hivyo haya mambo mengine ambayo yaliachwa bungeni kutokana na muda mimi nafikiri Bunge lichukue muda wake haya yote yamalizwe.

Kwa sababu unasema unakaa Bunge wiki tatu halafu unaleta jambo zito siku moja kabla halafu unasema baadaye. Sasa baadaye maana yake nini, tumalize mambo kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Mimi nafikiri Bunge liwe la wazi kwa sababu sasa hivi Watanzania tegemeo lao ni Bunge. Hawana tegemeo jingine sasa hivi.

Raia Mwema: Unasema tegemeo lao ni Bunge pekee, vipi kuhusu Serikali…huna imani nayo?

Raza: Aah ! Bunge ni Serikali kwa sababu wabunge wote wamechaguliwa moja kwa moja na wananchi kwa hivyo mimi nasema Bunge ndiyo nchi kwa hivyo Watanzania wote tunaamini, na matumaini yetu ni Bunge….najua kuna wengine wametishiwa lakini naawambia wabunge wetu majasiri walinzi wao ni Mwenyezi Mungu.

Na mimi nafikiri sauti zao zinasikika, na walio wengi ndiyo watakaorejea pale. Leo wabunge majasiri tunawajua kwa majina, wabunge ambao wameweka historia. Kama si wabunge haya mambo yasingefichuka.


Simu ya mkononi (simkono): 00 + 255 + 787 643151


1 comment:

Anonymous said...

Teta Raza tena.....