Wednesday, April 22, 2009

Tanzania inapotegwa

kwa ardhi yake



SIKU zote mwenye tamaa, mara nyingi uwezo wake wa muono wa mambo haulengi mbali. Anachokiona katika hilo analolitaka ni kupata tu hicho anachokihitaji tu. 

Hamu ya jambo au kitu humfanya awe kipofu na kiziwi. Haoni wala hasikii ingawa macho na masikio anayo. Hata wengine wakimuonyesha au kumwambia, hatilii maanani. 

Mtu anayetaka au kukamia jambo, kwake hakuna kingine isipokuwa kukisaka akitakacho kwa hali yoyote ile, hata kama kitu hicho kiko katika miliki ambayo si yake. Njozi zake huona anayekimiliki hastahiki na anapaswa kufuata utashi wake. 

Hali hiyo ndiyo inayokabili mustakabali wa Shirikisho la Afrika Mashariki linalotarajiwa kuundwa miongioni mwa nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki. Nchi hizo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.

Lakini kinachoshangaza katika mchakato huo wa kuelekea Shirikisho, baadhi ya nchi kwa hamu na utashi wao wanadiriki kutoa sharti la kuundwa kwake. wananataka kuasisiwa kwa umoja huo kufanyike kwa sharti kuwa suala la ardhi lihusishwe. Inakuwaje? 

Ni ile ile tamaa. Nchi zinazoshinikiza hilo za Kenya na Uganda, zinataka Tanzania ikubali ardhi yake iwe huru kwa yeyote kati ya wananchi wa nchi wanachama wa jumuia, ili raia wa nchi yoyote mwanachama akikaa kwa muda maalumu awe na haki ya kumiliki ardhi. 

Hilo halizungumzwi kwa bahati mbaya. Nchi hizo zina malengo na nia ya kweli ya kutaka kupata ardhi nje ya nchi zao. Kwao, ardhi imekwisha, yote inahodhiwa na kumilikiwa watu wachache. Wananchi wengi wanyonge hawana ardhi. Sera za ardhi za nchi hizo, zinawapa nafasi matajiri wachache kununua na kumiliki ardhi kubwa, hali ambayo kwa asiye nacho ndoto za kumiliki ardhi, hanazo na hata kama atakuwa nazo hawezi kuipata kwa sababu walio nayo hawaitoi. 

Baada ya kufikiri kwa muda mrefu, wameona kati ya nchi zote wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Tanzania pekee ndiyo yenye ardhi kubwa tupu ambayo miliki yake iko mikononi mwa serikali. 

Kutokana na ukubwa wa ardhi hiyo, suala la kumiliki ardhi katika Tanzania si jambo la kumuumiza mtu kichwa. Awe na uwezo au asiwe na uwezo. 

Wenye uwezo wanaruhusiwa kukodishwa ardhi na kuitumia kwa shughuli zozote wazifanyavyo. Iwe shughuli za kilimo, viwanda, ufugaji au ujenzi. 

Mnyonge wa Tanzania hadi sasa ana uwezo wa kumiliki ardhi kwa kuiomba tu kupitia serikali yake ya kijiji na akamilishwa kuitumia hadi ukomo wa maisha yake, mradi tu anaiendeleza. 

Katika nchi nyingine za Afrika Mashariki hilo linaonekana kama ndoto, na ndipo walipopiga Bongo na kutafuta njia ili raia wao nao waweze kumiliki ardhi nchini Tanzania. 

Lakini wakati wao wanashinikiza hilo, Watanzania haiwezekani kupata ardhi katika nchi zao kutokana na mfumo na sera zao za miliki ya maliasili hiyo. 

Achilia mbali ardhi, wakati raia wa nchi kama Kenya na Uganda ni rahisi kupata ajira nchini Tanzania, ni Watanzania wangapi wanapata nafasi ya kufanya kazi nchini humo wakati sifa na vigezo wanavyo? 

Dhana ya kuanzisha shirikisho imekuja raia wa nchi hizo wawe na uhuru wa kuendesha shughuli zao za kiuchumi na kijamii katika nchi hizo bila bughudha. 

Kinachopaswa kufanyika ni kuanza na masuala hayo kwanza ili ionekane ushirikiano huo utakwenda vipi na kila nchi itafaidika vipi, huku ikilinda haki za raia wake kuona wananufaika sawa na umoja huo. 

Ikiwa hilo halijadhihirika na kuridhisha kila upande, hoja ya kutaka suala la ardhi kuwa moja ya sharti ya kuanzishwa Shirikisho ni kuitega Tanzania, kwa sababu haitakubali suala hilo wakati haina hakika ya raia wake kuweza kupata ardhi katika nchi zingine wanachama.

Kutoka gazeti la Uhuru.

No comments: